Kijana aliyeshtakiwa kuchapisha picha ya Rais Ruto akiwa kwenye jeneza asema hana akaunti X
MWANAFUNZI wa chuo kikuu cha Moi anayeshtakiwa kwa kuchapisha habari za uwongo kumuhusu Rais William Ruto ameeleza mahakama ya Milimani hakuwa na mtandao wa X habari hizo zilipopeperushwa Novemba 13, 2024.
David Ooga Mokaya, alieleza hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani kwamba alikuwa akitumia mtandao wa Twitter na wala sio mtandao wa X.
“Nimeshtakiwa kwa kuchapisha habari za uwongo katika mtandao wa X ilhali nilikuwa natumia mtandao wa Twitter. Habari hizi sio zangu,” Mokaya alieleza mahakama alipojitetea na kuomba aachiliwe huru.
Mokaya aliyekamatwa Novemba 15, 2024 kutoka Eldoret alieleza mahakama ameshtakiwa kinyume cha sheria licha ya madai habari hizo zilikuwa zimetoka kwa simu yake.
Mshtakiwa ambaye alihitimu kwa shahada ya Digirii Somo la Fedha na Uchumi Desemba 2025 alieleza mahakama kesi hiyo ilimsumbua akili na mawazo ilhali Rais William Ruto angali hai.
Akiongozwa kujitetea na mawakili Ian Mutiso na Danstan Omari, Mokaya alieleza mahakama kwamba yeye ni mzalendo na “kamwe hawezi kuchapisha picha ya Rais Ruto akiwa ndani ya jeneza.”
Mwanafunzi huyo alieleza korti mtandao anaodaiwa alitumia ulikuwa unatumiwa na watu wengine watatu.
Mokaya alisema mtandao huo wa“X Space Account” almaarufu- “Landlord@bozgabi” ni ukumbi wa kufanyia biashara na wala sio wa kutuma picha chafu na habari za uwongo.
Alisema mbali na mtandao huo anadhibiti mitandao mingine mitatu ya kufanyia biashara.
Mokaya aliendelea kueleza mahakama kwamba alishtakiwa kimakosa na akaomba mahakama imwachilie huru.
Mokaya aliamibia korti alishtakiwa Novemba 18, 2024 wakati wa maandamano ya “Unga” Wakenya walipoingia barabara kulalamikia bei ya juu ya unga na kupanda kwa gharama ya maisha.
Wakati huo mahakama ilielezwa mitandao ya kijamii ilikuwa inachapisha kila aina ya habari na kwamba “alijikuta katika sokomoko hiyo.”
Mahakama ilielezwa na Bw Omari kwamba ni kesi tu ya Mokaya iliyosalia mahakamani kwa vile amehusishwa na jina la Rais Ruto.
“Kesi za waandamanaji na waliochapisha habari za uwongo waliachiliwa. Ni kesi ya Mokaya tu iliyosalia kortini kwa sababu ya jina la Ruto,” Bw Omari alisema.
Makoya aliambia korti: “Polisi walinishika bila kibali kutoka kwa mahakama kupiga darubini makazi yangu. Walitwaa simu yangu kinyume cha sheria na tarakilishi yangu.”
Mwanafunzi huyo alieleza mahakama wakiwa chuoni walikuwa wanatumia wanafunzi wengi tarakilishi moja na huenda mwanafunzi au mtu mwingine alituma picha hiyo akitumia simu yake iliyokuwa imeunganishwa na tarakilishi.
Mokaya ameshtakiwa kwamba mnamo Novemba 13, 2024, “alichapisha habari za uwongo kuhusu msafara wa idara ya kijeshi ukiwa na jeneza iliyofunikwa bendera ya Kenya ikiwa na mwili wa Rais Ruto.”
Katika cheti cha mashtaka, Mokaya alidaiwa alichapisha habari hizo za msafara huo ukitoka chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee ukiambatana na jeneza lenye mwili wa Rais Ruto.
Hakimu alielezwa Mokaya alichapisha habari hizo katika mtandao wake wa “X Space Account” almaarufu- “Landlord@bozgabi”.
Mokaya alikana shtaka hilo na kuomba aachiliwe kwa dhamana.
Mshtakiwa yuko nje kwa dhamana ya Sh50,000.
Kiongozi wa mashtaka na mawakili wa mshtakiwa watawasilisha taarifa za tetezi za kuachiliwa kwake mnamo Feburuari 5, 2026.