Michezo

Mashabiki wa Gor, NAHD wachemshana mtandaoni

February 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

MASHABIKI wa Gor Mahia waliendelea kujipiga kifua kwamba wataibisha Hussein Dey (NAHD) kwao Algeria, huku Jumatatu wakichemshana na wenzao wa Algeria kwenye mitandao ya kijamii kwa siku ya pili mfululizo.

Ujasiri wa mashabiki wa Gor ‘kuchafua’ hata mitandao ya NAHD kwa maneno makali ulitokana na mabingwa hawa mara 17 wa Kenya kupapura Waalgeria hao 2-0 katika mechi yao ya tatu ya Kundi D ya soka ya Kombe la Mashirikisho la Afrika uwanjani Kasarani mnamo Jumapili.

Maelfu ya mashabiki wa Kenya walifika uwanjani, na baada ya kuingiwa na kiwewe timu yao ilipokosa kuona lango dakika 80 za kwanza, walienda nyumbani wakiwa wamejawa na furaha pale Francis Kahata na Jacques Tuyisenge walipotikisa nyavu dakika ya 83 na 87 mtawalia na kuhakikisha wageni wao wanarejea Algeria mikono mitupu.

Baada ya ushindi huu muhimu na wapili kwa Gor katika kundi hili, K’Ogalo sasa wamechukua uongozi kutoka kwa NAHD.

Gor ya kocha Hassan Oktay imo kileleni kwa alama sita baada ya kuchapa Zamalek ya Misri 4-2 uwanjani Kasarani na kupoteza 2-1 dhidi ya Petro de Luanda nchini Angola katika mechi mbili za kwanza.

Mwanya 

Vijana wa Oktay wamefungua mwanya wa alama mbili dhidi ya wapinzani wao wa karibu Petro na NAHD nao Zamalek wanavuta mkia kwa alama mbili. Gor itaalikwa nchini Algeria mnamo Machi 3.
Mashabiki wa Gor na NAHD wamerushiana maneno makali, ambayo hatuwezi kuchapisha kila mmoja akivutia kamba upande wake.

Mashabiki wa NAHD wameahidi Gor mapokezi duni wakidai kwamba klabu yao “haikupokelewa vyema wala kupewa basi ama uwanja wa kufanyia mazoezi.”

Shabiki wa Gor Mahia ashabikia timu yake ilipokabiliana na Hussein Dey Februari 24, 2019, uwanjani Kasarani. Picha/ Sila Kiplagat

Nao mashabiki wa Gor almaarufu Green Army, wamesema hawatishiki na vitisho kutoka kwa Waalgeria hao na wako tayari kuwaaibisha katika ardhi yao.

Wachezaji wa Hussein Dey Ahmed Gasmi na Hocine El Orf walipata majeraha katika mechi ya kwanza kabisa kati ya klabu hizi, huku Chamseddine Harrag akilishwa kadi nyekundu.