MAONI: Demokrasia haifi kamwe, madikteta ndio hufariki
KWA Waganda wanaotishiwa na serikali yao kwamba itaangamiza upinzani kabisa, labda nchi yao isalie na chama kimoja pekee kinachoitawala, nawapa moyo kwa kuwakumbusha kuwa hata marehemu Rais John Magufuli wa Tanzania alinuia kumaliza upinzani nchini mwake ila akafa kabla.
Nia ya kuangamiza upinzani ni tishio la moja kwa moja dhidi ya demokrasia, yaani kuwapokonya wananchi uhuru na manufaa mengineyo yote ambayo wamepigania kwa miaka mingi.
Ni sawa na kuwaambia wananchi kwamba hawana thamani, maoni yao kuhusu wanavyotaka kutawaliwa si muhimu, aliye na usemi pekee ni mtawala aliye madarakani, na ana wasaidizi vibaraka ambao wako radhi kumfia bila aibu.
Utashi wa watu kujitawala daima hauishi, wanaokufa ni madikteta, na aghalabu vifo vyao husherehekewa kwa kuwa vinaashiria mwanzo mpya ambao, ingawa mfupi au mbaya, ni fursa ya waathiriwa kuutua mzigo mzito, ndiposa wao husherehekea mwanguko wa adui.
Demokrasia haifi, madikteta ndio hufa.
Magufuli yumo kaburini, Daniel Moi yumo futi sita chini ya ardhi. Mobutu Seseseko hakumbukwi tena na Wakongomani, kasri yake imejiotea magugu ovyo.
Iddi Amin Dada alifia chumba cha kupanga kama mtu wa kawaida tu, Uganda haikumpa hata kaburi la kuzikwa.
Mshindi ni demokrasia kwani haifi, na demokrasia inaposhinda watu huwa wameshinda.
Hiyo ni ithibati kwamba nchi ni ya wananchi pia, mtawala akiringa nayo au kuikalia mguu wa kausha ajue hana tofauti na mkoloni aliyetamba kishenzi ila mwishowe akatuwachia nchi yetu shingo upande.
Nusra macho yanitoke nje nilipoona polisi wakimshika mwanahabari na kugongesha kichwa chake kwenye gari wakati wa ghasia za uchaguzi wa Uganda, lakini ghafla nikakumbuka huko ni Uganda, nchi ambayo dola hutumia nguvu kuwanyamazisha wananchi.
Unapoona hali ambapo vyombo vya kulinda usalama vinajitwika mzigo wa kumdumisha kiongozi madarakani, basi jua hiyo si nchi bali pori kubwa ambako watu hulana kama wanyama bila maadili yoyote.
Ni mfumo uliooza, badala ya kuwafundisha polisi kutekeleza sheria kwa njia ya kisasa wanawafundisha kututumua misuli na kutumia nguvu dhidi ya raia ili waogopwe.
Kisa hicho cha mwanahabari kudhulumiwa kilinikumbusha kingine ambapo marubani wa jeshi la Uganda waliokuja Kenya kwa shughuli rasmi walipotelea angani, mwishowe wakaangusha ndege na kufa nazo miaka michache iliyopita.
Uchunguzi ulionyesha kuwa lilikuwa na tatizo dogo tu la mawasiliano, yaani marubani wa jeshi la Uganda walishindwa kuelewana na waelekezi wa ndege wa Kenya kwa kuwa Waganda hao walizungumza Kiganda pekee huku Wakenya wakiwazungumzia Kiingereza.
Labda utashangaa ilikuwaje kwa sababu tangu hapo tunaamini kwamba Waganda huzungumza Kiingereza kwa ukubwa kwa kuwa ndiyo lugha yao ya taifa.
Nakuelewa, lakini nakufahamisha kuwa katika nchi ambapo ujinga husifiwa kuliko werevu, ni rahisi kupata wajinga wengi wa kuingiza kwenye mfumo mbaya unaowadhalilisha watu.
Katika mfumo mchafu, werevu na ujasiri wa kuhakiki mambo huchukuliwa kama kilema.
Tatizo la kuongozwa na dikteta ni kwamba maovu yake huua wapinzani na wanaomuunga mkono vilevile.
Waganda, na Waafrika kwa jumla, wanapaswa kuwa makini sana wanapohusiana na dikteta Yoweri Museveni au mwingine yeyote.
Anaua watu katika jaribio lake la kuua demokrasia, sikwambii na unoko wake huo hula kwake pia.
Kila ofisa wa usalama, au mtu wa mkono tu anayetumiwa kuwakandamiza wananchi, anapaswa kujua kwamba dikteta haishi milele. Mpambanaji naye aipambanie nchi yake, si yao pekee.
-Douglas Mutua ni mwanahabari Mkenya anayeishi Amerika ([email protected])