Habari za Kitaifa

Serikali yaagiza wakuu wa Sekondari Pevu kusajili wanafunzi wote Gredi 10

Na DAVID MUCHUI, LYNET IGWADAH January 22nd, 2026 Kusoma ni dakika: 1

WIZARA ya Elimu imewaagiza wakuu wa shule za sekondari pevu kuwapokea mara moja wanafunzi wote wa Gredi 10 walioteuliwa kujiunga na shule zao, bila kujali kama wana sare za shule au wamelipa karo.

Agizo hilo linafuatia amri ya Rais William Ruto aliyotoa jana, akiwataka machifu na wadau wote wa elimu kuhakikisha watoto wote wanaripoti shuleni kufikia leo Ijumaa.

Rais alisema serikali tayari imetoa Sh44 bilioni kama mgao wa kufadhili elimu, akisisitiza kuwa hakuna mtoto anayepaswa kunyimwa elimu kwa kukosa karo.

“Kuna fedha za kutosha kuhakikisha watoto wetu wanafundishwa muhula wa kwanza. Kila mtoto, awe na sare au asiwe nayo, na awe amelipa karo au la, anaripoti shuleni kesho (leo) asubuhi. Nataka machifu wote, manaibu machifu na maafisa wa utawala kuhakikisha kila mtoto anaripoti shuleni kwa sababu tumetoa fedha za kufundisha watoto wetu,” alisema Rais Ruto.

Rais alikuwa akizungumza mjini Meru wakati wa hafla ya kuzindua mpango wa kuwezesha vijana kujikuza (NYOTA).

Aidha, aliwaagiza walimu kuwaruhusu wanafunzi wanaohitaji msaada kuendelea kuvaa sare za shule za Sekondari Msingi wanapojiunga na Sekondari Pevu.

Mnamo Alhamisi, Wizara ya Elimu ilisema kuwa asilimia 92 ya wanafunzi wa Gredi 10 tayari walikuwa wameripoti shuleni.

Waziri wa Elimu, Bw Julius Ogamba, alitoa mwongozo kwa shule zote za umma akisema wanafunzi waruhusiwe kujiunga na Sekondari Pevu wakiwa wamevaa sare za Sekondari Msingi.

“Wakuu wa shule za Sekondari Pevu wanapaswa kuwapokea mara moja wanafunzi wote walioteuliwa kujiunga na shule zao. Hakuna mwanafunzi atakayezuiwa kwa kutolipa karo,” alisema Bw Ogamba katika mkutano na wanahabari jijini Nairobi.

Aliongeza kuwa wakuu wa shule wanapaswa kutumia ipasavyo fedha za mgao zilizotolewa Januari 2, 2026, huku wakiwapa wazazi na walezi muda wa kushughulikia majukumu yoyote ya kifedha.

Agizo hilo linajiri huku idadi kubwa ya wanafunzi wa Gredi 10 bado hawajaripoti shuleni. Takwimu za wizara zinaonyesha kuwa kukosa sare za shule ndicho kikwazo kikubwa zaidi.