Serikali yakanusha wanafunzi wa Gredi 10 wanalala tu shuleni bila kusoma
SERIKALI imepuuzilia mbali madai kwamba hakuna masomo yanayoendelea katika Gredi ya 10 katika shule za upili baada ya kucheleweshwa kwa vitabu na changamoto nyingine zinazoshuhudiwa.
Waziri wa Elimu Bw Julius Ogamba alisema licha ya kucheleweshwa kwa vitabu, shughuli za masomo zinaendelea madarasani kote nchini huku wizara ikijizatiti kuhakikisha wanafunzi wote wanapokea vitabu hivyo.
Bw Ogamba alitoa ufafanuzi kuhusu kwa nini vitabu hivyo vilichelewa wiki moja sasa baada ya wanafunzi hao kujiunga na shule za upili.
Kuwa mujibu wa wazazi na baadhi ya walimu waliohojiwa na Taifa Leo, kucheleweshwa kwa vitabu hivyo ulisababisha kusitishwa kwa masomo kwa wanafunzi wa Gredi ya 10.
Hata hivyo, Bw Ogamba alihakikishia Wakenya kuwa masomo yanaendelea.
Bw Ogamba alisisitiza kuwa shule nyingi zimeanza masomo hasa kuwaelekeza wanafunzi kuhusu masomo katika shule za upili ili kuwasaidia katika kuchagua taaluma wanazotaka.
“Kwa sasa walimu wanawafafanulia kuhusu masomo waliyochagua na watakayosoma katika shule za upili. Huu ndio mchakato unaoendelea wakati huu. Kumbukeni hii ni mara ya kwanza kabisa kupokea wanafunzi wa Gredi ya 10. Kwa hivyo, haya ni masuala ambayo yanaweza kutokea,” alisema Waziri.
Hata hivyo, alisema mpito ujao utakuwa laini kwani vitabu vitakuwa viko tayari.
Mahojiano
Akiongea kwenye mahojiano na runinga ya KTN, Bw Ogamba alisema kwamba wizara yake bado itazingatia sera ya kitabu kimoja kwa kila mwanafunzi katika kila somo ili kufanikisha elimu bila malipo.
“Serikali ilikuwa ikidaiwa Sh11 bilioni na wachapishaji kutokana na madeni ya awali kuanzia Gredi ya 1 hadi Gredi ya 9. Wachapishaji walisimama kidete kwamba hawatatoa vitabu vya Gredi ya 10 hadi pale tutakapowalipa madeni yao. Wiki tatu zilizopita tuliwalipa Sh5.6 bilioni na tukakubaliana kwamba watasambaza vitabu hivyo shuleni,” akasema Bw Ogamba.
Serikali imekuwa ikitumia NEMIS kusambaza vitabu katika shule za umma.
Bw Ogamba alisema baada ya kulipa nusu ya deni hilo, wachapishaji hao walianza shughli za usambazaji Januari 16 na usambazaji huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Waziri huyo alisema shule zote za upili za umma zitapokea vitabu vya Gredi 10 ifikiapo mwisho wa mwezi huu.
Alibainisha kuwa kufikia sasa, asilimia 40 ya vitabu vimeshasambazwa, huku lengo likiwa ni kukamilisha zoezi hilo kufikia mwisho wa mwezi huu.
Alisema vitabu hivyo vya Gredi ya 10 vina muda wa kudumu wa miaka minne.
Serikali imekuwa ikisambaza vitabu kwa wanafunzi walioko shule za umma kote nchini kwa zaidi ya mwongo mmoja kupitia mpango wa elimu bila malipo huku ikitumia takwimu kutoka NEMIS kutathmini idadi ya wanafunzi.
Kila mwanafunzi amekuwa akipokea kitabu cha kila somo. Waziri Ogamba, alifichua kuwa malimbikizi ya madeni hayo ndiyo yalisababisha hali hiyo, ambayo imeanza kutatuliwa na asilimia 40 ya vitabu tayari imesambazwa kwa shule za umma.