Mashairi

Mjoli nakuombea

January 27th, 2026 Kusoma ni dakika: 3

Mjoli ondoa shaka, nakutakia makuu,
Ya mwili kunawirika, uwe na afya nafuu,
Unatimiza miaka, themanini mwaka huu,
N’nakuombea Mungu, akulinde maishani.

Ni Mjoli wa Shekina, ndu’ Wilson Muchai,
Nakuombea Rabbana, akuongeze uhai,
Uishi maradhi huna, wendelee kunirai,
N’nakuombea Mungu, akulinde maishani.

Umri wako mpana, mkubwa kuuratili,
Hauko kwenye ujana, shahidi ni wako mwili,
Uzee una kubana, kimwili na kiakili,
N’nakuombea Mungu, akulinde maishani.

Mwaka huu Aprili, watimiza themanini,
Anijalie Jalali, ningali kwenye sitini,
Miaka hiyo kwa kweli, na mimi isinihini,
N’nakuombea Mungu, akulinde maishani.

Mungu akujaze afya, ya akili na ya mwili,
Uishi upige chafya, uwashitue wa mbali,
Wakizuka wenye pufya, washindwe kukuhimili,
N’nakuombea Mungu, akulinde maishani.

Ba Mjoli wa Shekina, ni zako hizi salamu,
Mbogholi nakupa tena, wewe ni mtu muhimu,
Naomba uishi sana, ili unipe elimu,
N’nakuombea Mungu, akulinde maishani.

Umekuwa mshairi, muhimu moyoni mwangu,
Kwani moyo wenye siri, hata ungie machungu,

Una siri ya sifuri, mjuzi wa pili Mungu,
N’nakuombea Mungu, akulinde maishani.

Kwangu wewe ndio taa, au miwani ya macho,
Usije ukashangaa, wasemavyo chembilecho,
Kijinga cha kuni kaa, kiivishacho ni hicho,
N’nakuombea Mungu, akulinde maishani.

LUDOVICK MBOGHOLI
AL – USTADH – LUQMAN
NGARIBA MLUMBI (006)

Pesa ya mme tamu

Si kwamba n’na bwabwaja, na pia sina wazimu,
Nataka nena na waja, maneno myafahamu,
Dunia ina vioja, toka zama za Adamu
Pesa ya mme ni tamu, hata kama peni moja.

Tembea hata Naija, dunia utafahamu,
Pesa ya mme ni tija, hata kama ina sumu,
Inatibu wenye haja, hata na wenda wazimu,
Pesa ya mme ni tamu, hata kama peni moja.

Mke awe na daraja, Rais au makamu,
Hata awe ana koja, na makoja ya elimu,
Penye mme atangoja, akiona darahimu,
Pesa ya mme ni tamu, hata kama peni moja

Msidhani ni mauja, haya ninotakalamu,
Utampiga pambaja, na maneno tamu tamu,
Kama huna mkongoja, wa pesa tajilaumu,
Pesa ya mme ni tamu, hata kama peni moja.

Mme nyumbani akija, kawaida hujikimu,
Sukari Na kilo moja, ya nyama au Saumu,
Ataitwa bwana meja, na kuwekwa tabasamu,
Pesa ya Mme Ni tamu, hata kama peni moja.

Msone najikangaja, mkaja kunilaumu,
Hata uwe ni mseja, hujaoa walazimu,
Utaviona viroja, pesa kumbe ni wazimu,
Pesa ya mme ni tamu, hata kama peni moja.

MSHAIRI WETU,
KITALE

Mwambieni nampenda

Ninajifunza kutunga, japo sijakuwa gwiji,
Kuna jambo nimelenga, wala si la kufariji,
Najua ulinitenga, kwangu uko muuaji,
Mwambieni nampenda, arudi tuje tuishi.

Sitasema kwa ubaya, ila kwako mejifia,
Kusema sioni haya, kwako ninajisikia,
Nayakumbuka mabaya , yote nilokufanyia,
Mwambieni nampenda, arudi tuje tuishi.

Makosa nimeshakiri, naapa sitorudia,
Wewe ni wangu sayari, kwani ndo wanijulia,
Kukuacha si tayari, leo mimi nakwambia,
Mwambieni nampenda, arudi tuje tuishi.

Nisamehe wangu hayuni, waniumiza mtima,
Naomba rudi nyumbani, kuwa japo na huruma,
Kwangu yuko na thamani, hilo wazi nalisema,
Mwambieni nampenda, arudi tuje tuishi.

Habari nimezituma, naomba zifike kwake,
Moyo wangu umezima, naomba anikumbuke,
Nilipo sasa nahema, ninataka atamke,
Mwambieni nampenda, arudi aje kuishi.

Hapa ninafunga beti, kunena kumenishinda,
Unanicheka umati, msikivu ninakonda,
Naona sina bahati, mapenzini niko kinda,
Mwambieni nampenda, arudi tushe tuishi.

ONESMUS KATANA,
MALENGA MSIKIVU,
KILIFI

Siwezi chiti

Natuma zangu salamu, zende kwa wangu waridi,
Ye Hawa mie Adamu, Mungu kanipa zawadi,
Kila siku tabasamu, sio uchungu wa jadi,
Nimependwa kihakika, mwenzenu siwezi chiti.

Jina za uarabuni, nyonda anita habibu,
Makopakopa simuni, kumwacha sina sababu,
Nala vya uswahilini, penzi lenye unasibu,
Nimependwa kihakika, mwenzenu siwezi chiti.

Ukizona zake mboni, naapa upo tabani,
Kinikumbatia hani, chuchu zandunga kifwani,
Nimerudi utotoni, jina langu ni nani,
Nimependwa kihakika, mwenzenu siwezi chiti.

Mapishi habahatishi, kuoka vya mafutani,
Vilivyo virutubishi, protini na vitamin,
Kukumanga tena freshi, wanga na mdalasini,
Nimependwa kihakika, mwenzenu siwezi chiti.

Sijasema ya chumbani, kiuno chake bedini,
Switi, bebi pia hani, lakabu zangu chumbani,
Mabusu yake shavuni, mabusu yangu komoni,
Nimependwa kihakika, mwenzenu siwezi chiti.

Malenga hapa nafika, ujumbe upo simuni,
Asema ananitaka, nifike mwetu chumbani,
Siruhusiwi kutoka, mmenona shukuruni,
Nimependwa kihakika, mwenzenu siwezi chiti.

EZEKIEL NZEKE (KARMA)
MIKOBA YA BABU
CHUO KIKUU CHA MURANG’A

Ndovu Kichaa

Niruhusuni kusema, kwa kalamu kuandika,
Nudhumu hii mapema, natunga kulalamika,
Madhila yanatwandama, usalama ‘metutoka,
Ndovu kichaa balaa, serikali saidia!

Serikali saidia, kuwaweka pa salama,
Hapo nawakatulia, na vurugu ikakoma,
Wakazi ‘tafurahia, kwa amani ‘tasimama,
Ndovu kichaa balaa, serikali saidia!

Majeruhi wapo sana, makovu hayajapoa,
Kwa suluhu watapona, maisha yakendelea,
Dawa yao sanasana, ni ndovu kuwaondoa,
Ndovu kichaa balaa, serikali saidia!

Hasara sije sahau, ni mengi wamepoteza,
Shambani ‘mekula huu, mazao waliyokuza,
Twawalilia wadau, kwa sauti tunapaza,
Ndovu kichaa balaa, serikali saidia!

Ndovu wameleta vifo, wakati wa kwafurusha,
Wengi ‘melala fofofo, hakuna wa kuwamsha,
Wajane wa hivi vifo, wamelia imetosha,
Ndovu kichaa balaa, serikali saidia!

Kalamu naweka chini, mwisho hapa nimefika,
Sehemu hizi nchini, hasa ni mbuga tajika,
Laikipia jamani, Taita na kadhalika,
Ndovu kichaa balaa, serikali saidia!

CHRISTOPHER MUSA KALUNDA
Malenga Mwepesi
AIC VISA OSHWAL-KABARNET