Korti ilivyotibua mipango ya Ruto kwa mpigo
MAHAKAMA Kuu jana ilitibua mipango ya Rais William Ruto katika maamuzi ya kesi mbili yaliyofuta ofisi ya washauri wake na kufufua chama cha Amani National Congress ambacho kilimezwa na chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA).
Katika uamuzi wa kwanza, mahakama ilibatilisha kuundwa kwa ofisi za washauri wa Rais na kufuta uteuzi wa watu 21 waliokuwa wakihudumu katika nyadhifa hizo.
Mahakama pia ilizuia Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) na Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) kutambua ofisi hizo au kulipa mishahara na marupurupu yoyote yanayohusiana nazo.
Uamuzi huo ulitokana na kesi mbili zilizowasilishwa na shirika la Katiba Institute pamoja na mwanaharakati wa haki za binadamu wakili Suyianka Lempaa, waliopinga kile walichokitaja kama kurejea kwa “baraza la siri” ndani ya serikali kuu, linalofanya kazi nje ya Katiba na mifumo rasmi ya utumishi wa umma.
Jaji Mwamuye alisema ingawa Rais huenda alichukua hatua hizo kwa nia njema, mchakato uliotumika kuunda ofisi za ushauri ni “ukiukaji mkubwa” wa Katiba na sheria.
“Hatua, maamuzi na mapungufu katika mchakato huo yanaonyesha kukiukwa kwa kikatiba kwa kiwango cha hatari na kisichorekebishika,” aliamua jaji huyo.
Ofisi zilizobatilishwa ni pamoja na Baraza la Washauri wa Masuala ya Uchumi wa Rais, Ofisi ya Mshauri wa Usalama wa Chakula na Uzalishaji wa Mifugo, Huduma za Utekelezaji wa Serikali, Ofisi ya Mshauri wa Usalama wa Taifa, Ofisi ya Mshauri wa Haki za Wanawake na Ofisi ya Baraza la Ushauri wa Mabadiliko ya Tabianchi.
Nyingine ni Ofisi ya Masuala ya Fedha na Sera ya Bajeti, Ofisi ya Mabadiliko ya Kiuchumi, Mshauri wa Masuala ya Mifugo na Malisho, Mshauri Mkuu wa Masuala ya Kikatiba, Mshauri Mkuu wa Kisiasa, Mshauri Maalum wa Uwezeshaji wa Kiuchumi kwa Vijana na Ofisi ya Mshauri Mkuu wa Uchumi.
Miongoni mwa waliokuwa wakinufaika na ofisi hizo tata ni Bw David Ndii, Profesa Makau Mutua, Bw Jaoko Oburu ambaye ni mpwa wa marehemu kiongozi wa ODM Raila Odinga, aliyekuwa Wakili Mkuu Kennedy Ogeto na wakili Harriet Chiggai, miongoni mwa wengine.
Mahakama iliamua kuwa Rais Ruto alipuuza jukumu la lazima la kutoa mapendekezo kwa Tume ya Utumishi wa Umma chini ya Ibara ya 132(4)(a) ya Katiba na hakuzingatia masharti ya kisheria yaliyoainishwa katika Sheria ya Tume ya Utumishi wa Umma na kanuni zake.
Pia, ililaumu mchakato huo kwa kutekelezwa bila ushauri wa Tume ya Mishahara na Marupurupu kuhusu athari za kifedha.
Aidha, mahakama ilisema kuwa ofisi hizo ziliundwa kwa siri bila ushirikishwaji wa umma, kinyume na Ibara ya 10 na 201 za Katiba.
Jaji alisema hilo lilikiuka misingi ya utumishi wa umma ikiwemo uwazi, uadilifu, ushindani wa haki na matumizi bora ya fedha za umma.
Kutokana na hayo, mahakama ilitangaza ofisi hizo na uteuzi uliotokana nazo kuwa batili tangu mwanzo.
Ilitoa maagizo ya kubatilisha maamuzi yote ya kuunda ofisi hizo na kuwateua washauri hao, na kuizuia kabisa serikali kuwezesha au kuwalipa fedha zozote.
Jaji pia alitoa agizo akiitaka PSC, ndani ya siku 90, kufanya ukaguzi wa kina wa ofisi zote zilizoanzishwa katika Ofisi ya Rais tangu kutangazwa kwa Katiba ya 2010, hususan zile zilizoanzishwa chini ya Rais Ruto baada ya Agosti 2022.
Ofisi yoyote itakayobainika kuanzishwa kinyume cha Katiba itavunjwa, huku ripoti ya maendeleo ikitakiwa kuwasilishwa mahakamani ndani ya siku 120.
Katika uamuzi wa pili, Mahakama Kuu ilibatilisha kuvunjwa kwa chama cha kisiasa cha ANC, kinachohusishwa na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, na kukirejesha rasmi katika ulingo wa siasa.
Katika hatua ambayo ni pigo la kisheria kwa muungano wake na chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Rais Ruto, mahakama ilifuta Notisi ya Gazeti la Serikali iliyotolewa mwaka jana na kumuagiza Msajili wa Vyama vya Kisiasa kurejesha mara moja hadhi kamili ya kisheria ya ANC.
ANC ilivunjwa Januari 2025 na kuunganishwa na UDA cha Rais William Ruto, ikafutwa rasmi Machi 7, 2025 baada ya Mkutano Maalumu wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC) kukubali uamuzi huo.
Kufuatia muungano huo, Gavana wa Lamu Issa Timamy, aliyekuwa kiongozi wa ANC, aliteuliwa kuwa naibu kiongozi wa UDA, huku Mbunge wa Emuhaya Omboko Milemba, aliyekuwa katibu mkuu wa ANC, akichukua wadhifa wa naibu katibu mkuu wa UDA.
Hatua hiyo ilipigwa vita mahakamani na mwanaharakati wa haki za raia Stephen Mutoro, aliyemshtaki Bw Mudavadi, Msajili wa Vyama vya Kisiasa na maafisa wengine wa chama.
Kesi hiyo ilihusu haki za kisiasa za wanachama na mustakabali wa chama kilichoanzishwa kutetea siasa za mageuzi.
Katika uamuzi wake, mahakama ilitangaza kuwa, Mkutano Maalum wa NDC uliofanyika Februari 7, 2025 ulikuwa kinyume cha sheria, ikisema uliendeshwa “kwa kukiuka Katiba” kwa kukosa kuwahusisha wanachama.
Maamuzi yote yaliyofikiwa katika mkutano huo, yakiwemo kuvunjwa kwa chama na kuhamisha mali yake, yalitangazwa kuwa kinyume cha Katiba, haramu, batili na yasiyo na nguvu ya kisheria tangu mwanzo.
“ANC bado ni chama cha kisiasa kilichosajiliwa kihalali ambacho uhai wake wa kisheria haujawahi kukomeshwa kwa njia halali,” alisema Jaji Bahati Mwamuye.
Jaji huyo alitoa amri inayomlazimisha Msajili wa Vyama vya kisiasa, kufuta rekodi zote za kuvunjwa kwa chama na kutoa taarifa kwa taasisi za serikali na umma.
Aidha, alitoa amri ya kudumu ya kuzuia wahusika kuingilia mali ya ANC kama ilivyokuwa Februari 6, 2025 bila kufuata sheria, na akaagiza mali yoyote iliyohamishiwa UDA au taasisi nyingine irejeshwe mara moja.