Wakenya wamchangia Maraga Sh8 milioni apige kampeni ya urais
HALI ya kisiasa na uchaguzi nchini Kenya imekolea utamaduni wa kutumia hela na pesa haramu zinazotumika kwenye kampeni za uchaguzi ili kupata ushindi.
Kulingana na Elections Observation Group (ELOG), mtandao wa mashirika ya kiraia yanayofuatilia michakato ya uchaguzi nchini Kenya, wabunge walitumia zaidi ya Sh30 milioni kila mmoja kushinda kiti katika uchaguzi mkuu wa 2022.
Wanasiasa na wale wanaotafuta nyadhifa za kisiasa wanapenda utamaduni huu kwani umasikini na ukosefu wa elimu ya uraia hufanya wapiga kura maskini kuwa rahisi kudanganywa na wanasiasa.
Utamaduni huu unaendelezwa na wanasiasa kama njia ya kudhibiti umma, ikimaanisha kwamba wapiga kura wenyewe ni wahanga wa mfumo huu wa ufisadi.
Hata hivyo, katika hatua inayoashiria mabadiliko kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027, mgombea urais David Maraga, aliyekuwa Jaji Mkuu, tayari amejikusanya Sh8 milioni kupitia michango ya mtandaoni ili kufadhili kampeni yake.
Hadi Alhamisi iliyopita, jumla ya pesa zilizochangwa zilikuwa Sh7.75 milioni kutoka kwa wafuasi 1,834 na watu wengine waliokuwa wakimtia moyo kupitia namba maalumu ya malipo.
Wakenya walio nje ya nchi wametoa michango mingi zaidi, wakichangia zaidi ya Sh6 milioni, huku Maraga mwenyewe akiahidi kuchangia kati ya Sh1 na Sh2 milioni.
Pia amewaahidi wafuasi wake uwazi wa kila senti itakayotumika na kwamba fedha za ziada zitapelekwa kwenye miradi ya umma.
Maraga aliwashukuru wafuasi wake kwa michango yao, akisema ni ishara halisi ya siasa safi nchini Kenya.
“Michango yenu endelevu ni ishara halisi ya siasa yetu kwamba Wakenya wamekuwa wakidai mabadiliko haya kwa muda mrefu. Nanyi wenyewe mnajenga haya mabadiliko. Hii ni safari yenu,” alisema, ingawa hakufichua changamoto alizokumbana nazo au mikakati yake ya kampeni.
Mchambuzi wa siasa, Barasa Nyukuri, anasema kwamba wanasiasa wanahitaji “michezo ya pesa” ili kuwashawishi wapiga kura na hata kununua au kuiba kura.
“Wapiga kura wengi Kenya wamezoea kupokea pesa kutoka kwa wanasiasa na si kinyume chake,” alisema Nyukuri.
Aliongeza kuwa, “wanasiasa wanataka iwe hivyo na ndio sababu wamekataa mabadiliko yoyote ya ufadhili wa kampeni.”
Mgombea huyo wa urais, ambaye alianza kama wakili, kisha kuwa jaji wa Mahakama Kuu, Jaji wa Mahakama ya Rufaa kabla ya kustaafu akiwa Jaji Mkuu na Rais wa Mahakama ya Juu, hana historia ya utajiri mkubwa, hivyo anategemea michango ya wananchi kwa kampeni yake.
Amewaahidi wafuasi wake uwazi na uwajibikaji katika kutunza fedha.
“Ahadi yangu kwenu, kadri inavyowezekana kimsingi, ikiongozwa na uadilifu na kutii katiba, ni uwazi kamili na uwajibikaji katika kutumia rasilmali zenu,” alisema mgombea huyo.
Maraga anaweza kulinganishwa na kiongozi wa zamani wa ODM, marehemu Raila Odinga.
Ingawa watu walimpenda Odinga na mara nyingi kumchagua bila kuwapa pesa, alitegemea ufadhili mkubwa kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa na mashirika makubwa kwa njia ya siri, pamoja na uhusiano wake wa kimataifa.