Dhima za mbinu za kimtindo katika kitabu ‘Mapambazuko ya Machweo’
MBALI na nyimbo na barua, kuna mbinu nyingine zitumikazo kutekeleza majukumu mahususi katika hadithi fupi.
Maswali balagha ni yale ambayo majibu yake yanajulikana. Huulizwa ili kumchochea msomaji atafakari jambo. Katika ‘Fadhila za Punda’, mabadiliko katika tabia za Luka yanaangaziwa.
“Mbona Luka akageuka kuwa mzigo wa moto, habebeki, habebeki kamwe?” (Uk.1). Yanaweza kutumika kusisitiza wazo.
Katika ‘Msiba wa Kujitakia’, unyonge wa wananchi unasisitizwa.
“Pana haja gani ya kuendelea kushiriki zoezi hilo ikiwa wananchi wataendelea kulimbikiziwa viongozi wasiowataka?” (Uk.13). Aidha, hutumika kuwasuta watu mui.
Katika ‘Mapambazuko ya Machweo’, polisi waliomnasa Mzee Makutwa wanamkosoa.
“Mnadhani nchi itakuwa na viongozi gani kesho ikiwa mnawafungia watoto hapa wasiende shule? Hujui ni hatia kuajiri watoto enh?” (Uk. 23).
Kuongezea, maswali balagha hulenga kumzindua msomaji kudadisi mambo. Katika ‘Mzimu wa Kipwerere!’, jamii inazinduliwa kujiepusha na imani za kishirikina.
“Kwa nini mashetani wa mzimu wawe wanaogopwa na kila mtu ilhali …?” (Uk.44). Tathmini ya wazo hili ndilo lililosababisha ugunduzi wa unafiki wa Salihina.
Taswira ni mbinu ya kutoa maelezo ya kina yanayogusia hisi za binadamu; kuona, kuhisi, kusikia, kugusa na kuonja. Taswira oni hurejelea maelezo yanayomwezesha msomaji kupata mkao wa watu au mandhari.
Katika ‘Mzimu wa Kipwerere!’, kuna maelezo kuhusu mkao wa eneo hilo. (Uk.41-42).
Taswira hisi hurejelea maelezo yanayoathiri hisia za msomaji. Katika ‘Sabina’, msomaji anamhurumia kwa kupigwa bila huruma na Yunuke.
“Yunuke alimrukia kama simba anayelivamia windo lake… Kilio cha kwikwi kilimtoka na kuwafanya hata ng’ombe kumsikitikia.” (Uk. 38).
Taswira mwendo hujumuisha mwendo wa wahusika kutoka sehemu moja hadi nyingine.
Katika ‘Harubu ya Maisha’, Kikwai aliitwa na Bosi ofisini mwake kupokezwa habari za kuachishwa kazi.
Anaitwa na Thoma, mhasibu wa kampuni kukabidhiwa mshahara wake. Baadaye anapitia duka- ni kununua bidhaa kabla ya kuelekea nyumbani. (Uk.32).
Taswira sikivu huegemea sauti zinazosikika wakati kuna matukio fulani. Katika ‘Msiba wa Kujitakia’, mlio wa simu unaigwa.
“Ngrrrrrr! …ngrrrrr! Simu ya Fumo Matata ilikiriza.” (Uk. 13).
Taswira mguso huzingatia hisia apatazo mhusika akiguswa mwilini.
Katika ‘Pupa’, Mwakuona alijeruhiwa akitoroka kutoka Chenga-ways.
“… akaruka mara mbili tatu huku akikwaruzwa vibaya na ukuta… Alikokwaruzwa kunawasha.” (Uk.100).
Taswira mnuso huangazia harufu inayotawala mandhari husika. Katika ‘Sabina’, maelezo yanadhihirisha hali yake.
“… Sabina alifika nyumbani… huku harufu ya samadi inamvuka.” (Uk.40).
Tathmini: Jadili matumizi ya taswira katika ‘Nipe Nafasi’.