Msiharakishe ndoa na Ruto, Dadake Raila aonya
MWAKILISHI wa Kike wa Kaunti ya Kisumu, Ruth Odinga, amejiunga na mpwa wake, Winnie Odinga, kuonya baadhi ya viongozi wa chama cha ODM dhidi ya kuharakisha kuingiza chama hicho kwenye muungano na UD, akisema hatua kama hiyo inaweza kukiacha chama katika hali tata baadaye.
Bi Ruth aliwahimiza wanasiasa wa chama hicho kuzingatia kuimarisha miundo ya ndani ya chama na kuhakikisha utekelezaji kikamilifu wa ajenda ya vipengele 10 katika makubaliano ya aliyekuwa kiongozi wa ODM, marehemu Raila Odinga, na Rais Ruto kabla ya kuanza mazungumzo rasmi na UDA.
Aliongeza kuwa ODM inapaswa kuupa kipaumbele uthabiti wa ndani na kuzungumza kwa usemi mmoja kabla ya kuzingatia mpango wowote mpya wa kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.
“ODM haipaswi kuharakisha kuingia katika makubaliano ya muungano kana kwamba kuna dharura fulani. Mwaka wa 2027 bado upo. Hata kama ODM itakaa kimya, 2027 bado itafika,” alisema Bi Ruth.
Matamshi yake yanajiri wiki moja baada ya Kamati Kuu Simamizi ya ODM (CMC) kukutana Kilifi na kumtuma Kiongozi wa Chama, Dkt Oburu Oginga, kuanza mazungumzo na UDA.
Bi Odinga alizungumza Jumatano usiku katika mahojiano na kituo cha televisheni kinachotangaza kwa lugha ya kienyeji, takriban miezi mitatu baada ya kifo cha ndugu yake Raila na kifo kilichofuata cha dada yake, Beryl.
Ingawa alikanusha kuunga upande wowote ndani ya chama hicho – unaounga mkono au kupinga ndoa ya kisiasa na Rais Ruto – alisisitiza kwamba anabaki mwaminifu kwa mfumo wa Serikali Jumuishi ulioanzishwa na Raila.
Maneno yake yanafanana na ya mpwa wake, na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, (EALA) Winnie Odinga, ambaye akizungumza majuzi na wafuasi wake katika mtaa wa Kibra, Nairobi, aliwataka viongozi wa chama hicho kuzingatia maslahi ya umma badala ya maslahi binafsi.
“Tunachosema leo ni tulieni. Baba alifariki siku chache zilizopita. Haraka ni ya nini? Tuzungumze kwanza na tuchukue hatua ya pamoja,” alisema Winnie.
Jumanne, Bi Odinga alichochea mjadala zaidi kwa kudai kuwa kiasi kikubwa cha pesa kinatumika kuharibu ODM, jambo alilodai linapaswa kuwa kero kwa wafuasi.
“Tunaona hali ambapo pesa nyingi zinazunguka, na kuna dalili za jaribio la kuingiza chama cha ODM katika muungano, zaidi ya mwaka mmoja kabla ya Uchaguzi Mkuu. Pesa hizo zinatoka wapi? Najua serikali haijaipa ODM pesa. Hivyo basi, hizi pesa zote zinatoka wapi?” alihoji.
Aliongeza kwamba wale wanaosukuma maamuzi ya mapema wanaweza kuona faida, iwe ya kibinafsi au ya pamoja, lakini haraka kama hiyo inaweza kuacha ODM ikiwa imebeba lawama za kushindwa kwa utawala wa sasa.
Bi Odinga alisema viongozi wa ODM hawawezi kufanya maamuzi ya kulazimisha kabla ya kusikiliza wananchi, akisisitiza ODM ni chama cha kitaifa kuanzia Turkana hadi Kwale, Wajir na hata Isebania.
“Wakati mnapojadiliana, nguvu yenu ya kipekee kama chama iko wapi? Mnaweza kujadiliana kuhusu nafasi za Waziri, lakini kama hamna magavana au wabunge, mtafanya kazi vipi? Ndio sababu lazima tuchukue tahadhari. Na jambo muhimu zaidi, hatupaswi kuacha wananchi nyuma,” alisema.