Mbadi azima mradi wa Benki ya Dunia Nyamira
GAVANA wa Nyamira Amos Nyaribo anaendelea kuandamwa na changamoto mpya baada ya Wizara ya Fedha kuzima utawala wake dhidi ya kutekeleza mradi wa tabianchi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Wizara ya Fedha imechukua hatua hiyo kutokana na madai ya ufujaji wa fedha.
Katika barua iliyoandikwa mnamo Desemba 15, 2025 Wizara ya Fedha imezima kaunti kutekeleza mpango huo almaarufu kama FLLoCA kwa sababu ya ubadhirifu wa Sh22 milioni.
Kusitishwa kwa mpango huo ni pigo kwa Gavana Nyaribo na kunatokea wiki chache baada ya kunusurika kutimuliwa na Bunge la Seneti.
Pia anaandamwa na madai ya kushiriki ufisadi huku akichunguzwa na Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi Nchini (EACC).
Waziri wa Fedha John Mbadi alisema kuwa wachunguzi kutoka Benki ya Dunia waligundua ubadhirifu mkubwa wa pesa katika Kaunti ya Nyamira.
Barua hiyo ilinakiliwa pia kwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la Magavana Nchini (COG) Mary Mwiti.
Uchunguzi
“Benki ya Dunia iliwatuma mawakala wake na wakafanya uchunguzi ambao ulifichua ubadhirifu mkubwa wa fedha. Suala hili limeibua mtihani wa uwazi katika matumizi ya fedha kwenye miradi mbalimbali,” ikasema barua hiyo.
Barua hiyo ilikuwa inasema kuwa pesa zilikuwa zikitumika kiholela na rasilimali nyingine zimekuwa zikitumika kwa njia isiyokusudiwa.
“Kutokana na hili, kaunti hii imezuiwa dhidi ya kuendelea na mradi wa FLLoCA hadi masuala yaliyoibuliwa yalainishwe na Benki ya Dunia itume barua kwa Hazina Kuu ya Fedha,” ikasema barua hiyo.
Bw Nyaribo hata hivyo alipuuza madai kuwa pesa za ufadhili wa mradi huo zimeliwa badala ya kutumika katika miradi ya maendeleo.
“Watu wengine wanasema pesa zimepotea, acheni siasa hakuna pesa zilizopotea. Hata sumuni haijapotea,” akasema Bw Nyaribo akihutubu kwenye eneobunge la Borabu.
Aliahidi kuwa utawala wake utatoa ufafanuzi, akisema ukweli utajulikana.
Bw Nyaribo aliapa kuwa utawala wake utaendelea kutekeleza miradi yake akisema kuwa anamakinikia kuyabadilisha maisha ya wakazi wa Nyamira.
“Katika miezi michache inayokuja tutasambaza maji kutoka kwa visima Wadi ya Esise. Kituo cha afya cha Isoge kitamalizika mnamo Desemba mwaka huu na pia tutafungua barabara nyingi maishani,” akasema.