Siasa

Tofauti za ODM zajaa pomoni na kusambaa mpaka kwa MCAs

Na KEVIN CHERUIYOT January 30th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MJADALA unaoendelea ndani ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kuhusu nani anapaswa kudhibiti uongozi wa chama hicho kitaifa sasa umehamia katika Bunge la Kaunti ya Nairobi, ambako ODM ina idadi kubwa ya wabunge.

Kile kilichoonekana awali kama mvutano wa mamlaka kati ya kiongozi wa chama, Dkt Oburu Oginga, na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Bi Winnie Odinga, sasa kinatishia kugawanya madiwani wa chama hicho jijini Nairobi.

Makundi mawili yameibuka ndani ya chama, huku viongozi wakuu katika Bunge la Kaunti wakituhumiwa kumuunga mkono Bi Odinga na kwenda kinyume na Dkt Oburu.

Mnamo Jumatano, mapambano hayo ya ubabe yalijitokeza waziwazi pale kundi la madiwani wa ODM lilipozungumza na wanahabari na kutishia kumuondoa Kiongozi wa Wengi Peter Imwatok (MCA wa Makongeni) pamoja na Kiranja wa Wengi Moses Ogeto (MCA wa Kilimani) kwa madai ya kumuunga mkono mbunge wa EALA.

Viongozi hao wawili wa Bunge hilo la kaunti, wamekuwa wakionyesha wazi msimamo wao wa kuunga mkono wito wa mabadiliko ya uongozi ndani ya chama, wakisema kuwa uongozi unapaswa kurejeshwa kwa familia ya Raila Odinga.

Bw Imwatok na Bw Ogeto wamekuwa wakihusishwa kwa karibu na kundi ndani ya ODM linaloongozwa na Katibu Mkuu Edwin Sifuna, Naibu Kiongozi wa Chama Godfrey Osotsi, Gavana wa Siaya James Orengo na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, linaloonekana kushinikiza vigogo wa chama kupisha kizazi kipya cha viongozi.

Kundi hilo linaloongozwa na Seneta Sifuna, linalotajwa kuwa la waasi, pia limekuwa likipinga serikali jumuishi pamoja na mazungumzo yoyote ya makubaliano ya kumuunga mkono Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu ujao.

“Hawawezi kukaa katika nyadhifa za chama na kuendelea kushambulia chama ilhali wanakula meza moja na wapinzani wa chama. Ikiwa hawaungi mkono uongozi wa sasa, wana shughuli gani kushikilia nyadhifa hizo?” alihoji Diwani wa Baba Dogo, Bw Geoffrey Majiwa.

“Kama wao ni wanaume wa tosha, waende wakaunge mkono wale wanaodhani wanawaamini,” aliongeza.

Bw Majiwa alisema wao wanaunga mkono serikali jumuishi kwa kuwa hapo ndipo waliwachwa na aliyekuwa kiongozi wao marehemu Raila Odinga, na kwamba watafuata tu uamuzi utakaotolewa na kiongozi wa chama ifikapo 2027.

“Tunaunga Rais na kiongozi wetu wa chama Dkt Oburu, ambaye anasimamia chama, na tunasema wazi kuwa msimamo wetu kama wanachama wa ODM ni kwamba tunamuunga mkono kikamilifu Dkt Oburu na uongozi wake wote,” alisema Bw Majiwa.

Bw Majiwa alisema wale wanaompinga kiongozi wa chama ni wasaliti wanaopaswa kuchukuliwa hatua, akiongeza kuwa wanawapotosha wafuasi wa chama.

MCA wa Korogocho, Absalom Odhiambo, alisema wale wanaopinga uongozi wa Dkt Oburu hawana nia njema, akiongeza kuwa mabadiliko yatafanyika mara tu madiwani watakaporejea kutoka mapumziko marefu.