HabariSiasa

'Team Tangatanga' yafufuka

February 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

WANDERI KAMAU, GRACE GITAU, NDUNG’U GACHANE na DPPS

KUNDI la wanasiasa ambao wamekuwa wakimpigia debe Naibu Rais William Ruto kumrithi Rais Uhuru Kenyatta 2022, maarufu kama Team Tanga Tanga, limefufua kampeni hizo baada ya kuwa kimya kwa wiki kadhaa.

Hatua hiyo inaonekana kuwa ukaidi kwa Rais Uhuru Kenyatta, ambaye mwezi jana, aliwataka wanasiasa kukomesha kampeni hizo, hatua ambayo Dkt Ruto aliunga mkono.

Hapo Jumapili, wabunge zaidi ya 25 walikuwa eneo la Bureti, Kaunti ya Kericho kwenye hafla iliyohudhuriwa na Dkt Ruto ambapo walisisitiza kuwa nyuma yake kuhusu 2022.

Wabunge hao hasa kutoka Rift Valley na Mlima Kenya walikuwa ni pamoja na Kimani Ichungwa (Kikuyu), Kimani Ngunjiri (Bahati), Didmus Barasa (Kimilili), Purity Ngirici (Kirinyaga), Catherine Waruguru (Laikipia), Halima Mucheke (Maalum), Faith Gitau (Nyandarua), Tecla Tum (Nandi), Joyce Kameme (Machakos), Hillary Kosgei (Kipkellion Magharibi), Joseph Limo (Kipkelion Mashariki), Japeth Mutai (Bureti), Kipsengeret Koros (Soin/Sigowet) na Nelson Koech (Belgut).

Wengine walikuwa Janet Sitienei (Turbo), Aaron Cheruiyot (Kericho), Fatuma Dullo (Isiolo), Gerusha Momanyi (Nyamira), Beatrice Kones (Bomet Mashariki), Joyce Korir (Bomet), David Sankok (Maalum), Joseph Tonui (Kuresoi Kusini), Wilson Kogo (Chesumei) na Purity Kathambi (Njoro).

“Tutamuunga mkono Dkt Ruto kuingia Ikulu ifikapo 2022. Hii sio kwa sababu ni Mkalenjin, mbali ni kutokana na rekodi yake ya maendeleo,” akasema Bw Ngunjiri.

Bw Ngunjiri na Bw Ichung’wa waliwahakikishia wakazi wa Rift Valley kuwa wenzao wa Mlima Kenya wako imara nyuma ya Naibu Rais kumrithi Rais Kenyatta.

Mnamo Jumamosi, wanasiasa wengine wa kundi hilo waliendeleza kampeni hizo katika ngome ya Rais Kenyatta mjini Karatina, Kaunti ya Nyeri, wakisisitiza kwamba eneo la Mlima Kenya litamuunga mkono Dkt Ruto kwenye uchaguzi huo.

Wale waliompigia debe Dkt Ruto ni wabunge Rigathi Gachagua (Mathira), Kimani Ichung’wa (Kikuyu), Catherine Waruguru (Laikipia), Purity Ngirichi (Kirinyaga) na Gavana Ferdinard Waititu (Kiambu).

“Eneo la Mlima Kenya limepanga kwamba litamuunga mkono Dkt Ruto ifikapo 2022. Hakuna atakayebadilisha uamuzi wetu,” akasema Bw Rigathi, kwenye hafla ya ukumbusho ya kakake, aliyekuwa gavana wa Nyeri, Nderitu Gachagua, ambayo Dkt Ruto alihudhuria.

Bw Ichung’wa alisema hakuna kauli yoyote ambayo itawazuia kuendelea kumfamyia kampeni Dkt Ruto, kwani amedhihirisha utendakazi wake.

“Uamuzi wetu kumuunga mkono Dkt Ruto unatokana na utendakazi na uzalendo ambao ameonyesha kwa Rais Kenyatta. Hiyo ndiyo njia pekee ya kuonyesha shukrani zetu kwake,” akasema mbunge huyo.

Hayo yalijiri huku kundi pinzani la wabunge kutoka ngome ya Rais likiimarisha kampeni dhidi ya “Team Tanga Tanga” na Dkt Ruto.

Kupitia vuguvugu la Jukwaa la Viongozi wa Mlima Kenya na Ng’ambo (MDLF), viongozi hao walisema wenzao katika ‘Tanga Tanga’ wanafaa kukomesha siasa au wajiuzulu kama wanachama wa Jubilee (JP).

Wakiongea eneobunge la Kangema, Kaunti ya Murang’a, wabunge Maina Kamanda (Maalum), Muturi Kigano (Kangema), Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini), Paul Koinange (Kiambaa) na Naomi Shaaban (Taita Taveta), waliwataka wenzao wanaompigia debe Dkt Ruto kujiondoa katika Jubilee.

Katika hafla nyingine, Seneta Irungu Kang’ata wa Murang’a na Mbunge Ndindi Nyoro (Kiharu) walitofautiana huku Bw Nyoro akisisitiza kuwa ataendelea kumuunga mkono Dkt Ruto, naye Bw Kang’ata akichukua msimamo kinyume.

Kwenye agizo lake, Rais Kenyatta alisema wabunge wote wanapaswa kuacha kampeni za uchaguzi wa 2022 na kuangazia maendeleo.wa Jubilee kwamba eneo hilo halitaunga mkono azma yake kuwania urais.