Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Mkabala wa Ufeministi wa Kiafrika

February 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

MKABALA huu ulihusishwa na bara la Afrika.

Wanawake wa Kiafrika walisisitiza zaidi upinzani dhidi ya utamaduni unaomnyima mwanamke nafasi ya kutekeleza malengo yake.

Miongoni mwa vitengo vya utamaduni huu ni pamoja na:

  1. desturi na mila zinazomdhalilisha kama vile kuonewa kwa mwanamke asiyezaa
  2. kukosa uwezo wa kuchagua kuwa mke au mzazi wa mwanajamii
  3. tohara na ukeketaji wa wanawake
  4. kimya cha kulazimishwa

Kwa mujibu wa Millett (1977), Ufeministi wa Kiafrika umetokana na utamaduni katika jamii iliyojikita katika kilimo na ushirikiano wa kijamii.

Aidha, ufeministi umejengeka katika misingi thabiti ya kumhusisha mwanamke katika shughuli tofauti za jamii bila kuangalia asasi zinazotawaliwa na mwanamume.

Kama anavyofafanua Millett, Ufeministi wa Kiafrika husisitiza usawa katika shughuli za jamii na utoaji wa uamuzi kwa wanawake na wanaume.

Kwa upande wake Strobel (1980), anauona ufeministi wa Kiafrika kama uliokumbana na changamoto nyingi kutokana na asasi tofauti kwa sababu huwa unataka kujua chanzo cha ubaguzi katika maswala ya kiutawala.

Mwelekeo pinzani unasisitiza uongozi wa jinsia ya kiume ambao umeupa changamoto nyingi sana mwelekeo wa Ufeministi wa Kiafrika.

Naye Steady (1981), anasema kuwa Ufeministi wa Kiafrika unajikita katika misingi inayoangalia majukumu tofauti ya kijinsia kama yanayotegemeana na kukamilishana, yenye usambamba na usawa katika kuiendeleza jamii. Aidha,  anaeleza kuwa Ufeministi wa Kiafrika huweka pamoja maswala ya kijinsia, ubaguzi, utabaka na mielekeo tofauti ya kiutamaduni ili kuibua Ufeministi unaomwangalia mwanamke kama kiumbe lakini sio kama kiumbe kijinsia.

Anaongezea kuwa Ufeministi wa Kiafrika huchunguza maswala ya kitamaduni yanayomlenga mwanamke. Isitoshe, hushughulikia maswala ya kijinsia kwa kujikita katika muktadha wa Kiafrika.

Ni vyema kufahamu kwamba nadharia ya ufeministi ina sifa kuu bainifu zinazoitenganisha na nadharia nyinginezo katika uhakiki wa fasihi.

Tutachunguza na kupambanua kwa kina sifa hizo au ukipenda mihimili ya nadharia ya ufeministi ili kupata uelewa wa wazi zaidi kuhusu nadharia hii na kuweza kuitumia ipasavyo katika stadi zetu za fasihi katika viwango mbalimbali.

Marejeo

Wamitila, K. W. (2003). Kamusi ya Fasihi: Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus.

Wa Thiong’o, Ngugi (1998). Penpoints Gunpoints and Dreams. Oxford: Clarendon.

Wellek Rene & Austin Warren ( 1986). Theory of Literature. Harmondworth: Penguin