KINAYA: Tutaishi kushiriki vitimbi na sarakasi au tutajenga nchi?
NIMEKWAMBIA kwa muda sasa kwamba Kenya ni jukwaa kubwa la sarakasi na vituko, likiisha hili linaingia lile, na yote yanatishia kukutegua mbavu.
Mara RAO alituacha serikalini hatutoki; mara tochi ya Jirongo imezima na hivyo ikazima washukiwa; mara huyu kagunduliwa havai za ndani, hivyo kampuni ya chupi itamlipa ili aanze kuzivaa na kuzinadi.
Hapo ndipo unapouliza: tutajuaje amevaa? Atalipwa kwa saa, siku au mwezi?
Na usisahau kuna kichaa cha mbwa… samahani… cha kukumbatia miti, yaani tabia ya kuudhi sana ambapo watu wanaoiga wazo asili la mtu na kulitoa thamani.
Basi na ajitokeze jasiri amtomase simba pale Masai Mara, akiponea tumvike taji ya kivutio bora cha watalii.
Kwenye siasa, hebu angalia jinsi mwakilishi wa vijana katika ODM, mzee mzima wa karibu miaka tisini, anavyopigana miereka na mpwa wake kijana.
Tafakari Oburu Oginga, aliyewahi kuteuliwa mwakilishi wa vijana katika Bunge la Seneti, akipigana na Winnie Odinga, ambaye hajawahi kuwawakilisha vijana popote.
Hivi vita havina usawa kabisa, Winnie anaonewa. Haki itatendeka pale Winnie atakapoteuliwa mwakilishi wa wazee kwenye Bunge hilo-hilo, kisha yeye na mjomba wake huyo wajitose kwenye ulingo na kuendelea na miereka.
Vinginevyo, Babu Oburu anapaswa kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha kuongoza ODM kwa sababu tayari amewawakilisha vijana akiwa mzee, na kwa namna fulani aliwawakilisha wazee pia kwa sababu yeye ni mzee.
ata hivyo, kwa sababu Waafrika tunawaheshimu wazee, tutaisihi serikali imlipe Oburu mshahara wa miaka mitano ambapo aliwakilisha wazee bila malipo.
Atakuwa na bahati kubwa ya kula mara mbili kwa kuwa tayari alikwisha kulipwa huo wa kuwawakilisha vijana.
Ama tuseme aende nyumbani mikono mitupu tu kwa sababu alipokuwa anawawakilisha vijana, Babu Owino naye, ambaye ni mshirika wa Winnie, japo kijana, aliwakilisha wazee kwa jina lake tu – Babu.
Aliyemdanganya Oburu kwamba anaweza kushinda miereka yoyote dhidi ya vijana machachari – Winnie, Babu na Edwin Sifuna – alimkosea sana. ODM, kama tulivyoimba pambio tukiwa watoto, itajengwa na vijana.
Inatabirika kwamba vijana hao watatu, na wengine wengi wanaowaunga mkono, watakuwa kwenye siasa za Kenya kwa muda mrefu. Sijui utabiri wa wazee ving’ang’anizi unasemaje.
Eti tochi ya Jirongo kamla nani? Nimeona maprofesa wakisema tusiidharau, eti tusiseme utamaduni ulikuwapo hata kabla ya tochi kuundwa.
Lofa wa kawaida angesema hayo ningenyamaza, lakini sharti profesa anieleze tochi ilianza kutumika lini.
Na akisema zamani walitumia kaa la moto, basi nitasisitiza turejee huko kwa makaa ili tupate matokeo ya haraka. Kaa la moto huzima upesi ukilifutika kwa udongo. Hebu na tuharakishe mambo.
Usipoyacheka mambo haya yatakucheka na kukuhuzunisha, hivyo ni heri uyatangulie. Msongo wa mawazo nchini Kenya ni ugonjwa wa matajiri.
-Douglas Mutua ni mwanahabari Mkenya anayeishi Amerika ([email protected])