Makala

Tulijaribu kuokoa maisha ya Walibora ikashindikana, daktari wa KNH aeleza jopo

Na RICHARD MUNGUTI January 23rd, 2026 Kusoma ni dakika: 1

DAKTARI mmoja katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) jana aliambia mahakama ya Milimani kwamba, msomi na mwanahabari Prof Ken Walibora alifariki kutokana na majeraha makubwa wakijaribu kuokoa maisha yake.

Dkt Stellah Rono aliambia hakimu anayechunguza chanzo cha kifo cha Prof Walibora kwamba, alifariki huku akiendelea kumhudumia.

“Mgonjwa ambaye alikuwa na majeraha makubwa aliwekwa katika chumba cha kuokoa wagonjwa akiwa bado hai ingawa alikuwa na majeraha makubwa,” Dkt Rono alisema.

Aliongeza kuwa walichukua hatua haraka kujaribu kuokoa maisha yake “lakini kwa bahati mbaya alifariki. Daktari huyo alieleza mgonjwa aliyefikishwa katika hospitali hiyo, awali alisajiliwa kama “mwanaume ambaye hakuweza kutambuliwa.”

Dkt Stella Rono akitoa ushahidi katika jopo la kuchunguza kifo cha mwanahabari Ken Walibora, Alhamisi, Januari 22, 2026. Picha|Richard Munguti

Utata kuhusu kifo chake ulizuliwa na ripoti ya upasuaji wa maiti iliyotolewa na mwanapatholojia mkuu wa serikali Johansen Oduor, aliyethibitisha kwamba kulikuwa na majeraha kwenye upande wa kulia wa kichwa, huku mkono wa kulia ukiwa umevunjika na damu kuvuja ubongoni.

Kulikuwa na jeraha la mkono wa kulia ambao ulionyesha kwamba alikuwa amedungwa kwa kisu. Ni madai haya yaliyomfanya kaka yake marehemu, Mwalimu Patrick Lumumba atoe wito kwa serikali ichunguze kwa kina na kujua kilichosababisha mauti ya nduguye.

Madai mengine ambayo yametolewa ni kwamba, Prof Walibora alikuwa ameelekea katika eneo la Muthurwa kusemezana na dereva wa lori aliyekuwa amsafirishie vifaa vya ujenzi nyumbani kwake katika Kaunti ya Trans-Nzoia.

OCPD wa Kituo cha Polisi cha Central, Bw Mark Wanjala,  alisisitiza kuwa uchunguzi kuhusiana na kifo cha Prof Walibora sasa umetwaliwa na maafisa wa DCI.

Mwandishi huyo maarufu anadaiwa kugongwa na gari katika barabara ya Landhies karibu na Soko la Muthurwa mnamo Aprili 10, 2020.

Uchunguzi unaendelea.