Ukimtegemea sana Uhuru utauma kavu, wabunge waambia Matiang’i
BAADHI ya wabunge wanaomuunga mkono Rais William Ruto wamemtaka aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i kukoma kumtegemea Rais mstaafu Uhuru Kenyatta katika azma yake ya kuwania urais.
Wabunge hao waliozungumza Jumapili katika Kaunti ya Kisii, walimweleza Dkt Matiang’i kwamba rais huyo wa zamani atamwangusha jinsi alivyomfanya aliyekuwa kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) marehemu Raila Odinga.
Wakihutubia waumini wakati wa ibada ya kanisa katika kijiji cha Nyansakia, Kegogi katika Eneobunge la Kitutu Chache Kaskazini, kikosi cha United Democratic Alliance (UDA) kilimwambia Dkt Matiang’i ajitayarishe kulamba sakafu iwapo ataweka matumaini yake yote kwa Bw Kenyatta.
Wakiongozwa na Waziri wa Elimu Julius Ogamba na msaidizi wa kibinafsi wa rais Farouk Kibet, wabunge hao walidai Dkt Matiang’i si mtu wa kumtisha Dkt Ruto katika urais, na kuongeza kuwa hajafanya vya kutosha kuwashawishi Wakenya kote nchini wamuunge mkono.
“Nataka kumwambia mwanenu akome kumtegemea rais wa zamani ili amfanye rais. Ikiwa Uhuru Kenyatta hakumwezesha Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha 2022, unafikiri atamfanya Dkt Matiang’i kuwa rais?” Mbunge wa Taveta John Bwire alijinadi.
Bw Bwire alionyesha matumaini kuwa Rais Ruto atashinda muhula wa pili katika uchaguzi wa 2027 akidai kuwa kiongozi huyo wa nchi amefaulu kuwaunganisha wananchi wa Kenya na kuanzisha miradi mingi ya maendeleo.
Mbunge huyo wa awamu ya kwanza aliongeza kuwa eneo la pwani anakotoka, pia lilikuwa na mpango wa kusimamisha mgombeaji urais katika kinyang’anyiro cha Ikulu 2027 lakini wakabadili niabaada ya kujua jukumu lililo mbele yao si jepesi na hivyo basi kuamua kumuunga mkono Dkt Ruto.
“Tuliketi na watu kama Hassan Joho. Pia tulitaka kumpigia debe mtu wetu kumpinga Dkt Ruto lakini tukagundua haikuwa rahisi hivyo. Baada ya kufikia uamuzi huo, tulisema tuungane kumuunga mkono rais hadi 2032,” Bw Bwire alisema.
Aliendelea, “wacha niwaambie, mtu anayempotosha mwanao ni yule aliyemdanganya Raila Odinga,”
Mbunge wa Likuyani Innocent Mugabe alimtaka Dkt Matiang’i kufikiria kufanya kazi na Dkt Ruto kisha kuzingatiwa kwa malengo yake ya kisiasa 2032. Aliomba jamii ya Abagusii ipate funzo kutokana na uchaguzi wa 2002 wakati pia walikuwa na mgombeaji urais kwa aliyekuwa Waziri wa Barabara marehemu Simeon Nyachae, ambaye alishindwa na marehemu Mwai Kibaki.
Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse alisema Dkt Matiangi hawezi kunyakua urais kwa kura ya Gusii pekee.
“Nyinyi nyote husikiliza redio na kutazama runinga na mnaweza kuona wazi kila mtu anakoelekea. Kila mmoja anamuunga mkono Rais Ruto. Sasa nataka kuwauliza nyinyi watu wangu wa Gusii, hata mkimpigia kura zote kwa mtu wenu, mnadhani anaweza kushinda mkiwa nyinyi pekee yenu,” Bw Mutuse aliuliza.
Kwa upande wake, msaidizi wa rais aliendeleza mashambulizi yake makali ya kawaida dhidi ya kiongozi wa Democratic for the Citizens Party (DCP) Rigathi Gachagua.
Bw Kibet alimtaja Bw Gachagua kuwa mkabila ambaye hajifunzi kamwe kutokana na makosa yake, akitaja kuondolewa kwake afisini kama Naibu Rais kuwa jambo bora zaidi kuwahi kutokea nchini.
Waziri wa Elimu Ogamba pia aliunga mkono Utawala wa Kenya Kwanza na kuhamasisha jamii yake kuuunga mkono uongozi wa Dkt Ruto.
Wabunge wengine wa Kisii Silvanus Osoro (Mugirango Kusini), Japheth Nyakundi (Kitutu Chache Kaskazini na mwenyeji), Jerusha Momanyi (Nyamira) na Dorice Aburi (Kisii), wote walitangaza utiifu wao kwa rais.