Habari za Kitaifa

Maswali dereva wa lori akipatwa amekufa Burnt Forest mzigo wa kahawa ya Sh8m ukitoweka

Na ANTHONY KITIMO January 29th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

FAMILIA moja katika Kaunti ya Mombasa inataka uchunguzi wa kina kufanywa baada ya jamaa wao ambaye ni dereva wa lori la masafa marefu kupatikana amefariki kwa njia tatanishi.

Bw Musyoki Kilundo alipatikana akining’inia kwa mti eneo la Bayete karibu na Burnt Forest, Kaunti ya Uasin Gishu wiki iliyopita, huku kahawa ya karibu Sh8 milioni aliyokuwa akisafirisha kuelekea bandari ya Mombasa ikitoweka.

Bi Eunice Musenya, mkewe, alisema ijapokuwa hajaona mwili wa mumewe, kisa hicho kimemwacha na maswali mengi.

“Kwa sasa hatujui la kufanya lakini uchunguzi lazima ufanywe kwani kifo chake ni cha kutilia shaka,” alisema Bi Musenya.

Mama huyo wa watoto wawili alisema mara ya mwisho kuzungumza na mume wake ilikuwa Alhamisi, Januari 22, saa tisa na dakika 32 alasiri, akimjulisha alikuwa salama njiani kuelekea Mombasa. Hakujua kwamba hayo yangekuwa mawasiliano ya mwisho kati yao.

“Aliniuliza kama abebe nyanya, viazi na karoti, lakini hiyo ndiyo ilikuwa mara ya mwisho kuwasiliana naye. Baada ya hapo nilijaribu kumpata kwa laini zake zote za simu bila mafanikio,” alisema Bi Musenya.

Aliongeza, “Siku iliyofuata nilipokea simu ikinijulisha kuwa mume wangu amepatikana amefariki katika eneo la Bayete karibu na Msitu wa Burnt Forest, Kaunti ya Uasin Gishu.

“Habari hizo zilinishtua sana kwani sikuwa nimetarajia taarifa ya kusikitisha kiasi hicho. Hadi sasa sijaona mwili wa mume wangu, na tukio hili linahitaji uchunguzi wa kina zaidi.”

Kumekuwa na ongezeko la visa vya mashambulizi na uporaji wa bidhaa zenye thamani kubwa katika barabara kuu ya Mombasa–Nairobi hivyo kuathiri uchumi na kuacha familia bila wapendwa wao.

Kulingana na ripoti ya polisi katika Kituo cha Polisi cha Kesses, Kilundo alipatikana ameuawa katika msitu wa Bayete, huku lori lake likiachwa kando ya barabara kuu na mzigo uliokuwa na thamani ya zaidi ya Sh8 milioni kutoweka.

“Lori lenye nambari ya usajili KDB 364A lilipatikana limeachwa kando ya barabara, na baada ya uchunguzi, mwili ulipatikana ukining’inia katika mti mita chache kutoka kwenye lori. Lori lilichukuliwa hadi kituoni huku uchunguzi ukiendelea,” ilisoma ripoti ya polisi.

Hata hivyo, kwa mujibu wa madereva wengine wa malori walio karibu na familia hiyo, tukio hilo lilikuwa la kipekee na limeacha maswali mengi bila majibu.

Chama cha Wasafirishaji Kenya (KTA) kimeeleza wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya madereva wa malori katika Ukanda wa Kaskazini, kikisema visa hivyo vinahitaji kuchunguzwa kwa kina ili kukomesha mashambulizi hayo.

“Tumekuwa tukipokea taarifa za kuongezeka kwa vifo vya madereva na wizi wa mizigo katika barabara kuu, na tumetoa mapendekezo kadhaa ili kukomesha matukio haya. Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kusitisha usafirishaji wa bidhaa zenye thamani kubwa, kama vile kahawa, wakati wa usiku,” ilisema KTA.

Mnamo Januari 23, SGA Security Kenya, kampuni inayohusika na uwekaji alama na ufuatiliaji wa harakati za makontena yote kutoka Malaba hadi Mombasa, ilitoa tahadhari ya kiusalama kwa wasafirishaji wote kufuatia kuongezeka kwa wizi na utekaji nyara wa malori katika mkondo wa Malaba–Mombasa.