Habari za Kitaifa

Mafuta yanayochimbwa Turkana yaibua mvutano mkali Pwani

Na JURGEN NAMBEKA, VALENTINE OBARA January 23rd, 2026 Kusoma ni dakika: 3

VIONGOZI katika eneo la Pwani wamegawanyika kuhusu ni bandari ipi kati ya Mombasa na Lamu itakayoshughulikia usafirishaji wa mafuta yanayochimbwa Turkana pindi zoezi hilo litakapoanza rasmi.

Viongozi wa Mombasa wanataka kiwanda cha kusafisha mafuta cha Changamwe kilichofungwa kitumike kwa biashara hiyo, ilhali wenzao wa Lamu wanataka mpango wa awali wa kujenga bomba la mafuta kutoka Lokichar hadi Bandari ya Lamu utekelezwe kikamilifu.

Wakizungumza katika mkutano wa kushirikisha umma ulioandaliwa na Kamati ya Pamoja ya Bunge kuhusu Nishati katika Kaunti ya Mombasa, viongozi wakiungwa mkono na wakazi walisema kufunguliwa upya kwa kiwanda hicho kutasaidia pia kuongeza thamani ya mafuta ghafi.

“Ikiwa tutaendelea kufunga viwanda hivi, tunawanyima watu wetu fursa za kujiendeleza. Watu wasipokuwa na ajira, viwango vya uhalifu huongezeka, uvivu huongezeka na watu wanakuwa wazembe,” alisema Mbunge wa Changamwe, Bw Omar Mwinyi.

Hata hivyo, viongozi na wakazi walitoa wito wa tahadhari kuhusu mazingira na afya, wakieleza changamoto za awali kama vile utoaji wa hewa yenye sumu zilizoharibu mabati na kusababisha matatizo ya kupumua.

“Nataka kuwahakikishia kuwa nimezingatia mapendekezo yenu, na kwa kura yangu moja, nikiona kuwa ufufuzi wa kiwanda cha mafuta cha Changamwe na ajira kwa watu wa Changamwe haviko kwenye pendekezo, nitapinga,” alisema Seneta wa Nairobi, Bw Edwin Sifuna.

Katika Kaunti ya Lamu, viongozi walitoa wito mradi wa uchukuzi kati ya Bandari ya Lamu-Sudan Kusini-Ethiopia (LAPSSET) utekelezwe kikamilifu, wakisema ucheleweshaji umeathiri uwezo wake wa kiuchumi na jukumu lake katika kusafirisha mafuta ya Turkana hadi soko la kimataifa.

“Hatujatumia kikamilifu rasilimali zetu za asili, lakini hatupaswi kukosa fursa hii ya bomba la mafuta,” alisema Gavana wa Lamu, Bw Issa Timamy.

Mpango wa awali wa ulikuwa umependekeza ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Lokichar hadi Bandari ya Lamu kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi.

Hata hivyo, mpango mpya uliowasilishwa Bungeni mnamo Septemba 2025 na kampuni ya Gulf Energy, ambayo ilinunua rasilimali zote za kampuni ya Tullow, ilipendekeza usafirishaji wa mafuta kwa malori hadi Mombasa.

Kampuni hiyo ilitaja gharama kubwa na muda unaohitajika kujenga bomba, pamoja na ukosefu wa reli kutoka Turkana ambayo ingekuwa mbadala bora, kama sababu kuu za kuchagua usafiri wa barabarani.

Gulf Energy ilipendekeza mpango wa utekelezaji kwa awamu unaoanza na uzalishaji wa mapipa 20,000 ya mafuta kwa siku yatakayosafirishwa kwa malori hadi Mombasa ili kuharakisha uingizaji wa mafuta sokoni.

“Katika awamu ya awali, mafuta ghafi yatasafirishwa kwa barabara hadi kituo cha Kenya Petroleum Refineries Limited (KPRL) iliyo Changamwe kwa ajili ya kusafirishwa nje kupitia Kituo Kipya cha Mafuta cha Kipevu. Chini ya mpango huo, uzalishaji unatarajiwa kuanza Desemba 1, 2026.

“Uzalishaji utabaki kuwa mapipa 20,000 kwa siku kwa miaka minne ya kwanza, kabla ya kuongezeka hadi mapipa 50,000 kwa siku pindi tu miundomsingi muhimu ya reli itakapokamilika,” nakala hiyo ikasema.

Mbali na gharama, uzito wa mafuta yanayochimbwa Turkana pia ulitajwa kuwa changamoto katika usafirishaji wake kupitia bomba.

Gulf Energy ilieleza kuwa, mafuta hayo huganda katika nyuzi joto 45°C na huanza kutengeneza nta katika 69°C, hivyo lazima yahifadhiwe juu ya viwango hivyo wakati wa usafirishaji.

Kwa kutumia usafiri wa barabara, kampuni hiyo ilipendekeza kuwa, mafuta yatapakiwa kwenye malori maalumu yanayohifadhi joto katika eneo la uzalishaji Lokichar kwa takribani nyuzi joto 80°C na yanatarajiwa kufika Mombasa yakiwa na joto lisilopungua 69°C.

Kenya ilifanya majaribio ya kusafirisha mafuta ghafi kwa malori kutoka Lokichar hadi Mombasa mwaka wa 2018, zoezi lililozinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Wizara ya Nishati hivi majuzi ilifichua kuwa, mafuta hayo yaliuzwa kwa dola milioni 28.34 (Sh3.65 bilioni) kwa kampuni za Glencore Singapore Pte Ltd na ChemChina UK Ltd.

Mbunge wa Lamu Mashariki Ruweida Obo aliambia kamati ya pamoja ya bunge kuwa mabomba ni nafuu zaidi katika usafirishaji wa mafuta, akionya kuwa kubadilisha mpango wa awali utakuwa pigo kubwa kwa Kaunti ya Lamu.

“Kusafirisha mafuta kupitia bomba hugharimu takribani dola tano kwa pipa, ikilinganishwa na dola ishirini kwa barabara. Kuondoa kipengele chochote kunaleta hatari ya kufanya jamii zilizotengwa Lamu na nchi nyingine za Afrika Mashariki zikose imani kwa serikali,” alisema.

Mbunge wa Embakasi Kusini, Bw Julius Mawathe, ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo, alifafanua kuwa lengo la kukutana na umma lilikuwa kusikiliza na si kuamua kuhusu mpango utakaotumiwa kusafirisha mafuta hayo.

Hata hivyo aliongeza kuwa, Kenya lazima ikamilishe mradi wa LAPSSET, huku Ethiopia na Sudan Kusini zikiwa washirika wakuu katika kipengele cha bomba la mafuta.

Maafisa wa Mamlaka ya Maendeleo ya Ukanda wa Lapsset wakiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu, Bw Stephen Ikua, walisema upangaji ramani na usanifu wa bomba zimekamilika, huku ujenzi ndio ukisubiri kuanza.

“Bomba hilo halitahudumia tu mafuta ghafi ya Lokichar Kusini. Tunaweza kupata takribani dola 35 kwa pipa kwa kusafirisha mafuta kutoka Sudan Kusini, ambayo huzalisha mapipa 110,000 kwa siku lakini haiwezi kuyasafirisha kwa sasa kutokana na vita,” alisema Bw Ikua.