Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Viambajengo vya Nadharia ya Udhanaishi katika Fasihi

February 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

KWA mujibu wa Soren Kieregaard, mtu haishi kwa nguvu zake mwenyewe kwa kuwa kuna nguvu zinazomtawala ambazo ni za Mungu.

Aidha, anasema kwamba binadamu anapoishi hutenda dhambi na ili apate utulivu wa kiroho inambidi atubu dhambi hizo.

Wanaamini kuwepo kwa Mungu kwa binadamu wote.

Mwanafalsafa huyu anaeleza kuwa ashakum si matusi, binadamu ni kikaragosi cha nguvu zilizomuumba. Ni katika kuzicha ndipo mtu huyu hupata utulivu wa kiroho.

Kulingana naye, udhanaishi ni dhana ya hofu pale ambapo binadamu huogopa adhabu kutoka kwa Mungu kwa hivyo amegubikwa na wasiwasi hataki  kumkosea Mungu na kuhimiza ubinafsi wa binadamu.

Friedrich Nietzche (1927) katika kazi yake ya ‘Joyful Wisdom’ anasema kuwa mungu amekufa.

Tamko hili lake pamoja na misimamo ya wenzake vinakuwa misingi muhimu ya kuzuka kwa udhanaishi wa ukanaji-mungu.  Nadharia hii ilishika kasi baada ya vita vikuu vya dunia ambapo watu walikata tamaa maishani.

Kulingana na wanafalsafa walioshikilia dhana hii walidai kuwa mtu anapozaliwa, hujipata ametumbukia katika ombwe la aina fulani. Aidha,  mtu yuko huru kuishi tu na kukabiliana vilivyo na ulimwengu unaomzunguka.

Mwandishi Kezilahabi ni mwasisi wa nadharia hii katika Kiswahili kwa kuwa kazi zake nyingi zimejikita katika maisha ya binadamu, kama vile ‘Dunia Uwanja wa Fujo’, ‘Rosa Mistika’ miongoni mwa nyingine.

Viambajengo vya Udhanaishi

Nadharia hii imejikita katika nguzo kadha kama ilivyosawiriwa na wanafalsafa mbalimbali.

Kwa kuwa ilizalishwa baada ya Vita Kuu ya Kwanza vya Dunia, wakati binadamu alionekana kukata tamaa, nadharia hii imejikita katika mihimili ifuatayo:

Baadhi ya wanaudhanaishi wanatilia mkazo matatizo halisi yanayomsibu mwanadamu na wanakwepa imani ya kinjozi juu ya imani ya kuishi.

Kulingana na wasomi wa Kijerumani Heidegger na Jaspers, watu walikata tamaa kwa kuwepo kwa wasiwasi na hofu kwa sababu ya giza la fujo na mapambano ya silaha.

Wanafalsafa hawa pia hawaamini uwepo wa Mungu na uumbaji wake wa ulimwengu.

Kwa kuzingatia maafa yaliyokuwa yakiwasibu wanadamu wakati wa vita vya dunia. Madai haya yalipata mashiko miongoni mwa wanafalsafa waliodai kuwa iwapo mungu angalikuwepo basi hangeruhusu watu kuendelea kutenda uovu na kuwanyanyasa watu waso hatia.

 

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo

Mulokozi, Mugyabuso & Kahigi K.(1979). Kunga za Ushairi na Diwani Yetu. Dar es Salaam: Tanzania Publishing House.

Njogu, K. & R.M. Wafula (2007). Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.

Shihabuddin, C. (1970). Utangulizi. Malenga wa Mvita. Nairobi: Oxford University Press.