Habari za Kitaifa

Kindiki apanga kutumia Sh338m kwa usafiri angani kipindi serikali ‘inakaza mshipi’

Na PETER MBURU January 30th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

NAIBU Rais Kithure Kindiki anatarajiwa kutumia Sh338.8 milioni kwa safari za ndege katika mwaka wa kifedha unaoisha Juni 2026, kwa mujibu wa taarifa mpya, huku serikali ikiahidi hatua za kupunguza matumizi kutokana na changamoto za kifedha.

Mipango ya ununuzi kutoka Ofisi ya Naibu Rais, inaonyesha kuwa Profesa Kindiki atatumia Sh150.2 milioni kwa safari za helikopta, Sh144 milioni kwa ndege za kibiashara na Sh44.6 milioni kwa ndege za kukodi kati ya Julai 2025 na Juni 2026.

Kiasi kilichopangwa kwa safari za ndege za Prof Kindiki ni zaidi ya mara tatu ya Sh100 milioni zilizotengewa Mpango wa Basari wa Shule za Upili wa Rais katika mwaka huu, au karibu sawa na Sh350 milioni zilizotengewa Hazina ya Biashara kwa Wanawake, ambayo mamia ya wanawake hutegemea kupata mikopo ya biashara.

Taarifa hizi zinajitokeza wakati Ofisi ya Naibu Rais ilizidisha bajeti yake ya mwaka kwa Sh219.3 milioni ndani ya miezi sita pekee, ikitumia Sh3.2 bilioni dhidi ya bajeti ya mwaka ya Sh2.97 bilioni kufikia Desemba.

Matumizi ya ndege peke yake yatazidi bajeti ya safari zote za ndani na nje ya nchi za ofisi hiyo katika mwaka wa kifedha uliopita kwa Sh88.35 milioni, ikionyesha ongezeko la matumizi yasiyo ya lazima wakati serikali ina changamoto za utekelezaji wa hatua za kupunguza matumizi.

Katika mwaka wa kifedha 2024/25, ofisi hiyo ilitumia Sh250.45 milioni kwa safari za ndani na nje ya nchi, lakini hii inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 35.3 mwaka huu, kutokana na safari za ndege pekee.

Hati zilizopakiwa kwenye mfumo wa ununuzi wa kielektroniki (e-GP) zinaonyesha Ofisi ya Naibu Rais imepanga kutumia Sh409.66 milioni kwa usafirishaji na huduma za posta, ambapo safari za helikopta, ndege za kibiashara na ndege za kukodi zinajumuishwa.

Ofisi pia imetenga Sh150 milioni kwa huduma za helikopta kwa wanawake, vijana na Watu Wenye Ulemavu (PWDs) ambao watagawana karibu sawasawa.

Pia imetoa zabuni 11 za Sh144 milioni kwa safari za ndege za kibiashara na zabuni nne za Sh44.6 milioni kwa ndege za kukodi.

Matumizi makubwa yalikuwa yamepangwa kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Oktoba 2025 hadi Machi 2026.

Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha Ofisi ya Naibu Rais ilitumia Sh43.84 milioni katika robo ya tatu ya mwaka wa kifedha uliomalizika Septemba 2025, sawa na asilimia 10.3 ya matumizi yote ya Sh425.87 milioni ya ofisi hiyo, yote yakiwa kwa shughuli za kawaida.

Bajeti ya Ofisi ya Naibu Rais kwa mwaka wa kifedha 2025/26 ilikuwa Sh3.07 bilioni, ikilinganishwa na Sh3.22 bilioni mwaka wa kifedha 2024/25. Bajeti hiyo ni Sh2.97 bilioni kwa shughuli za kawaida na Sh100 milioni kwa maendeleo.

Ofisi ilizidi bajeti ya Sh2.97 bilioni katika nusu ya kwanza ya mwaka, ikitumia Sh3.2 bilioni kufikia Desemba na kuhitaji bajeti ya ziada.

Ofisi ya Naibu Rais haikujibu maswali kuhusu safari za helikopta, ndege za kibiashara na ndege za kukodi, kiasi kilichotumika katika kipindi cha miezi sita, na safari za ndani na nje zilizoorodheshwa kwenye e-GP.