Makala

Simu zinazoibwa Kenya husubiriwa kwa hamu na wanunuzi Uganda, Tanzania na Burundi

Na ERIC MATARA, HILLARY KIMUYU January 29th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

SIMU za rununu zinazoibwa katika miji mikuu nchini Kenya huishia katika masoko ya Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi, uchunguzi wa Taifa Leo umegundua.

Maafisa wa upelelezi kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) wamevunja genge la kisasa la wahalifu wanaovuka mipaka wanaohusishwa na mtandao wa wataalamu waliobobea kiteknolojia, wanaorekebisha na kubadilisha simu zilizoibwa kutoka miji mikubwa kama Nairobi, Nakuru, Mombasa, Kisumu na Eldoret kabla ya kuziuza.

Uhalifu wa kuiba simu si tena kazi ya wahuni wa mitaani pekee. Genge hili sasa linahusisha wanawake na wanaume wanaoonekana wa kawaida na wasioweza kushukiwa kuwa wahalifu.

Kukamatwa hivi karibuni kwa washukiwa saba jijini Nairobi wakiwa na simu 150 zilizoibwa kumefichua jinsi magenge ya wizi wa simu yanavyombatia tekinolojia ya kisasa.

Katika oparesheni iliyofanyika Januari 23 jijini Nairobi, iliyoongozwa na Kitengo Maalum cha Operesheni (OSU) cha DCI, washukiwa saba walikamatwa na zaidi ya simu 150 zilizoibwa zikapatikana.

Misako katika maeneo ya Shauri Moyo, katikati ya Jiji la Nairobi, na Kasarani ilifichua simu za kisasa zaidi ya 150, vipatakalishi 16 na tarakilishi sita—vifaa vilivyonyang’anywa raia kwenye foleni za magari na ndani ya matatu.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa DCI Mohamed Amin, baadhi ya vifaa vilivyopatikana vilikuwa vimerejeshwa katika hali ya jinsi vilitoka viwandani, huku vingine vikiwa bado na maelezo ya wamiliki wake halisi.

“Baadhi ya vifaa vilivunjwavunjwa na kuuzwa kama vipuri, jambo linalofanya iwe vigumu kuvifuatilia licha ya uchunguzi unaoendelea,” alisema Bw Amin, akiongeza kuwa oparesheni kama hizo zinafanywa maeneo mengine.

“Tuko mbioni kuwakamata mafundi wanaohusika na watu wanaozisafirisha hadi nchi jirani,” aliongeza.

Miongoni mwa waliokamatwa ni raia wa Uganda anayedhaniwa kuwa kinara wa mtandao aliyeendesha shughuli zake kutoka mafichoni Shauri Moyo. Anadaiwa kuratibu usafirishaji wa simu kutoka kwa wezi wa Kenya hadi kwa wanunuzi wa soko haramu nje ya nchi.

“Yeye ndiye mratibu. Simu ikiibwa Moi Avenue, inafutwa maelezo ya matumizi, inapakiwa upya na kusafirishwa hadi Kampala ndani ya saa 24,” alisema afisa wa DCI.

Upekuzi nyumbani kwake ulipelekea kupatikana kwa simu 75 zilizopakiwa kwenye masanduku yaliyofungwa kwa mkanda wa njano, pamoja na vipakatilishi mbili.

Uchunguzi umebaini kuwa soko tayari katika miji ya Afrika Mashariki linaendeleza uhalifu huu. Ukosefu wa mifumo ya pamoja ya kisheria na kiteknolojia kati ya nchi za Afrika Mashariki hurahisisha wahalifu kukwepa mkono wa sheria.

“Kwa mfano Kampala, simu rahisi ya Tecno huuzwa kwa Sh4,000 pekee,” alisema afisa huyo.

DCI sasa inafanya kazi kwa kushirikiana na kampuni za mawasiliano na Interpol kuvunja mtandao huu wa magendo. Hata hivyo, maafisa wanasema visa vingi vya wizi wa simu haviripotiwi, jambo linalozuia kukamatwa kwa wahalifu.Simu zinazoibwa Kenya uuzwa hadi Burundi