Habari

Murkomen: Nimeshangazwa sana na tukio la uvamizi kanisani Witima

Na FATUMA BARIKI January 25th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

WAZIRI wa Usalama Kipchumba Murkomen amesema ameshangazwa na tukio la kuvamiwa kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kanisani Witima ACK, Othaya ambapo watu waliobeba silaha na wengine wakiwa kwenye magari ya polisi walifyatua bunduki na vitoza machozi kwa waumini.

Bw Murkomen amesema ghasia hazifai kokote nchini haswa eneo la kuabudu, akitaja kitendo hicho kuwa kisichokubalika.

SOMA Chapisho la Waziri Murkomen akikemea ghasia kanisani Watima, Othaya

“Nimeongea na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja ambaye amenihakikishia kwamba uchunguzi umeanzishwa na waliohusika watachukuliwa hatua haraka iwezekanavyo,” akasema kwenye chapisho katika safu zake za mitandao.

Aliwataka polisi kuchukua hatua upesi bila woga wala upendeleo kukabiliana vilivyo na waliopanga na kudhamini uvamizi huo bila kujali cheo wala hadhi yao katika jamii.

“Kama serikali, tunashikilia kwa uzito na kudumisha vipengele vya demokrasia ikiwemo haki ya kukusanyika na kuabudu. Naomba umma uwe na utulivu wakati ambapo vikosi vya usalama vinakabiliana na jambo hili,” akahitimisha.