Habari

Mwalimu alenga kuvunja rekodi kwa kufunza somo la Hisabati kwa saa 45

Na MERCY KOSKEI January 29th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

MWALIMU mmoja wa Hisabati anayeishi Nakuru anajiandaa kukabiliana na changamoto ya kipekee wikiendi hii, akilenga kuvunja Rekodi ya Dunia kwa kufundisha somo la Hisabati kwa muda mrefu zaidi, rekodi ambayo kwa sasa ni zaidi ya saa 31.

Fenwick Maloba, mwalimu wa Hisabati katika Shule ya Upili ya Menengai jijini Nakuru, anapanga kufundisha mfululizo kwa saa 45 akitumia makundi tofauti ya wanafunzi.

Jaribio hilo la kuvunja rekodi linatarajiwa kuanza Ijumaa, Januari 30, saa mbili asubuhi, katika shule hiyo iliyoko eneo la Nakuru Mashariki.

Ili kuandika jina lake katika vitabu vya rekodi, Maloba atalazimika kuvunja rekodi ya sasa ya somo refu zaidi la Hisabati ya saa 31, dakika 42 na sekunde 54, iliyowekwa na Sanusi Kazeem mjini Ilorin, Nigeria, Aprili 12, 2025.

Hatua hii inajiri siku chache tu baada ya Guinness World Records kuthibitisha rekodi mpya ya mwanaharakati wa mazingira kutoka Kenya, Truphena Muthoni, aliyekumbatia mti kwa muda mrefu zaidi wa saa 72 mjini Nyeri kati ya Desemba 8 –11 na kuvunja rekodi yake ya awali ya saa 48.

Kwa mujibu wa Bw Maloba, ambaye amekuwa akifundisha Hisabati na Fizikia katika shule hiyo kwa miaka sita, mpango huo uliopewa jina “Hisabati si jitu, ni mbio za marathon” unalenga kukuza somo hilo, kuwatia motisha wanafunzi kufaulu na kubadilisha mtazamo uliodumu kwa muda mrefu kuwa Hisbati ni ngumu, ya kutisha au ni somo la watu wachache wenye kipaji.

Anasema kuwa kwa juhudi, ubunifu na mtazamo sahihi, Hisbati inaweza kuwa rahisi, ya kuvutia na hata ya kufurahisha.

“Ikiwa ninaweza kufundisha kwa saa 45 mfululizo, basi yeyote anaweza kujifunza Hisabati maishani. Tuinue Nakuru na Kenya katika ramani ya dunia. Nategemea kuungwa mkono na Wakenya wenye nia njema,” alisema Maloba.