Michezo

Nahodha wa U-20 Amos Wanjala ajiunga na Valencia ya Uhispania

Na TOTO AREGE January 27th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

NAHODHA wa Rising Stars ya wachezaji chini ya miaka 20 Amos Wanjala, amejiunga na timu ya pili klabu ya Valencia CF ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), kwa muda usiojulikana.

Kupitia mitandao ya kijamii Jumapili, Valencia iilitangaza kuwa, klabu hiyo imefikia makubaliano na beki huyo mwenye umri wa miaka 19 kujiunga na VCF Mestalla, timu ya pili ya klabu hiyo.

“Valencia CF imefikia makubaliano ya kumjumuisha Amos Wanjala katika kikosi cha VCF Mestalla,” Valencia walitangaza kupitia mitandao yao ya kijamii.

“Amos Emmanuel Wanjala, 19, ni beki wa kati ambaye anajiunga na VCF Academy kutoka Athletic Club Torrellano, na kuwa sehemu ya timu ya Valencian ambayo imeshiriki katika Kombe la Mikoa la UEFA. Beki huyo mpya wa Valencia ni mchezaji wa kimataifa wa Kenya na alikuwa nahodha wa timu ya taifa yake ya chini ya miaka 20 katika Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka jana,” taarifa hiyo ilisema.

Mestalla inashiriki Ligi ya Divishen B, ambayo ni ngazi ya nne ya ligi ya Uhispania.

Wanjala alianza safari yake ya soka ya Ulaya mwishoni mwa 2023 baada ya kupata udhamini wa kwenda Nastic Sports Academy huko Tarragona, Uhispania.

Aliwavutia maskauti katika Michezo ya Kitaifa ya Shule za Sekondari ambako alichezea timu St Anthony’s Boys High School Kitale na michuano ya Talanta Hela.

Mnamo Agosti 2024, Wanjala alijiunga na klabu ya Athletic Club Torrellano CF ya ngazi ya tano ya Uhispania hadi alipohamia Mestalla.

Alikuwa sehemu ya kikosi cha Harambee Stars kwa mechi za kufuzu kwa AFCON 2025 dhidi ya Zimbabwe na Namibia, ila hakucheza.