Makala

WASONGA: Uhuru anasubiri nini kutimua wafisadi serikalini?

February 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI ya Jubilee imekuwa ikijidai kuwa inaongozwa na kauli mbiu ya “Kusema na Kutenda” katika utendakazi wake tangu ilipoingia mamlakani mnamo 2013.

Lakini sasa matukio ya hivi majuzi yanaashiria kuwa Jubilee imefeli kuzingatia kauli mbiu hiyo iliyobuniwa na kilichokuwa chama cha United Republican Party (URP).

Kimsingi, Jubilee inaonekana kushindwa kutimiza ahadi zake kwa Wakenya hata baada ya utulivu kurejea katika ulingo wa siasa baada Rais Uhuru Kenyatta kuridhiana na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.

Kwa mfano, mwezi mmoja baada ya Rais Kenyatta kuahidi kuwa atawafuta kazi mawaziri au maafisa wakuu serikalini watakaotajwa katika sakata za ufisadi, hajafanya hivyo.

Kiongozi wa taifa alitoa ahadi hiyo katika Kongamano la Ufisadi lililofanyika katika Ukumbi wa Bomas mwezi jana, kuashiria kujitolea kwa serikali yake kufanikisha mojawapo ya maazimio kwenye muafaka kati yake na Bw Odinga.

Na juzi akihutubu katika kaunti ya Kisii, Rais Kenyatta aliwataka mawaziri wafisadi wabebe msalaba wao watakapochukuliwa hatua za kisheria.

Kinaya ni kwamba sasa amechelea kuwapiga kalamu mawaziri watatu ambao wakati huu wanachunguzwa kuhusiana na sakata mbalimbali za ufisadi. Wao ni Henry Rotich (Fedha) na Simon Chelugui (Maji), ambao wamehojiwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), baada ya kufichuka kuwa mwanakandarasi mmoja amelipwa mabilioni ya fedha kwa ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, ilhali hakuna kazi imetekelezwa.

Naye Waziri wa Utalii, Najib Balala anaandamwa na EACC kwa tuhuma kwamba aliidhinisha tenda ya thamani ya Sh100 milioni ambayo wizara yake iliipa shirika moja la kitalii kutoka Amerika bila kufuata sheria.

Kulingana na hitaji la Sura ya Sita ya Katiba, afisa yeyote wa umma aliyetajwa katika sakata ya ufisadi anafaa kusimamishwa kazi kwa muda, ili kutoa nafasi kwa uchunguzi dhidi yake kuendeshwa. Na endapo ataondolewa lawama na asasi husika, anapasa kurejeshwa kazini.

Na kulingana na Sheria ya Maadili na Uongozi kwa maafisa wa Umma ya 2012 mienendo ya maafisa wa umma inapasa kuleta heshima kwa ofisi wanazoshikilia.

Chini ya msingi huu, Rais Kenyatta anapasa kuwasimamisha kazi mawaziri wake ambao wanachunguzwa na asasi za EACC na DCI.

Kusimamishwa kazi, kwa muda, kwa mawaziri hao kutatoa nafasi kwa uchunguzi dhidi yao kufanyika katika mazingira huru. Hii ni tofauti na hali ilivyo sasa ambapo huenda wakatumia ushawishi wao serikalini kuvuruga uchunguzi unaoendeshwa dhidi yake.

Ikiwa Rais Kenyatta ataendelea kudhihirishwa kujitolea kwake katika vita dhidi ya ufisadi basi, kwa maoni yangu, juhudi zake kutimiza ajenda zake nne kuu za maendeleo zitaambulia patupu.