Tutaandamana- Viongozi wa muungano wa upinzani waambia IG Kanja
MUUNGANO wa Upinzani umetoa makataa ya wiki mbili kwa Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, ukionya kuwa utaitisha maandamano ya kitaifa iwapo idara za usalama hazitawasimamisha kazi na kuwafikisha kortini maafisa wanaotumiwa kuvuruga mikutano yao na wanaopanga na kufadhili ghasia.
Vinara hao pia walitaka uchunguzi huru wa mashambulizi yote ya hivi karibuni.
Viongozi wa upinzani wakiongozwa na kiongozi wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, walitoa onyo hilo katika Jogoo House walipokutana ana kwa ana na mkuu wa polisi nchini.
Walidai kumekuwa na hadi mashambulizi 24 yaliyolenga mikutano, misafara, mikutano ya hadhara na hata ibada za kanisani alizohudhuria Bw Gachagua katika maeneo mbalimbali nchini.
Waliohudhuria mkutano huo ni kiongozi wa People’s Liberation Party Martha Karua, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa Democratic Action Party of Kenya Eugene Wamalwa na kiongozi wa Democratic Party Justin Muturi.