• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:45 AM
AKILIMALI: Mifuko ya nailoni ilizimwa ikawa bahati mpya kwake

AKILIMALI: Mifuko ya nailoni ilizimwa ikawa bahati mpya kwake

Na STEPHEN DIK

MARY Night Ateka, 33, ni mzawa wa kaunti ndogo ya Maseno, kijiji cha Esivalu, mpakani mwa kaunti ya Kisumu na kaunti ya Vihiga.

Ni mama wa watoto wawili na anafichua kwamba, hadi mwaka wa 2008, alikuwa hana kazi wala mtaji wa kumwezesha kufungua biashara kulea watoto wake kwani yeye ndiye mama tena baba.

Waswahili walisema mtafutaji hachoki akichoka ashapata, rafiki yake wa karibu alimkopesha pesa ambazo zilimwezesha kusafiri hadi Sudan Kusini.

Alipata kazi ya kuhudumia wateja kwa kampuni inayojulikana kama TIN TOLA huko Sudan Kusini, kazi ya kupika vyakula kwa wafanyakazi benki ya KCB ofisini.

Baada ya kuwa Sudan kwa miaka sita akifanya kazi, alirejea nchini Kenya Aprili mwaka wa 2017 na kuamua kuanza biashara mara moja.

Alihamia mjini Busia na kufungua biashara ya kuuza maziwa na mayai kwa bei ya jumla, akiwa na mtaji wa Sh200,000.

Bi Ateka anasema alionelea arudi Kenya kufungua biashara badala ya kuajiriwa, hii ni kwasababu mtoto wake wa kwanza alikuwa katika darasa la saba, anaelekea kufanya mtihani wa darasa la nane mwaka uliofuata. Alitaka kumtayarisha mwanawe vizuri kwasababu alikuwa akielekea kuingia darasa la nane.

Hata hivyo, kwa bahati mbaya, biashara ya kuuza mayai na maziwa ilianguka baada ya miezi mitatu tu.

Aligundua amepata hasara kubwa pia ikizingatiwa kwamba mayai yalikuwa yanavunjika kwa urahisi yanaposafirishwa mbali.

Wauzaji maziwa nao walikuwa wengi ambapo palikuwa na ushindani mkubwa kwa biashara ya kuuza maziwa.

Baada ya biashara kuporomoka 2017, akiwa amebaki na mtaji wa Sh50,000 pekee, Bi Ateka aligeuza mawazo na kuamua kuanza biashara tofauti kulingana na mahitaji ya wateja. Wateja walitaka mifuko mbadala ya kubeba bidhaa, baada ya serikali kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki, juala.

Baada ya serikali kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki, Bi Ateka alifungua biashara ya kuuza mifuko ya kisasa ya kubebea bidhaa inayojulikana kama shopping bags.

Alinunua mifuko hiyo nchini Uganda, mji wa Kampala na pia jijini Nairobi na kuuzia wenye maduka na wafanyabiashara wadogo wadogo kwa bei ya jumla.

Aimarika kibiashara

Sasa Bi Ateka ameimarika kibiashara na hutembelea masoko ya miji mingi katika kaunti ya Busia kama vile Bumala, Matayos na Mundika. Katika kaunti ya Siaya huuza kwa masoko ya Sega, Ugunja, Siaya mjini, Sidindi na Yala. Pia anasafiri kuuza katika soko za kaunti za Kakamega, Bungoma, Kisumu na Vihiga.

Kuna mifuko ambayo Bi Ateka anauza kwa bei ya Sh5, Sh10, Sh15, Sh20, Sh25, Sh30, Sh35, Sh40 hadi Sh50 kwa bei ya rejareja, kuna pia bei ya jumla katika mifuko hii.

Anafichua kwamba yeye hutengeneza zaidi ya Sh100,000 kwa mwezi kwa kuuzamifuko hii ambayo anasema haina msimu.

Bi Ateka amepanuka kimawazo katika biashara hii, kwasababu ana wateja wengi, amekuwa akiangazia mahitaji ya wateja wake ili kuepuka kuuza bidhaa ambazo zimepitwa na msimu.

Bidhaa ambazo wateja wanahitaji zaidi na hawawezi kupata kwa urahisi, yeye husafiri kuenda kuzinunua mbali na kuuzia wateja.

Kwa mfano wakati kama huu ambapo shule zimefunguliwa, Bi Ateka huuza saa za mkononi, vitabu, kalamu, viatu, mikoba ya shule na pia huuza vifaa vya kufanya mazoezi kwa watu wazima.

Wakati wa sherehe za Siku ya Wapendanao, Bi Ateka huuza maua, mavazi mekundu na zawadi kadha wa kadha zinazoambatana na sikukuu hii.

Wakati wanafunzi wanaelekea kufanya mtihani wa kitaifa, yeye huuza success cards na wakati wa Krismasi anauza maua na bidhaa zingine zinaoashiria siku hiyo.

Katika mipango yake ya mwaka huu wa 2019, anapanga kupanua soko la bidhaa zake na kuuza hadi Nakuru, Eldoret na Mombasa.

Atakuwa analenga kuuzia wenye maduka makubwa ya Supermarket bidhaa wanazohitaji wakati wote kama vile mifuko ya kuweka bidhaa.

Hata hivyo, kuna changamoto kadha wa kadha ambazo Bi Ateka anakumbana nazo, kwa mfano wakati mvua inanyesha kwa wingi huwa vigumu kusafiri kwa soko za mbali, na hii humsababishia hasara.

Na pia anahitaji kuwa na bohari la kuhifadhi bidhaa nyingi hasa zile za kuenda kuuza kwa maduka ya jumla.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Kuna jamaa mjini ananitaka ila nahisi ana...

AKILIMALI: Mbunifu wa fasheni aliyeweka mawazo katika...

adminleo