Habari

Wawaniaji uchaguzi 2027 walipa donge kukutana na Ruto

Na MOSES NYAMORI January 28th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

CHAMA tawala cha United Democratic Alliance (UDA) kimeandaa mpango wa kukusanya mamilioni ya pesa kutoka kwa wawaniaji wa uchaguzi mkuu wa 2027 wanaopanga kuhudhuria mkutano wa Ikulu wiki ijayo.

Chama kimeunda tovuti na kimewataka wote wanaotaka kuwania nafasi kwa tiketi ya UDA kujisajili kabla ya mkutano na Rais William Ruto mnamo Februari 4.

Ingawa lengo ni kuimarisha mtandao wa kisiasa kutoka mashinani hadi juu katika maandalizi ya uchaguzi wa urais wa 2027 na pia kupima ushawishi wa chama katika ngazi za kitaifa, tovuti inatoa kipato cha haraka kutoka kwa maelfu ya wagombea wanaotaka tiketi ya chama.

Kufikia jana, UDA ilikuwa imekusanya karibu Sh17 milioni, na chama kinatarajia kiasi hiki kuongezeka katika siku saba zinazobaki.

Kulingana na taarifa iliyotolewa Januari 21 na Mwenyekiti wa Bodi ya Uchaguzi ya Chama Anthony Mwaura, wawaniaji wa udiwani wanatakiwa kulipa Sh2,000 kujiunga na mkutano, wale wa Wabunge, Wawakilishi wa Wanawake na Seneta Sh5,000, na wagombea wa ugavana Sh10,000.

Wale wanaotaka kuwania tiketi ya urais ya chama walipewa ada ya Sh100,000.

Mwaura aliambia Taifa Leo kuwa kufikia jana asubuhi wagombea 4,200 walikuwa wamejiandikisha kuwania nafasi za MCA.