Michezo

Ng'eno bingwa wa Safi Half Marathon Morocco

February 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

BERNARD Kipkorir Ng’eno alitifulia wakimbiaji wenzake vumbi na kuibuka bingwa mpya wa mbio za kimataifa za Safi Half Marathon nchini Morocco mnamo Februari 24, 2019.

Ng’eno, 22, alijizolea Sh314,350 kwa ushindi wake mjini Safi pamoja na bonasi ya kuweka rekodi mpya ya Safi Half Marathon ya saa 1:01:06. Alifuta rekodi ambayo mshindi wa mwaka 2018 Getaneh Molla kutoka Ethiopia aliweka ya saa 1:03:01.

Mkimbiaji huyu, ambaye alishinda Bomet Half marathon mnamo Februari 16, aliingia mbio hizi za kilomita 21 akiwa amepigiwa upatu kutwaa taji. Baada ya kukata utepe, Ng’eno aliambia tovuti ya Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) kwamba alikuwa na uhakika atabeba taji la Safi Half Marathon kabla ya mashindano.

“Nilijua nitaibuka mshindi. Niko katika fomu nzuri,” alinukuliwa na IAAF. Alibadilishana uongozi mara kadhaa na Mkenya mwenzake Edwin Koech na Muethiopia Gizachew Hailu Negasa kabla ya kuwaacha zikisalia kilomita sita. Alikamilisha sekunde 27 mbele ya Negasa naye Koech akaridhika katika nafasi ya tatu kwa saa 1:01:41.

Taji la wanawake lilinyakuliwa na Mtanzania Failuna Matanga ambaye aliwazidi wapinzani wake katika kilomita ya mwisho. Alikuwa bega kwa bega na Waethiopia Asnakesh Awoke Mengesha na Hiwot Ayalew kwa muda mrefu kabla ya kuwazidi maarifa katika mwinuko wa mwisho uliofuatiwa na mteremko. Matanga, 26, alinyakua taji kwa saa 1:10:50 akivunja rekodi ya Muethiopia Meseret Belete Tola ya saa 1:13:27 iliyowekwa mwaka 2018.

MATOKEO (10-BORA)

Wanaume

Bernard Kipkorir Ngeno (Kenya) saa 1:01:06

Gizachew Hailu Negasa (Ethiopia) 1:01:33

Edwin Koech (Kenya) 1:01:41

Othmane El Goumri (Morocco) 1:01:50

Mustapha El Aziz (Morocco) 1:01:56

Faraja Lazaro Damasi (Tanzania) 1:02:20

Ashenafi Moges Weldegiorgis (Ethiopia) 1:03:21

Jaouad El Jazouli (Morocco) 1:03:24

Paul Kibet (Kenya) 1:04:09

Abderrahmane El Moujib (Morocco) 1:04:14

Wanawake

Failuna Abdi Matanga (Tanzania) saa 1:10:50

Asnakesh Awoke Mengesha (Ethiopia) 1:10:57

Hiwot Ayalew (Ethiopia) 1:11:01

Sanae Achahbar (Morocco) 1:12:29

Salome Jepkosgei Kipruto (Kenya) 1:13:15

Gladys Chepkurui (Kenya) 1:13:31

Rkia El Moukim (Morocco) 1:13:37

Neheng Melida Khatala (Lesotho) 1:16:09

Shuba Aman (Bahrain) 1:16:33

Wafa El Gazouir (Morocco) 1:21:08