Habari za Kitaifa

Msururu wa mashambulio tangu ang’atuliwe mamlakani: Nani anawinda Rigathi?

Na MWANGI MUIRURI, GITONGA MARETE January 27th, 2026 Kusoma ni dakika: 3

TUKIO la Jumapili ambapo ghasia zilitokea katika ibada iliyohudhuriwa na aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua eneo la Othaya, Nyeri, limeibua maswali kuhusu ni nani anamwinda kinara huyo wa DCP huku viongozi mbalimbali wakiendelea kukashifu fujo hizo.

Ibada katika kanisa la Kianglikana la Witima, eneobunge la Othaya ilikosa kuendelea Jumapili baada ya Bw Gachagua kuvamiwa huku milio ya risasi na vitoza machozi ikitanda kotekote.

Mali ya kanisa na magari yaliharibiwa, wanawake, watoto na wazee waliokuwa wamehudhuria ibada hiyo wakibaki kuchanganyikiwa kuhusu tukio hilo.

Ghasia ambazo zimekuwa zikiandama mikutano ya Bw Gachagua sasa zimefikia kilele ambapo wengi wanauliza kiini chake na iwapo heshima kwa maeneo ya kuabudu si muhimu tena.

Tangu atimuliwe kama naibu wa rais mnamo Oktoba 2024, Bw Gachagua amekuwa akikumbana na fujo kwenye mikutano yake na kuzua maswali nani anamwinda na kwa manufaa yapi kisiasa.

Mnamo 28, 2024 alivamiwa na watu waliodaiwa kuwa wanachama wa kundi haramu la Mungiki katika hafla ya mazishi Limuru ambapo magari yake yaliharibiwa.

Hali haikuwa tofauti Desemba 2024, alirushiwa vitoza machozi wakati wa mkutano wa kisiasa eneo la Shameta, Kaunti ya Nyandarua.

Visa hivyo viliendelea Februari 2025, mkewe Bw Gachagua, Dorcas, akilazimika kuhepa maombi Kaunti ya Nyeri baada ya vijana kuwasili na kuzua fujo.

Matukio mengine ni Februari 2025 ambapo alivamiwa kwenye ibada ya Kanisa la PCEA Mwiki Nairobi tena katika Kanisa la AIPCA Kigumo, Murangá Julai 2025.

Hayakukomea hapo ambapo alirushiwa vitoza machozi wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo mjini Narok, Novemba 2025.

Mnamo Agosti 2025, vijana walitibua msafara wa Bw Gachagua alipokuwa ameondoka kwenye ziara ya muda Amerika.

Visa hivyo viliendelea mapema mwezi huu ambapo vijana walijaribu kumzuia Bw Gachagua asishiriki ibada Kanisa la AIPCA, Gatundu Kusini, Kaunti ya Kiambu.

Licha ya kuwa visa hivi vimekuwa vikishirikisha maafisa wa polisi ambao wamenaswa kwenye kamera, hakuna hatua zozote ambazo zimechukuliwa dhidi yao. Duru zinaarifu kuwa baadhi hushikwa kisha kuwaachiliwa hata bila kuandikisha taarifa.

Rais William Ruto mnamo Desemba 1 2025 alionekana kusikitishwa na ghasia hizo ambapo alitoa amri kwa polisi kupambana na magenge hatari na wahuni kuzuia taifa kuingia kwenye machafuko.

Jana, Baraza la Makanisa Nchini (NCCK) lilishutumu uvamizi dhidi ya Bw Gachagua kanisani na kusema ulikuwa haramu, kinyume cha katiba na dhihaka kwa mwili wa Mwokozi Yesu Kristo.

Baraza hilo kisha lilitaja matukio sita ambapo waumini wamevamiwa wakiwa makanisani mwao wakiendelea na ibada kwa amani.

“Inasikitisha kuwa katika matukio haya yote, polisi ambao walivunja sheria kimakusudi hawajaachishwa kazi, kuchunguzwa au kushtakiwa mahakamani. Hii huenda inaashiria kuwa serikali inaruhusu visa hivi,” ikasema taarifa ya NCCK.

“Tunataka Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen na Inspekta Jenerali wa Polisi waombe msamaha kwa kanisa na waumini,” wakasema Kasisi Dkt Elias Otieno Agola mwenyekiti wa NCCK na Katibu wake Kasisi Chris Kinyanjui kupitia taarifa.

Mkuu wa Kanisa la Kianglikana Jackson Ole Sapit naye alitoa wito wa uchunguzi wa kina ili wanaohusika na uvamizi makanisani kwenye hafla ya Bw Gachagua wachukuliwe hatua kali.

“Kilichotokea Kanisa la ACK Witima, eneo la kuabudu kinasikitisha sana. Watoto wa Mungu waliumia, wengine wakipambana kupumua na uoga ukitawala. Hekalu ya Mwenyezi Mungu ni mahala pa kuabudu na hakufai kuingiliwa na ghasia,” akasema.

Naye mkuu wa ACK, Jimbo la Mlima Kenya Magharibi Gerald Murithi alisema uvamizi huo ulifanywa kimakusudi wala si ghasia za kujipangia jinsi ambavyo baadhi ya viongozi na wanasiasa wamekuwa wakidai.

Askofu Murithi alitaja uvamizi huo kama mbaya zaidi katika historia ya kanisa na akawashutumu maafisa wa polisi kwa kuhusika moja kwa moja.

“Haukuwa uvamizi dhidi ya mtu mmoja bali waliokuwa wakiabudu, watoto, wanawake na wakongwe ambao waliachwa wameingiwa na uoga. Waumini walikuwa wakihangaishwa huku maafisa wa usalama wakitazama tu na ni vibaya kuwa rasilimali za serikali sasa zinatumika kuwadhulumu wanaotofautiana na serikali,” akasema Askofu Murithi.

Huku viongozi mbalimbali wakiwemo wale wa upinzani wakilaani ghasia hizo, Mbunge wa Mathira Eric Wamumbi alidai kuwa Bw Gachagua amekuwa akijipangia ghasia dhidi yake.

Bw Wamumbi ambaye ni mbunge wa kiongozi huyo wa DCP alisema ana ushahidi na analenga kuandikisha taarifa na maafisa wa usalama.

Naibu Rais Prof Kithure Kindiki, Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen ni kati ya viongozi ambao walikashifu ghasia hizo Jumapili.

Jana aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i alisema kuwa Kenya inaelekea katika machafuko iwapo ghasia dhidi ya viongozi wa upinzani zitaendelea kushuhudiwa.