Makala

GWIJI WA WIKI: Mwanahabari Zubeidah Koome

February 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na CHRIS ADUNGO

UNAPOJITOSA katika ulingo wa uanahabari, la muhimu zaidi ni kufahamu unachokitaka.

Wengi wanapotoka kwa kudhani kuwa uanahabari ni kuonekana runingani na kupata umaarufu.

Ukiwa na mawazo ya sampuli hii, hutadumu kwa muda mrefu.

Lazima pia uwe mtu wa kujitolea na mwenye kujinyima mengi. Sawa na polisi na madaktari, wanahabari huhitajika kuwa kazini kwa muda mrefu.

Chipukizi wawe wenye subira ndipo wapae kutoka kiwango kimoja hadi kufikia wanakotamani. Unaweza kupatwa na majaribu ya kutaka kuhusiana kimapenzi na mkuu wako ili upandishwe cheo, upendelewe kazini au upate ajira.

Jihadhari sana na ujue kwamba nidhamu, msimamo thabiti na uadilifu hukupa heshima na taadhima miongoni mwa wanataaluma wenzako.

Tambua fani spesheli ambayo utaipalilia kadri unavyopania kukua kitaaluma. Mfano mahojiano, usomaji wa taarifa, masuala ya michezo, biashara, na kadhalika. Uripota na usomaji wa taarifa si kilele cha uanahabari! Una uwezo wa kung’aa katika kitu kingine tofauti.

Huu ndio ushauri wa mwanahabari wa runinga ya KTN, Zubeidah Rose Kananu Koome.

Tueleze kwa ufupi kukuhusu

Zubeidah ni mke, mama na mwanahabari. Navutiwa zaidi na habari, hasa za siasa na afya kutoka humu nchini na kimataifa. Maishani mwangu, sijapenda kabisa kumwona mtu akiteseka wakati nahisi nina uwezo wa kumsaidia. Napenda sana usafi, mazingira na kuzuru mbuga za wanyama. Heri uninyime nyama wiki nzima, lakini usininyime samaki!

Tufafanulie kuhusu maisha yako ya awali

Nilizaliwa katika eneo la Makutano viungani mwa mji wa Meru nikiwa mtoto wa pili katika familia yenye wasichana watatu. Nilisomea katika Shule ya Msingi ya Kaaga iliyoko Kaunti ya Meru, kisha nikajiunga na Shule ya Upili ya wasichana ya St Theresas Riiji iliyoko Meru ya Kati. Hata hivyo, niliondoka shuleni humo baada ya mwaka mmoja kutokana na baridi kali eneo hilo ambalo ni maarufu kwa ukuzaji wa majani-chai. Mwaka wa pili wa shule ya upili nilijiunga na Shule ya Wasichana ya Ruiri iliyoko Imenti ya Kati.

Mara yangu ya kwanza kuondoka Meru ilikuwa mwaka wa 2002 nilipojiunga na Kenya Institute of Professional Studies kusomea Teknolojia ya Mawasiliano (IT).

Nilihisi kuwa hiyo haikuwa kozi ya ndoto yangu ndipo nikaondoka nikiwa mwanafunzi wa Mwaka wa Pili na kujiunga na Cross World Institute na Shang Tao Media kusomea uanahabari.

Nilipopata stashahada katika taaluma ya uanahabari mnamo Januari 2007, nilituma ombi katika runinga ya KTN kwa minajili ya mafunzo ya muda nyanjani (Internship).

Baada ya kuwasiliana kwa simu na aliyekuwa mhariri wa KTN Leo wakati huo Bw Ali Mtenzi, nilifaulu kupata nafasi hiyo na kutokana na bidii yangu na kudura ya Mwenyezi Mungu, sijaondoka hadi sasa.

Nani aliyekuchochea zaidi kukipenda Kiswahili?

Mwalimu wangu katika Shule ya Upili ya Ruiri, Bw Mike Nyaga aliyefanya somo hili kuwa la kusisimua. Alitambua vipaji vyetu, akavipalilia na kuvikuza. Kupitia usaidizi wake, nilivigundua vipaji vyangu vya uimbaji, uigizaji, kukariri mashairi aliyoyatunga na la mno zaidi, uanahabari! Kwa mfano, ningezikusanya taarifa kutoka magazetini na hata mitaani, nikaziandika kwa Kiswahili na kisha kumpa Bw Nyaga azihariri. Ningezisoma taarifa hizo mbele ya wanafunzi wenzagu nyakati za mikutano ya asubuhi gwarideni hasa Ijumaa. Japo nilikuwa mpole, Bw Nyaga alinifunza ukakamavu nikaja kuwa jasiri kila nilipokuwa nikijieleza mbele ya umati.

Mbona ukaamua kujitosa katika ulingo wa uanahabari?

Nadhani nilikuwa mwanahabari hata kabla ya kuzaliwa. Hata ningezaliwa upya hii leo, bado ningechagua kuwa mwanahabari. Niliwahi kuwa mwanachama na mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari katika shule ya msingi na upili. Kwangu, uanahabari si kazi, ni misheni ya maisha!

Majukumu yako katika runinga ya KTN/KTN-News ni gani?

Mimi ni Mhariri wa habari za Siasa katika KTN Leo, mtangazaji na mtayarishi wa Jukwaa La KTN – kipindi cha pekee nchini kinachotoa mafunzo kuhusu ugatuzi na kuangazia jinsi utendakazi unatekelezwa katika kaunti zote za humu nchini. Kipindi hiki hupeperushwa moja kwa moja Jumatatu hadi Almahisi.

Mbali na kuwa ripota, mimi pia huendesha vipindi Dira ya Wiki, Shujaa wa Wiki na Fahamu Lugha Ishara ambacho kinapania kuelimisha umma kuhusu Lugha ya Ishara.

Ni kipi cha pekee unachokifanya tofauti na wenzako kitaaluma?

Kinacholeta tofauti kati ya ripota na watangazaji si hasa tunachokifanya, bali ni jinsi mtu anavyotekeleza majukumu yake.

Kila mtu ana talanta yake ambayo ni tofauti na ya mwenzake. Mimi kwa mfano napenda zaidi siasa. Kuna mwenzangu anayevutiwa sana na masuala ya kijamii, mwingine michezo, afya na kadhalika.

Si kwamba sote hatuna ujuzi wa kufanya taarifa hizi, lakini kuna kitu ambacho mtu akikifanya, humtambulisha na kumpa utofauti. Kuna vitu ambavyo pia vinampa mtazamaji mvuto kwako. Mfano jinsi unavyoyatamka maneno, unavyojieleza, unavyovalia, unavyotabasamu, unavyoendesha mahojiano, na kadhalika.

Nahisi kwamba watazamaji wangu hupenda jinsi ninavyoyafanya mahojiano, muingiliano wangu na ninaowasaili, ninavyomwakilisha mtazamaji kihisia, ninavyouliza maswali kwa niaba yake na pengine ninavyotabasamu!

Ni mwanahabari yupi anayekutia hamasa zaidi kila uchao kutokana na ubora wa kiwango chake?

Christiane Amanpour wa CNN. Navutiwa na ukakamavu wake, anavyouliza maswali na kuviendesha vipindi vyake.

Una maazimio gani ya baadaye kitaaluma?

Kuviboresha vipindi vyangu na hata vya wenzangu ili kuona kuwa vinafikia malengo ya watazamaji. Napania kuyabadilisha maisha ya Wakenya (hata kama ni kwa akali ndogo) kutokana na kazi yangu.

Nitakapostaafu, naazimia kuendeleza mwanga wa uanahabari bora kwa kuwahamasisha chipukizi pindi nitakapopata fursa labda kupitia mafunzo ya vyuo au unenaji wa hadhara.

Mbali na uanahabari, unajishughulisha na nini kinginecho?

Nilikamilisha masomo na kupata Shahada ya Uzamili katika masuala ya Uongozi, Amani na Usalama kutoka Chuo Kikuu cha Africa Nazarene. Nilijiunga tena na Chuo Kikuu cha Nairobi ambako ninapokea mafunzo kuhusu Lugha ya Ishara (Sign Language). Nikiwa afisini, pia najihusisha na miradi mingi ya kuboresha mazingira ya kazi na pia kuinua maisha ya wenzangu.