Habari za Kitaifa

Mmejishusha bei: Spika Wetang’ula ashutumu ulaji hongo katika Bunge

Na SAMWEL OWINO January 28th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

UADILIFU wa wabunge wanapotekeleza majukumu yao ya kikatiba katika kamati za Bunge umetiliwa shaka tena huku Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula akiwaonya vikali wabunge dhidi ya matumizi mabaya ya mamlaka yao.

Bw Wetang’ula amewataka wabunge wazingatie sheria na maadili ya kazi ya Bunge akilaumu kamati kwa kula hongo.

Bw Wetang’ula alisema kuna dalili zinazoashiria kuzorota kwa uhusiano kati ya wabunge na maafisa wa Serikali, akibainisha kuwa, baadhi ya wabunge wamegeuza kamati za Bunge kuwa majukwaa ya kujinufaisha kibinafsi.

Alidai kuwa wapo wabunge wanaodai hongo au kuwatumia mawakala, wanaoitwa “maafisa wa ustawi” ili kushinikiza maafisa wa Serikali kutoa pesa kwa matarajio ya ripoti au uamuzi unaowapendelea.

Spika alisema amepokea malalamishi mengi kutoka kwa maafisa wa Serikali wanaodai kunyanyaswa na hata kutishwa wanapofika mbele ya kamati za Bunge.

Alisema hali hiyo imeharibu taswira ya Bunge na kudhoofisha jukumu lake la msingi la usimamizi wa serikali.

“Kuna mwenendo wa kutia wasiwasi katika baadhi ya kamati zetu. Kila kunapokuwepo mchakato wa uajiri katika taasisi za umma, wakuu wa taasisi hizo huanza kuitwa mara kwa mara mbele ya kamati mbali mbali kuhusu hoja ile ile,” alisema Wetang’ula.

Akizungumza wakati wa kikao cha Bunge la Kitaifa kilichofanyika Naivasha, Spika alieleza masikitiko yake kuwa baadhi ya wabunge wamejipatia majukumu yasiyo rasmi katika kamati zao na kutumia nafasi hiyo kuwatapeli maafisa wa Serikali.

“Ninapokea malalamishi mengi kuwa baadhi yetu tunawanyanyasa maafisa wa Serikali wanaofika mbele ya kamati zetu, wengine wakijigeuza kuwa maafisa wa ustawi katika kamati. Haya ni mambo ninayokataza kabisa,” aliwaambia wabunge.

Alifafanua kuwa kwa maana halisi, afisa wa ustawi ni mtu anayeshughulikia masuala ya ustawi wa jamii, lakini katika muktadha wa kamati za Bunge, baadhi ya watu hutumiwa kama wapatanishi wa kukusanya hongo kwa niaba ya wabunge.

Spika alitaja kisa mahsusi ambapo taasisi moja ya umma iliyokuwa na hoja ndogo ya ukaguzi wa Sh400,000 ililazimika kukimbia ofisini kwake baada ya kudai kunyanyaswa na kamati ya Bunge, ambayo hakuitaja jina.

“Nilikutana na kesi ambapo taasisi moja ilikuja ikikimbia ofisini kwangu. Walikuwa na suala ndogo la ukaguzi, lililoelezeka, la takriban Sh400,000, lakini mambo yaliyoibuliwa hayakuwa mazuri kwa heshima ya Bunge,” alisema.

Bw Wetang’ula aliwakumbusha wabunge kuwa jukumu la usimamizi ni la kikatiba na halipaswi kutumiwa vibaya. Alisema lazima litekelezwe kwa njia inayoheshimu sheria, taasisi nyingine za serikali na kuepuka kusababisha kukwama kwa shughuli za kiutawala.

“Ingawa usimamizi ni jukumu la kikatiba la Bunge, lazima litekelezwe bila kuunda taswira ya shinikizo isiyofaa au kusababisha kulemaa kwa huduma na usimamizi,” alisema.

Aliongeza kuwa amepokea malalamishi kuhusu makatibu na mawaziri kuitwa kwa wakati mmoja na kamati tatu tofauti za Bunge, jambo alilosema halikubaliki.

Alitaja Inspekta Jenerali wa Polisi na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) kama mifano ya taasisi ambazo zimewahi kuitwa mara nyingi kuhusu masuala yanayofanana.

Kauli ya Wetang’ula imeibua tena kumbukumbu za matukio ya awali ambapo kamati za Bunge zilihusishwa na madai ya hongo.

Katika Bunge la 12, aliyekuwa Spika Justin Muturi aliwahi kutoa mwongozo mkali kuhusu mienendo ya wabunge katika kamati, akipiga marufuku tabia ya wabunge kuwasindikiza mashahidi baada ya vikao, akisema hatua hiyo ilitoa mwanya wa kufanyika kwa makubaliano ya siri.

Katika miaka ya hivi karibuni, Rais William Ruto pia amewahi kukemea vikali wabunge, akiwatuhumu kwa kuendeleza ufisadi kwa kudai hongo kutoka kwa mawaziri, magavana na maafisa wa serikali wanaohusika na masuala ya uwajibikaji.

Historia ya Bunge imegubikwa na sakata kadhaa za rushwa, zikiwemo kuhusu ripoti ya sukari yenye sumu, sakata ya ardhi ya Ruaraka, ripoti ya BBI na madai ya hongo katika kamati za Bajeti na Hesabu za Umma.