Taji ni letu!
Kocha Jurgen Klopp amesema klabu yake ya Liverpool ndiyo iliyo na nafasi kubwa ya kutwaa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kuliko timu nyingine yoyote iliyo kwenye vita hivyo kwa sasa.
Mjerumani huyo alisema kwa sasa klabu yake haifai kulinganishwa na timu nyingine zinazopigania ubingwa wa mwaka huu kwa kuwa kikosi chake kimeimarika zaidi kuliko vyote.
“Liverpool ilishinda ubingwa wa EPL kwa mara ya mwisho mnamo 1990, na kufikia sasa tunaongoza jedwalini kwa tofauti ya pointi moja mbele ya Manchester City (kabla ya mechi za Jumatano usiku), lakini hatujakata tamaa. Matumaini ya kunyakua ubingwa ni makubwa,” alisema Klopp.
Kabla ya mechi ya Jumatano dhidi ya Watford ugani Anfield ambapo wenyeji walishinda 5-0, Liverpool wenyewe walikuwa wametoka sare mara tatu katika mechi zao nne za EPL, ikiwemo sare ya kutofungana mwishoni mwa wiki na mahasimu wao, Manchester United.
Hata hivyo, vita vya kuwania ubingwa vinazidi kuwakosha usingizi mabingwa hao wa zamani ambao wametwaa mara 19.
“Tungekuwa na uhakika zaidi wa kutwaa ubingwa kama tungekuwa na mwanya wa pointi 25 kufikia sasa, lakini tutaendelea kung’ang’ana hadi dakika ya mwisho,” alisema Mjerumani huyo.
“Taji limekuwa likiiponyoka timu hii katika dakika za mwisho, lakini sioni kama hali hiyo itaendelea kutuandama. Nina kikosi ambacho kiko imara kufanya lolote na kuondoa dhana hii mbovu,” alisema kocha huyo.
“Timu imeimarika kiajabu na tutazidi kucheza mechi zilizibakia kwa makali zaidi. Kwa sasa timu iko katika hali njema zaidi kuliko hapo awali. Kila mtu anajua jukumu lake. Muda unayoyoma na ni juu yetu kuamua. Tuna nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa,” aliongeza.
Klopp alisisitiza kuwa wao ndio watakaotwaa ubingwa wa msimu huu.
“Tumejipanga vyema kuliko timu nyingine zinazopigania taji hili,” alisema.
“Vita vya kuwania taji vinazidi kupamba moto lakini tuna matumaini makubwa ya kuibuka mabingwa. Natamani tuendelee kushinda na kubakia kileleni hadi dakika ya mwisho,” Klopp aliwaambia waandishi.
Jordan Henderson alishangaza Jumapili baada ya kukataa kumshika mkono kocha huyo alipoondolewa uwanjani, Jumapili wakicheza na Manchester United.
Klopp hata hivyo amesema hayo yalipita na sasa wanaelekeza macho yao kwa mechi zijazo.
Robert Firmino anatarajiwa kucheza Jumapili dhidi ya Everton, licha ya kutolewa uwanjani Old Trafford kwa machela akiwa katika hali mbaya.
Baada ya nyota huyo kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu, iligunduliwa jeraha hilo halikuwa la kutisha.
Wakati huo huo, kocha wa Real Madrid, Santiago Solari amesema timu yake bado inaweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), licha ya kuwa na pointi 12 nyuma ya vinara FC Barcelona.
Juzi, mabingwa hao wa Ulaya mara tatu mfululizo, walifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Levante na kufikisha pointi 45 huku wakiwa katika nafasi ya tatu jedwalini.
“Nina wachezaji wanaoweza kupambana hadi dakika ya mwisho na tutawashangaza wote wanaotubeza,” alisema.