MAPOZI: Lenana Kariba
Na PAULINE ONGAJI
KATIKA uwanja wa uigizaji, jina lake sio geni ikizingatiwa kwamba tayari ameshiriki katika baadhi ya vipindi na filamu maarufu nchini Kenya.
Licha ya ufanisi huu, kwa Lenana Kung’u Kariba au kwa usahili Lenana Kariba, kama waigizaji wengi nchini, hakijakuwa kibarua rahisi kujitambulisha miongoni mwa mashabiki.
Huku akiwa ameshiriki kwa vipindi na filamu kadha maarufu humu nchini, Lenana amethibitisha kipawa chake kama mmojawapo wa waigizaji wanaotamba sana nchini.
Baadhi ya vipindi na filamu ambavyo ameshiriki ni kama vile How to Find a Husband, Changing Times, Saints, Lies that Bind, House of Lungula na Live or Die miongoni mwa vingine na zingine.
Ni suala ambalo limemvunia sifa na utambulisho mkubwa huku kushiriki kwake katika baadhi ya vipindi maarufu nchini kukimpa nafasi ya kugusana mabega na baadhi ya majina makubwa katika ulingo wa uigizaji nchini ikiwa ni pamoja na Lizz Njagah, Ian Mbugua, na Gerald Langiri miongoni mwa wengine.
Lakini mbali na masuala ya uigizaji Lenana ni msomi kwani ana shahada ya Uanahabari na mauzo kutoka Chuo Kikuu cha Daystar.
Safari yake katika fani ya uigizaji ilianza akiwa bado katika shule ya upili, wakati huo kama mwanafunzi wa shule ya upili ya St. Christophers High School, Nairobi, ambapo alijiunga na chama cha drama.
Lakini cha kushangaza ni kuwa wakati huo uigizaji haukuwa penzi lake, na hivyo kujihusisha kwake na chama hiki kulitokana na sababu kwamba kama mwanafunzi mwingine yeyote, hakuwa na budi ila kujiunga na kikundi hiki.
Hata hivyo ni mtazamo ambao aliubadilisha mwisho wa mwaka wa 2009 baada ya kukamilisha shule ya upili, ambapo kwa usaidizi wa rafikiye alishiriki katika majaribio ya uigizaji katika Kenya National Theatre, na kwa bahati nzuri akapata nafasi hiyo.
Haikuwa muda kabla ya nyota ya muigizaji huyu kuanza kung’aa ambapo mwaka wa 2010 alibisha rasmi kwenye uga huu baada ya kupata nafasi katika kipindi cha Changing Times ambapo aliigiza kama Dr. Max. Kufikia hapa nyota yake ilikuwa inang’aa zaidi kwani mwaka wa mmoja baadaye alikuwa ashajivunia nafasi ingine, wakati huu ikiwa ya kushiriki kwenye kipindi cha Saints.
Kati ya mwaka 2012 na 2014, Lenana alishiriki kwenye kipindi Lies that Bind, huku akiigiza nafasi ya Joseph Juma. Katika kipindi hiki hiki alikuwa mojawapo ya washiriki wakuu kwenye kipindi House of Lungula ambapo aliigiza kama Alex Kijani.
Msururu wa fursa za uigizaji zilizomjia ulizidi kuwa mrefu kwani mwaka wa 2014 aliigiza nafasi ya Boi kwenye filamu Live or Die.
Mwaka mmoja baadaye alipata nafasi ya kuigiza kwenye kipindi cha How to Find a Husband.
Mwaka mmoja baadaye alishiriki katika kipindi News Just In ambapo aliigiza nafasi ya Simon Mambo huku mwaka jana akipata fursa ya kushiriki katika kipindi Selina, nafasi ambayo anaishikilia hadi sasa.
Sekta imenawiri?
Yeye ni mmojawapo wa waigizaji ambao japo bidii yao imedhihirika kupitia kazi zao za ubora wa hali ya juu, bado wanakumbwa na ugumu wa kupata mvuto miongoni mwa mashabiki wa vipindi na filamu nchini.
Huenda ni kutokana na sababu kwamba sekta hii haijanawiri vilivyo nchini.
Licha ya hayo, Lenana hana budi kufurahia mambo ambayo ameafikia kama mwigizaji, na haitakuwa ajabu iwapo hivi karibuni tutaanza kumtazama katika filamu na vipindi vinavyonasa mvuto wa kimataifa.