Presha upinzani ukionya IEBC ifanye mabadiliko kabla ya 2027, lau sivyo waite maandamano
MUUNGANO wa Upinzani Jumatano uliongeza shinikizo kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kwa kuwasilisha matakwa na madai yanayohusu teknolojia ya uchaguzi, usalama na uendeshaji wa taasisi hiyo, huku ukionya kuwa kushindwa kuchukua hatua kunaweza kusababisha maandamano ya kitaifa.
Baada ya kikao cha faragha na makamishna wa IEBC, viongozi wa upinzani walisema masuala yao yanahusu uaminifu wa chaguzi ndogo zilizofanyika hivi majuzi na maandalizi ya kimuundo ya Tume kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, wakitoa taswira ya taasisi inayojitahidi kurejesha imani ya umma katika mazingira ya kisiasa yaliyojaa taharuki.
“Haturidhishwi kabisa na mchakato wa ununuzi wa vifaa vya KIEMS na kampuni ya Smartmatic ambayo imelaumiwa kimataifa,” alisema kiongozi wa Chama cha Wiper Patriotic Front, Kalonzo Musyoka, akisema maamuzi ya kiteknolojia yasiyo wazi yamekuwa tishio kubwa kwa uhalali wa uchaguzi.
Zaidi ya kasoro za kiutendaji, upinzani ulitaja IEBC kama taasisi ya kikatiba inayokumbwa na mzozo wa kuaminika, hali hatari katika nchi ambayo chaguzi tata zimekuwa zikisababisha ghasia, kesi mahakamani na msukosuko wa kisiasa.
Kiini cha mzozo ni teknolojia ya uchaguzi, suala ambalo kwa muda mrefu limekuwa mwiba katika siasa za uchaguzi nchini. Bw Musyoka na kiongozi wa Democratic Action Party–Kenya, Eugene Wamalwa, walihoji chanzo cha mifumo ya kielektroniki ya kutambua wapiga kura, wakiihusisha na kampuni zinazokabiliwa na tuhuma nje ya nchi na matumizi tata katika ukanda huu.
“Teknolojia hii hii ilitumika hivi karibuni Uganda. Vifaa vya KIEMS vilikosa kufanya kazi. Hatutaki kuona uchaguzi kama huo Kenya,” alisema Bw Wamalwa, akionya kuwa ukosefu wa uwazi wa kiteknolojia unaweza kuamua matokeo kimyakimya hata kabla kura hazijapigwa.
Hata hivyo, walisema teknolojia ni sehemu moja tu ya tatizo pana. Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, sasa kiongozi wa chama cha Democracy for Citizens Party, aliwaalaumu maafisa wakuu wa serikali na makundi yenye ushawishi wa kisiasa kwa kutwaa vituo vya kupigia kura wakati wa chaguzi ndogo za hivi karibuni.
“Majambazi wao walitwaa vituo vya kupigia kura. Mawaziri walitwaa vituo vya kupigia kura,” alisema Bw Gachagua, akitaja hali hiyo kama kuporomoka kwa mfumo wa usalama wa uchaguzi.
Alionya kuwa iwapo chaguzi ndogo zijazo hazitaonyesha mageuzi ya kweli na kutoegemea upande wowote, basi mgongano wa umma hautaepukika.
“Kuna chaguo la maandamano ya umma. Tunatumai hatutafikia hapo,” alisema.
Upinzani pia ulitaja visa vya rushwa, kukosa kuwafikisha wahusika wa ghasia za uchaguzi mahakamani na kile walichokiita utamaduni wa kutochukuliwa hatua, hali iliyosababisha machafuko kuonekana kama jambo la kawaida katika chaguzi ndogo.
Kwa siri na hadharani, viongozi walionyesha kutoridhishwa kwao na uongozi wa juu wa IEBC, hasa Afisa Mkuu Mtendaji, ambaye wanamchukulia kama mhimili wa udhaifu wa kiutawala ndani ya Tume.
“Kwa hakika hatufurahishwi naye. Tuliweka wazi hilo,” alisema Bw Musyoka.
Ili kuondoka kwenye mvutano wa kisiasa na kuelekea uwajibikaji wa kitaasisi, pande zote zilikubaliana kuunda timu za pamoja za kiufundi zitakazopitia mifumo ya ununuzi, sheria za uchaguzi na mapungufu ya kiutendaji. Hatua hiyo ilitajwa na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i, kama ya lazima ingawa imechelewa.
“Hakuna suala ambalo hatukuliibua—ununuzi, usalama, usimamizi wa chaguzi ndogo, mfumo mzima wa uchaguzi,” alisema Bw Matiang’i.
Hata zoezi la usajili wa wapiga kura kwa wingi, linalotarajiwa kuanza Machi, lilikosolewa, huku viongozi wa upinzani wakionya kuwa muda uliopangwa ni mfupi mno.
Viongozi hao walizungumza baada ya Mkutano wa Kitaifa wa Wajumbe wa Chama cha Democratic Party uliofanyika Ufungamano House, ambapo aliyekuwa Waziri Justin Muturi alitambulishwa kama kiongozi mpya wa chama na mgombea urais, tukio lililoonyesha mshikamano wa upinzani.