Habari za Kitaifa

Serikali ikichukulia suala la usalama kwa mzaha itajuta hivi karibuni – Matiang’i

Na RUTH MBULA January 27th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MWANIAJI wa Urais kupitia chama cha Jubilee Dkt Fred Matiang’i amesema kuwa Kenya huenda ikatumbukia kwenye machafuko kutokana na jinsi serikali inashughulikia masuala ya usalama.

Dkt Matiang’i alitaja kuvurugwa kwa hafla za makanisa ambazo zinahudhuriwa na viongozi wa upinzani, changamoto zinazokabili sekta ya elimu na ghasia za uchaguzi kama masuala ambayo yanatishia kusambaratisha nchi.

Alikashifu ghasia ambazo zilishuhudiwa Jumapili katika kanisa moja eneobunge la Othaya kwenye ibada iliyokuwa imehudhuriwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Ripoti zinaarifu kuwa kuvamiwa kwa Bw Gachagua ni tukio ambalo lilipangwa Nairobi na baadhi ya maafisa wa usalama na wanasiasa kisha likatekelezwa bila kuingiliwa kisiasa.

“Kilichotokea Othaya ni aibu kwa sababu vitoza machozi vilirushwa ndani ya kanisa ilhali serikali ipo,” akasema Dkt Matiangí.

Alishangaa kwa nini hakuna mtu ambaye amekamatwa kutokana na ghasia hizo akidai ushahidi u wazi.

“Hakuna chochote cha kufanyia uchunguzi kwa sababu picha ya waliotekeleza uvamizi huo wapo kila mahali. Mbona hawajakamatwa? Huwezi kutaka sheria iheshimiwe ilhali unavunja sheria hiyo hiyo,” akaongeza.

Dkt Matiang’i alimtaka Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki anayetoka Mlima Kenya, aingilie kati ili kuzima misururu ya ghasia za kisiasa ambazo zimekuwa zikishuhudiwa eneo hilo.

Pia alikashifu vyombo vya usalama akidai vinatumiwa vibaya kuendeleza ajenda za kisiasa.

“Inspekta Jenerali wa polisi ni mtu ambaye amehitimu lakini anashinikizwa na wanasiasa. Tukiendelea hivi basi tunaelekeza nchi kwenye njia ya machafuko ikizingatiwa pia hana maafisa wa kutosha wa usalama iwapo raia wataamua kuchukua sheria mikononi mwao,” akasema Dkt Matiang’i.

Waziri huyo wa zamani alishangaa taifa linaelekea wapi kiusalama baada ya mwanaume kuingia katika afisi ya Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen bila kutambuliwa na kusalia huko kwa zaidi ya saa tano.

“Inakuaje mwanaume anafika katika afisi hizo zenye ulinzi wa hali ya juu? Hii huenda ilipangwa na watu wa ndani na utetezi wa wizara yenyewe inachezea tu hekima ya Wakenya,” akasema akishiriki mahojiano na Kituo cha redio cha Kameme.

Katika mawanda ya kisiasa, Dkt Matiang’i alisema mabadiliko yaliyotekelezwa katika uongozi wa Jubilee, yanalenga kuimarisha umaarufu wa chama hicho.

Alisema mwandani wake Vincent Kemosi, mbunge wa zamani wa Mugirango Magharibi kupewa uenyekiti wa Jubilee, kunalenga kueneza umaarufu wa chama hicho sehemu zote za nchi.

Pia alikanusha kuwa aliyekuwa Katibu Mkuu Jeremiah Kioni alishushwa cheo baada ya kuteuliwa naibu kiongozi wa chama, akisema ukweli ni kuwa alikwezwa cheo.

Alitangaza kuwa hivi karibuni wataanza mikutano ya mashinani kufungua afisi maeneo mbalimbali kisha waandae Kongamano la Kitaifa la Chama (NDC).

Kuhusu viongozi wa Jubilee wanaofanya kazi na serikali, Dkt Matiangí alisema hilo ni jaribio la kudhoofisha chama hicho kunufaisha UDA.

“Hatumakinikii kuwatimua kwa sababu tunalenga umoja katika uchaguzi mkuu ujao. Kinachoendelea ni njama ya UDA kulemaza demokrasia,” akasema.