Wito vijana wajitokeze kwa wingi kujisajili kama wapiga kura
HUKU Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027 ukikaribia, viongozi wa chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) wameanzisha kampeni ya kuhamasisha Wakenya kujisajili kwa wingi kama wapiga kura, wakilenga hasa vijana.
Kampeni hiyo inaongozwa na Maseneta maalum Tabitha Mutinda na Hamida Kibwa, pamoja na diwani wa Wadi ya Nairobi Kusini, Bi Waithera Chege.
Viongozi hao wamesisitiza kuwa usajili wa wapiga kura ni hatua muhimu katika kuimarisha demokrasia na kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika maamuzi ya kisiasa.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Nairobi Kusini, viongozi hao waliwataka vijana kujitokeza kwa wingi kujisajili, wakisema kundi hilo lina nguvu kubwa ya kubadilisha mwelekeo wa uongozi wa nchi iwapo litatumia haki yake ya kupiga kura ipasavyo.
“Vijana ndio wengi nchini. Mkipata vitambulisho na kujiandikisha mapema, mtakuwa na nafasi ya kuchagua viongozi wenye maadili na maono ya kulisukuma taifa mbele,” alisema Seneta Mutinda.
Kwa upande wao, viongozi hao pia walitumia fursa hiyo kuhimiza uongozi wa wanawake, wakisema wanawake wana nafasi muhimu katika siasa na maendeleo ya nchi.
Walisema ongezeko la idadi ya wanawake wanaowania na kushikilia nyadhifa za uongozi ni ishara ya jamii inayokua kidemokrasia.
Kando na hayo, viongozi hao walieleza imani yao kwa utawala wa Rais William Ruto wakisema atapata ushindi wa muhula wa pili katika uchaguzi ujao.
Walitaja miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya Kenya Kwanza katika maeneo mbalimbali kama sababu ya imani hiyo.
Kauli zao zilipokelewa vyema na wakazi wa Nairobi Kusini, ambao walisema kuna hatua zilizopigwa chini ya utawala wa sasa, huku wakitoa wito kwa serikali kuendelea kushughulikia changamoto za ajira, gharama ya maisha na huduma za kijamii.