Siasa

Wanasiasa wa Taita-Taveta waonekana kumkimbilia Rais Ruto kuelekea 2027

Na ANTHONY KITIMO January 26th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI wa kisiasa wanaohudumu Kaunti ya Taita-Taveta, wamesalia kwenye njiapanda baada ya vyama vilivyowafadhili kuingia mamlakani na kupoteza umaarufu eneo hilo huku vikionekana kuegemea kwa uongozi wa Rais William Ruto.

Wanasiasa wengi waliochaguliwa kwa tiketi za chama cha ODM na Wiper, sasa wanaonekana kukimbilia kuidhinishwa na Rais Ruto ili kubakia kwenye viti vyao huku wakazi wakilalamika na kuwalaumu kwa kutotimiza ahadi zao walizotoa wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

Hili lilidhihirishwa na mashindano yaliyojitokeza wiki mbili zilizopita mtandaoni kila mmoja akitaka kuhusishwa na Rais Ruto alipokuwa anajipanga kuzuru kaunti hiyo licha ya tofauti vya vyama.

Viongozi kutoka vyama tofauti na UDA haswa ODM ambao wameonekana kuendelea kupiga siasa bila mwelekeo rasmi katika uchaguzi ujao baada ya kuaga dunia kwa kinara wa chama hicho Raila Odinga, wameonekana wakijipigia debe kuonekana kumuunga mkono Rais Ruto ili kupata baraka za kujitosa uwanjani mwaka ujao.

Ikizingatiwa kuwa katika uchaguzi mkuu wa 2022, Rais Ruto alipata mbunge mmoja wa chama chake cha UDA, (mwakilishi wa wanawake Bi Lydia Haika) wakati huu dalili zaonyesha kuwa ana kazi rahisi kupata uungwaji mkono kwani viongozi hao wameanza mbio za kujitambulisha kwake.

Viongozi wa zamani wakiwemo magavana wanaonuia kurudi katika siasa za 2027 pamoja na wanasiasa wanaohudumu wameweka mabango na kupiga kampeni mtandaoni wakimkaribisha kiongozi huyo wa nchi ambaye alitarajiwa kuweka jiwe la msingi wa soko la kisasa eneo la Voi siku ya Ijumaa ambayo hakuhudhuria.

Gavana wa kwanza na wa pili wa kaunti hiyo Bw John Mruttu na mwenzake Granton Samboja mtawalia wameonekana wakijihusisha na uongozi wa Bw Ruto huku mwakilishi wa wanawake Bi Haika ambaye alikuwa kiongozi wa UDA katika uchaguzi uliopita eneo hilo naye akionekana kujidai ndiye anayetakiwa kumwalika kiongozi huyo.

Viongozi wengine ambao wamejitokeza kualika kiongozi huyo licha ya miaka ya nyuma kuwa katika vyama vilivyompinga Bw Ruto ni pamoja na Mbunge wa Voi Abdi Chome, mwenzake wa Taveta John Bwire na wa Mwatate Peter Shake.

“Tunasikitika kuona viongozi wakitaka kuidhinishwa na Rais Ruto kwa kipindi kingine badala ya kututimizia ahadi walizotoa mwaka wa 2022,” alisema Bi Phedes Saru, mkazi wa Voi.

Mwishoni mwa mwaka jana katika ziara yake Kaunti ya Taita-Taveta, Rais Ruto alijitenga na kuhusishwa na viongozi ambao wanategemea kuidhinishwa bila kufanyia wakazi kazi na wasio na sera.

Aliyekua mwakilishi wa kike wa Taita-Taveta Joyce Lay naye amesisitiza umuhimu wa viongozi kufanya hamasa kwa wapiga kura wafahamu majukumu ya viongozi kabla ya uchaguzi wa mwaka wa 2027.

Wakazi wa Taita-Taveta wakiongozwa na viongozi wa makanisa na wanaharakati wa haki za kibinadamu wamekuwa kipaumbele kuhamasisha wakazi na kuchambua utendakazi wa wanasiasa jambo ambalo limewatia tumbo joto viongozi wa kisaisa.

Wanasiasa wamekuwa wakikashifiwa kwa unyakuzi wa ardhi ambao umeshughudiwa miaka mitatu iliyopita bila wao kutetea wakazi na badala yake kuegemea upande wa wanyakuzi.

Hata hivyo, licha ya kuelekea kuidhinishwa na Rais Ruto, wakazi wanaendelea kushawishi viongozi ambao wanataka kufanya kazi naye kuomba serikali kutekeleza miradi mbalimbali iliyoahidi wakazi wa Taita-Taveta wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.

Rais Ruto aliahidi miradi ya usambazaji wa maji, ujenzi wa barabara, ufufuaji wa reli ya zamani kutoka Voi hadi Taveta, ukamilishaji wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Voi, miongoni mwa ahadi zingine.

Miongoni mwa miradi iliyoanzishwa na kukwama ni mradi wa bomba la pili la Mzima, ujenzi wa barabara ya Bura-Mghange-Mbale-Mtomwagodi pamoja na ile ya Taveta-Illasit.

Wakati wa ziara yake mwaka jana, Rais aliahidi kuwa mradi wa maji ya Mzima ungeanzishwa kufikia Desemba mwaka wa 2024 lakini mpaka sasa haujang’oa nanga.

Vilevile, Rais aliahidi kuwa serikali yake itahakikisha kuwa kaunti hiyo inapata asilimia 50 ya mapato ya hifadhi ya mbuga ya Tsavo.