Habari

Binti ya bwanyenye Devani adai dadake alighushi wosia wa baba yao kuwatapeli

Na RICHARD MUNGUTI January 26th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

BINTI ya bwanyenye Balkrishna Ramji Haribhai Devani alishangaza mahakama ya Milimani alipofichua kwamba dada yake alighushi sahihi ya baba yake mwezi mmoja baada ya kufariki kwake kisha akawatapeli urithi wao na dada mwingine anayeishi nchini Uingereza.

Kalpa Chandarana alishangaa akiwa kortini “ikiwa baba yao alifufuka kutoka kwa wafu akatia sahihi stakabadhi ya kumpa dada yake Dinta Devani Pathanjana mali zote kisha akarudi kaburini.”

Kalpa alisema baba yao aliaga baada ya kuugua kwa muda mrefu akiwa na umri wa miaka 82 na kabla ya kupungia dunia mkono wa buriani alikuwa amewagawia yeye na dada zake wawili mali.

Kalpa Chandarana alipokuwa kortini Januari 26, 2026. Picha|Richard Munguti

“Nakumbuka vizuri baba yetu (Devani) aliaga Juni 7, 2019 lakini aliyoleta katika Mahakama Kuu ya Milimani katika kesi ya urithi wa mali ya baba yetu ilikuwa imetiwa sahihi Julai 12, 2019 mwezi mmoja baada ya kuaga kwa baba,” Kalpa alimweleza hakimu mwandamizi Rose Ndombi.

Akihojiwa na kiongozi wa mashtaka, Kalpa alisema “haiwezekani baba yao kuongoza mkutano wa wakurugenzi wa kampuni ya Pelican Limited na alikuwa ameaga na akazikwa. Hangeweza kufufuka kutoka kwa wafu kutia sahihi makubaliano ya wakurugenzi wa Pelican waliompa Dinta hisa zote za Pelican kisha akarejea mautini.”

Mahakama ilifahamishwa na binti huyo tanzia nyingine kama hiyo ilitokea 2018 na 2019 wakati baba yao alipokuwa ameenda nchini Uingereza kwa matibabu- Dinta na Samuel Ngugi Ndinguri na Addah Nduta Ndambuki walighushi stakabadhi za kuhamisha hisa 131 katika kampuni ya Silverstar kwa Ndinguri.

Kalpa alisema wakati wa zoezi hilo baba yake alikuwa Ulaya.

Alienda Ulaya Julai 12, 2018 na kurejea nchini Feburuari 5, 2019.

Akiwa Uingereza, Devani pamoja na mkewe yadaiwa aliongoza mkutano wa wakurugenzi ambapo walikubaliana Samuel Ndinguri apewe hisa za Dinta katika kampuni ya Silverstar.

Mahakama ilielezwa bwanyenye Devani alikuwa mgonjwa kiasi kwamba “hangeweza kuendeleza shughuli za kampuni zake.”

Kalpa alisema hayo alipotoa ushahidi katika kesi ya ughushi wa Wosia alioandika Devani kuwapora dada zake wawili mali ya baba yao.

Kalpa alieleza mahakama kwamba ameteseka mno kwani katika muda wa miaka saba iliyopita amekuwa akipigana mahakamani kurejeshewa hisa zake katika makampuni ya baba yao marehemu.

Dinta ameshtakiwa pamoja na mumewe Abbay, Samuel na Nduta kwa kula njama kughushi mali za baba yake.

Kesi inaendelea.