Habari za Kitaifa

Nikipata ODM nitashinda uchaguzi kwa kura 3M – Ruto

Na MOSES NYAMORI January 27th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto sasa anasema muafaka unaoendelea kusukwa kati ya ODM na UDA utamweka kifua mbele kwa angaa kura milioni tatu zaidi ya upinzani.

Alisema muafaka huo utahakikisha anashinda kwa zaidi ya kura milioni tatu kuliko pengo la kura 200,000 alizomshindia marehemu Raila Odinga mnamo 2022.

Aliyatoa matamshi hayo baada ya kuongoza mkutano wa Baraza Kuu (NGC) la UDA linalojumuisha viongozi wote waliochaguliwa kuidhinisha mazungumzo ya muungano na ODM.

Mkutano huo ulihudhuriwa na baadhi ya wabunge waliokuwa wameonyesha uasi ila katika siku za hivi majuzi wakaanza kurejea.

Miongoni mwao ni Mbunge wa Githunguri, Gathoni Wamuchomba na George Koimburi wa Juja.

Mohamed Ali ‘Jicho Pevu’ ambaye ni Mbunge wa Nyali aliyechaguliwa kwa chama cha UDA hakuhudhuria.

Katika kinyang’anyiro cha 2022, Rais alizoa kura 7,176,141 dhidi ya marehemu Raila aliyepata kura 6,942,930.

Kabla ya kifo chake Oktoba 15, 2025, Bw Odinga aliingia kwenye muafaka wa serikali ya muungano na UDA ya Dkt Ruto.

ODM kupitia kamati yake kuu vilevile imemtwika wajibu kinara wa chama hicho Dkt Oburu Oginga kuendeleza mazungumzo hayo.

“Katika uchaguzi ujao, tunataka kushinda kwa kiwango cha kura milioni mbili hadi tatu ili tuendelee kuunganisha nchi na kutembea pamoja. Katika uchaguzi uliopita, tulishinda kwa mwanya wa kura 200,000. Tuna kila sababu ya kuunganisha taifa kuwa moja,” akasema Rais Ruto.

“Tuna rekodi na mpango bora wa kuleta mabadiliko lakini tunahitaji mikakati ya kisiasa kufanikisha malengo yetu na hiyo ndiyo tunafanya na ODM.”

Katika uchaguzi 2022, kaunti 10 za Mlima Kenya na saba kutoka Kaskazini mwa Bonde la Ufa kwa pamoja zilimpa Dkt Ruto kura 4.5 milioni, zilizojumuisha asilimia ya 63 za kura zote alizopata.

Laikipia, Tharaka-Nithi, Murang’a, Kiambu, Nyeri, Kirinyaga, Nyandarua, Embu, Meru na Nakuru kwa jumla zilimpa Dkt Ruto karibu kura milioni tatu.

Akiwa na kura 2,938, 309 za kaunti za Mlima Kenya, Ruto alijazilia kwa kura milioni 1.6 milioni kutoka kaunti saba za Bonde la Ufa Kaskazini.

Eneo la Mlima Kenya, hata hivyo, linaonekana kusonga mbali na utawala wa Kenya Kwanza kufuatia ufurushaji wa ‘mwana wao’, Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua mnamo Oktoba 2024.

Dkt Ruto kwa sasa anaonekana kutegemea uungwaji mkono kutoka maeneo ambayo yamekuwa yakimuunga mkono tangu jadi Bw Odinga.

Katika ugombeaji wake wa urais, 2007, 2013, 2017 na 2022, Bw Odinga alifurahia uungwaji kwa wingi kutoka maeneo ya Nyanza, Magharibi, na Pwani.

Dkt Ruto na naibu wake Prof Kithure Kindiki vilevile wameimarisha kampeni zao katika eneo la Mlima Kenya lenye wingi wa kura baada ya miezi kadhaa ya kilichoonekana kuwa kuogopa kuzuru eneo hilo.

“Rais Ruto, sawa na binadamu mwingine yeyote, ana haki ya kuota na kuota ndoto kubwa anavyopenda. Lakini kuna hekima katika kuepuka kutangaza ndoto kubwa hadharani. Sidhani kuwa ndoto zake ni za uhalisia,” Seneta Enoch Wambua (Kitui) alieleza Taifa Leo.