Habari

Ripoti: Wafanyakazi 27,284 waliajiriwa kinyume cha sheria katika kaunti 41

Na PETER MBURU January 25th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

TAKRIBAN wafanyakazi 27,284 waliajiriwa kinyume cha sheria katika kaunti 41 ndani ya kipindi cha miaka mitatu hadi Juni 2024, taarifa mpya zinaonyesha.

Isitoshe, magavana walikiuka sheria katika uajiri huo, hali iliyozifanya kaunti zikabiliwe na hatari ya kuwa na wafanyakazi wengi kupita kiasi.

Kaunti hizo ziliajiri maelfu ya wafanyakazi kati ya mwaka wa kifedha wa 2021/22 na 2023/24 licha ya kukosa mipango ya ajira au bajeti, kulingana na ukaguzi maalumu wa usimamizi wa mishahara.

Ripoti za ukaguzi zinaonyesha kuwa, katika kipindi hicho cha miaka mitatu, ni kaunti sita pekee ambazo hazikuajiri wafanyakazi wapya.

Kaunti ya Uasin Gishu iliongoza kwa kuajiri wafanyakazi wapya 3,982 (bila kujumuisha vibarua), ikifuatwa na Kitui (1,715), Trans Nzoia (1,082) na Turkana (1,054).

“Serikali ya kaunti iliajiri wafanyakazi 3,982 katika kipindi cha miaka mitatu ya kifedha. Hata hivyo, ilibainika kuwa idara zilizofanya uajiri hazikuwa na mipango ya kila mwaka ya ajira ya kuongoza zoezi hilo,” asema Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu katika ukaguzi maalum wa mishahara ya Kaunti ya Uasin Gishu.

“Kukosekana kwa mipango ya ajira kunaweza kusababisha kuajiri wafanyakazi kupita kiasi au wachache, au kuwaajiri kwa nyadhifa zisizolingana na vipaumbele vya taasisi.”

Kati ya wafanyakazi wote walioajiriwa katika kaunti 41, asilimia 14.6 walikuwa Uasin Gishu, hali inayodhihirisha ukubwa wa uajiri haramu katika kaunti hiyo ambako mzigo wa mishahara ulifikia wastani wa asilimia 41.7 kwa kipindi cha miaka mitatu, ikizidi kiwango cha kisheria cha asilimia 35.

Mkaguzi wa Hesabu anakosoa kaunti kwa kuendesha ajira bila mifumo ya kubaini mahitaji halisi ya wafanyakazi au kuhakikisha upatikanaji wa fedha za kuwalipa.

Hali hiyo inaweka kaunti katika hatari ya kuwa na wafanyakazi wengi katika idara fulani huku zingine zikiwa na upungufu, jambo linaloathiri utoaji wa huduma.

Kaunti nyingine zilizoajiri wafanyakazi wengi ni Bomet (1,046), Nyamira (1,031), Nakuru (985), Nairobi (965), Narok (923) na Laikipia (913), zikikamilisha orodha ya kaunti 10 zilizoajiri wafanyakazi wengi zaidi.

“Mchakato wa ajira ulionyesha udhaifu mwingi, ikiwemo kuajiri bila kutangaza nafasi, kuajiri watu ambao hawakuomba nafasi zilizotangazwa, na kuthibitisha upatikanaji wa bajeti baada ya matangazo ya ajira,” alisema Bi Gathungu kuhusu Kaunti ya Narok.

Alionya kuwa mienendo hiyo inadhoofisha uwazi, haki na taratibu za ajira, na inaweza kuruhusu kuajiri watu wasio na sifa, hali inayobebesha kaunti mzigo wa kifedha.

Kaunti 10 zilizoajiri wafanyakazi wengi zaidi ziliajiri jumla ya wafanyakazi 13,696—zaidi ya nusu ya ajira zote mpya katika kaunti 41.

Katika Kaunti ya Embu, Mkaguzi wa Hesabu alibaini kuwa gavana alianzisha ofisi za kasisi wa kaunti na mshauri wa afya wa gavana kinyume cha sheria.

Jumla ya wafanyakazi 775 waliajiriwa katika kipindi hicho.

“Nyadhifa kadhaa zilijazwa kati ya 2022, 2023 na 2024 bila kuzingatia mapendekezo ya Kamati ya Ushauri ya Usimamizi wa Wafanyakazi ya Kaunti,” alisema.

Aidha, Kaunti ya Lamu iliajiri wafanyakazi 100 bila tathmini ya mahitaji ya ajira, huku 16 wakiajiriwa kabla ya matangazo kutolewa.

Katika Kaunti ya Samburu, ambako wafanyakazi 746 waliajiriwa, ukaguzi ulibaini kuwa wafanyakazi 26 waliajiriwa kupita idadi iliyotangazwa , huku wengine 192 wakiteuliwa moja kwa moja na kulipwa Sh47.7 milioni katika kipindi cha miaka mitatu.