Rodgers, Moyes wako pazuri zaidi kupokezwa ukocha Leicester City
Na MASHIRIKA
LONDON, UINGEREZA
KOCHA wa zamani wa Everton na Manchester United, David Moyes amefichua azma yake ya kudhibiti mikoba ya Leicester City ambao walimtimua Claude Puel mwishoni mwa wiki jana kutokana na msururu wa matokeo duni.
Ingawa hivyo, itamlazimu Moyes kudhihirisha kwamba anawapiku wakufunzi Brendan Rodgers, Rafael Benitez, Harry Redknapp na David Wagner ambao pia wanahusishwa na mikoba ya kikosi hicho.
Japo wakufunzi Mike Stowell na Adam Sadler watawaongoza Leicester leo kuchapana na Brighton, usimamizi wa kikosi hicho umedokeza uwezekano wa kuajiriwa kwa muda ama Michael Appleton au Neil Lennon hadi mwishoni mwa msimu huu.
Moyes hajakuwa na kazi tangu alipofurushwa na West Ham United mwaka jana na huenda rekodi nzuri aliyojivunia kambini mwa Everton ikamfungulia milango ya kuingia ugani King Power.
Licha ya ushawishi wa Moyes kushuka pakubwa alipokuwa akidhibiti chombo cha Man-United, huenda Leicester wakamwajiri iwapo wataambulia pakavu katika jitihada za kujinasia huduma za aliyekuwa kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers.
Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, Leicester wana kiu ya kumwajiri Rodgers na wapo radhi kuwapokeza Celtic kima cha Sh800 milioni ili kuwashawishi kumwachilia mkufunzi huyo mwishoni mwa muhula huu.
Kichapo mara nne mfululizo mbele ya mashabiki wa nyumbani ni kiini cha kutimuliwa kwa Puel wikendi iliyopita baada ya waajiri wake kupepetwa 4-1 na Crystal Palace. Hiyo ilikuwa rekodi mbovu zaidi kuwahi kuandikishwa na Leicester katika kipindi cha miaka 19.
Ushindi haupo!
Mabingwa hao wa EPL mnamo 2015-16 hawajawahi kusajili ushindi wowote tangu Januari 1 na huenda leo ikawa fursa ya kubatilisha matokeo hayo watakapokuwa wenyeji wa Brighton.
Kulingana na Aiyawatt Srivaddhanaprabha ambaye ni Mwenyekiti wa Leicester, kikosi chake kitapania zaidi kujinasia huduma za Rodgers ambaye ubora wa rekodi yake kambini mwa Swansea ulichangia kuajiriwa kwake na Liverpool.
Akihojiwa na wanahabari mnamo Jumapili, Srivaddhanaprabha alikiri kwamba maamuzi ya kutimuliwa kwa Puel yalitokana na msururu wa matokeo duni ya Leicester katika jumla ya mechi tisa zilizopita ambapo walisajili ushindi mara moja pekee.
Aidha, wengi wa wachezaji wa Leicester ambao walikosa kuridhishwa na mbinu za ukufunzi wa Puel walikuwa katika mgomo baridi wa mara kwa mara.