Michezo

Riara University yazima FC Interdjinamory 2-1

February 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya wasomi wa Riara University iliichabanga FC Interdjinamory mabao 2-1 kwenye patashika ya Kanda ‘A’ kufukuzia ubingwa wa Ligi ya Kaunti ya Nairobi West iliyochezewa uwanja wa Nairobi Prisons. Wanafunzi hao chini ya kocha, Owen Makokha waliteremsha mechi safi huku wakiwinda kuvuna pointi tatu muhimu baada ya kuandikisha sare tatu mfululizo.

Riara ilihangaisha wapinzani wao na kujizolea ufanisi huo kupitia Fidelis Sennah na Nick Oduor waliopiga moja safi kila mmoja.

Hata hivyo, Collins Kakai wa Riara aliikosea timu yake baada ya kuwapa wapinzani wao bao la kufuta machozi alipoteleza na kufunga katika lango lao.

”Hakika tumejaa furaha tele kufuatia matokeo hayo maana hatuna la ziada mbali tumepania kujizatiti kufa na kupona kupigania tiketi ya kupandishwa ngazi msimu ujao,” alisema kocha wa Riara University.

Kadhalika kocha huyo alikiri kuwa kipute hicho kamwe siyo mteremko maana timu zote zimejipanga kujituma mithili ya mchwa kupigania tiketi ya kutwaa taji hilo na kufaulu kusonga mbele.

Nao wachana nyavu Wal Johnson, Rash Mogusu na Paul Ochieng kila mmoja alitikisa nyavu mara moja na kuipiga jeki timu ya Green Santos kubamiza Karen Golf FC mabao 3-0.

Nayo Re Union ilivuna alama moja ilipotoka sare ya bao 1-1 na South B United. Bao la Re Union lilitingwa na Brandon Njoroge. Wakati huo uo katibu wa Re Union, Caleb Ochieng amewaomba wafuasi wao wawe wakifika viwanjani kushabikia wachezaji wao. Kadhalika amerai wahisani wajitokeze kuipiga jeki timu hiyo kwenye kampeni za ngarambe ya msimu huu.

RIARA: Mchezaji wa Cheza Sports (kulia) mwenye jezi ya Njano akishindana na mwenzake wa Riara University kwenye mechi ya fainali ya kipute cha Sub County League mechi iliyopigiwa uwanjani RTI, Nairobi. Kwenye mechi ya juzi Jumapili ya Ligi ya Kaunti ya Nairobi West, Riara University ilikomoa FC Interdjinamory mabao 2-1.