IEBC yataka mifereji ya fedha kutoka nje ifungwe uchaguzi usiingiliwe na wageni
TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imewasilisha kwa Bunge la Kitaifa kile inachosema ni mwongozo wa kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki mwaka ujao, ikipendekeza mabadiliko ya baadhi ya sheria na miongozo ya uchaguzi.
Katika orodha yake ya matakwa, IEBC inataka marekebisho yafanyiwe Sheria ya Uchaguzi na Sheria ya Makosa ya Uchaguzi ili iwe na meno ya kung’ata wale wanaokiuka kanuni za uchaguzi.
“Baada ya kuzindua ripoti ya Tathmini ya Uchaguzi ya 2022, Tume ilianza marekebisho ya kisheria ya uchaguzi kupitia majadiliano na wadau mbalimbali. Mpango huu ulikusudia kubaini yale yaliyofanikiwa, mapungufu na kutoa mapendekezo kwa ajili ya marekebisho ya sheria,” Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon, aliwaambia wabunge wanaohudhuria kikao jijini Naivasha Jumatano.
Katika Sheria ya Ufadhili wa Kampeni za Uchaguzi, Tume inapendekeza wabunge wafute na kubadilisha kifungu cha 11 ili kupunguza michango kwenye kampeni za uchaguzi na kuweka wazi wapi michango inakotoka.
Aidha, Bw Ethekon aliwaambia wabunge kurekebisha kifungu cha 14 ili kuzuia michango ya kampeni inayotoka moja kwa moja kwa serikali za kigeni.
Hatua hii, ikiwa itatekelezwa, itakuwa pigo kwa wanasiasa wengi ambao chanzo cha fedha zao za kampeni kimekuwa kikizua utata.
“Kutokuwa na kanuni wazi za nani anayeweza kufadhili kampeni, kiasi gani wanaweza kuchangia na ni wapi fedha hizo zinatoka kunadhoofisha michakato yetu ya kidemokrasia na kufungua mlango kwa ushawishi usiofaa,” alisema Bw Ethekon.
Alionya kwamba kukosa kuweka kanuni za ufadhili wa kampeni kutaweka uhalali wa uchaguzi wa 2027 kwenye hatari.
Japo Sheria ya Ufadhili wa Kampeni za Uchaguzi ilipitishwa mnamo 2013, bado haijatekelezwa kikamilifu kwani kanuni zake hazijapokelewa Bungeni.
Kuhusu kifungu cha kutimua wabunge, Tume inapendekeza kuingiza vifungu vya 27, 28 na 29 vya Sheria za Serikali za Kaunti kwenye Sheria ya Uchaguzi ili kuwe na njia wazi ya kisheria ya wapiga kura kutimua Mbunge.
Mahakama ilitangaza mnamo 2017 kuwa kifungu cha 45(2) cha Sheria ya Uchaguzi kilichotoa msingi wa kuondolewa ofisini kwa mbunge ni kinyume cha katiba, hivyo haki ya kuwatimua wabunge haina msingi.
Katika Sheria ya Makosa ya Uchaguzi, Tume inapendekeza iongezewe nguvu ya kuchukulia hatua wale wanaokiuka kanuni za uchaguzi.
Bw Ethekon alisema kuwa kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu mnamo 2022 kwenye kesi ya Sabina Wanjiru Chege dhidi ya IEBC, hatua zinapaswa kuchukuliwa na Tume, si Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP).
“Mahakama ilithibitisha mamlaka ya Kamati ya Tume ya kusimamia Kanuni za Maadili ya Uchaguzi,” alisema.
Aidha, Tume inapendekeza ufafanuzi wa alama za wagombea huru ndani ya kaunti, pamoja na kurekebishwa kwa mchakato wa uteuzi na usajili wa wagombea ili kuwa na uwazi wakati wa ukaguzi wa teknolojia ya uchaguzi.
Bw Ethekon pia alisisitiza umuhimu wa bajeti ya kutosha, akisema Tume inahitaji Sh63 bilioni kwa maandalizi ya 2027 lakini Wizara ya Fedha imeitengea Sh41 bilioni tu.
“Pengo hili linapunguza uwezo wa Tume kutekeleza shughuli hizi kwa ufanisi,” alisema.
Kuhusu ghasia za kisiasa, Bw Ethekon alisema ni vyama vya siasa vinavyopaswa kubeba jukumu kuu, si IEBC.
Spika wa Bunge, Moses Wetang’ula, aliagiza Kamati ya Sheria na Masuala ya Kikatiba (JLAC) na Kamati ya Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Katiba (CIOC) kukutana na IEBC ndani ya wiki moja ili kuharakisha utekelezaji wa mapendekezo yao.
“Naagiza CIOC na JLAC kukutana na IEBC ili kushughulikia matakwa yao ndani ya miezi minne ijayo,” alisema Bw Wetang’ula.