HabariMakala

Kuna busara mabawabu wakipewa bunduki?

February 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na MWANGI MUIRURI

HATUA ya Wizara ya Usalama wa Ndani ya kufichua inapanga kuwahami askari rungu kwa bunduki ili kuimarisha usalama imezua hisia mseto hapa nchini Kenya.

Kuna baadhi wanapinga kwa kauli moja mwelekeo huo, huku wengine wakiunga mkono japo kwa masharti, wote wakiungama pia ikiwa serikali itaamua kuwa hiyo itakuwa sera, basi kuwe na umakinifu mkuu wa kuwahami.

Mkurugenzi wa mamlaka ya kudhibiti utendakazi wa mabawabu nchini, Fazul Mahamud ndiye amefichua kuwa sera hiyo huenda iafikiwe kabla ya Juni 2019, akisema kuwa tayari baraza kuu la kiusalama nchini (NSC) ambapo Rais Uhuru Kenyatta ndiye mwenyekiti limeidhinisha.

Bw Fazul amesema kuwa hatua hiyo imeafikiwa ili kuimarisha sekta ya usalama nchini ambapo kuna uhaba wa maafisa wa kiusalama wa kulinda usalama wa ndani.

“Tukiwahami mabawabu, ina maana kuwa tumeimarisha idadi ya maafisa wanaozingatia usalama hapa nchini, wale ambao serikali inalenga kuhami wakiwa ni wale ambao wanalinda hifadhi muhimu za serikali na pia biashara za kibinafsi,” akasema Bw Fazul.

Dharura ya kuwahami mabawabu imeonekana kushika kasi baada ya magaidi kuvamia jumba la Dusit lililoko mtaani Westlands Jamuari 15, 2019, na ambapo watu 21 walipoteza maisha katika tukio lililodumu muda wa saa 20 maafisa wakikabiliana na magaidi.

Katibu wa muungano wa wafanyakazi nchini (COTU) Bw Francis Atwoli akiunga mkono hatua hii alisema: “Sina shida na uamuzi huo bora tu utekelezwe kwa uangalifu tusiishie kuunda genge jipya ndani ya sekta hii ya usalama.”

Hata hivyo, aliyekuwa Mkurugenzi wa mpango wa usalama wa Nyumba Kumi, Joseph Kaguthi anapinga akisema hili ni wazo la kugeuza sekta ya usalama kuwa hatari na “isiyo na uwajibikiaji bunduki na risasi.”

Anasema kuwa maelezo kuwa mabawabu hao watapewa masomo ya uhamasisho kuhusu bunduki ni kama kejeli ikizingatiwa kuwa hakuna sera maalum nchini ya kitaaluma kuhusu mabawabu.

“Utamuelimisha kwa muda gani na ni mtaala gani utatumika? Mabawabu hao watakaopewa bunduki wataelimishwa katika taasisi gani? Kwan je, ni suala ambalo linaonekana kuwa na busara, lakini kwa undani, ni wazo butu,” asema Bw Kaguthi.

Mbunge wa Embakasi Kusini, Wamwea Gakuya anateta kuwa kuna mtindo wa Wakenya kuingiza siasa katika kila suala, akitaja kuwahami mabawabu kama wazo lenye busara kwa kiwango fulani.

“Hofu yangu kuu ni kuhusu nidhamu katika sera hii. Ikiwa kuna maafisa wa polisi awamehitimu kitaaluma huwa wananaswa katika visa vya utumizi mbaya wa silaha, hawa raia wakipewa bunduki nani atawadhibiti?” ahoji Gakuya.

Boniface Oduor wa Bunge la Mwananchi anasema kuwa sera hii sio ya kushtua.

“Kama kawaida uwezekano ni mkubwa kuna kundi la watu serikalini ambao wamepata fursa ya kuunda pesa kupitia uagizaji silaha,” asema Oduor.

Aidha, anasema kuwa tangu serikali ya Rais Kenyatta ianze kujiingiza katika mikataba ya mikopo “kiholela”, imekubwa na wasiwasi mkuu wa uthabiti wa uchumi na inaunda kila aina ya njama ya kutafuta ushuru wa ziada kutoka kwa kila hali.

“Uliona serikali hii ikizindua msako wa magari mabovu barabarani ikiapa kuwa haitawahi tena kuvumilia ukiukaji wa sheria za barabarani. Sasa enda kwa hizo barabara meizi miwili baadaye na uniambie kama abiria hawabebwi kupita idadi inayokubalika kisheria ndani ya gari moja, uniambie kama vidhibiti mwendo havijachokorwa nay ale magari mabovu hayajarejea barabarani maafisa wakizidi kupokezwa hongo ya Sh50,” asema.

Ada

Anasema kuwa kila kampuni ya mabawabu itahitajika kujisajili rasmi kwa kiwango fulani cha ada na pia kuwe na ada za kupewa bunduki “na ambayo ni Sh27,000 kwa kila bunduki ndogo na Sh55, 000 kwa kila bastola.”

Bw Gakuya anateta kuwa huenda walinzi wa watu mashuhuri ambao wanajulikana kwa kutumia silaha vibaya wanapoandamana na wakubwa wao wazidishe ukosefu wa nidhamu kuhusu silaha.

“Ninawazia kuhusu walinzi wa gavana Mike Sonko ambao wamekuwa wakinaswa katika visa vya kuangazia wazi ukosefu wa kinidhamu kuhusu silaha. Wanafanya hivyo leo kukiwa hakuna sera maalum ya kuwathibiti. Je, hali itakuwa namna gani sera hiyo ikianza kutekelezwa rasmi?” ahoji.

Bw Oduor anasema kuwa hali hii ina utata mwingi kwa kuwa inafahamika wazi kuwa nyingi za kampuni za kibinafsi za huduma za ulinzi huajiri kila aina ya watu na hata wakati mwingine ikiwemo maafisa wa polisi na kijeshi ambao wamefutwa kazi kutokana na ukosefu wa maadili.

Anauliza ni mikakati gani itawekwa ya kuthibiti maafisa hao wa zamani ambao huenda bado wako na kisasi na kufutwa kazi kwao.

“Na wakati unatwambia kuwa utaweka mikakati ya kuwaelimisha watakaopewa bunduki, ni mstakabali upi utatumika ikizingatiwa kuwa huenda mmoja wa mabawabu hao anapata kazi hiyo leo na unamhami, lakini kesho yake anapata kazi kwingine…Hii elimu itakuwa ya kila siku ili kumpa mwingine masomo hayo ili kuzimba pengo la huyo ameondoka?” ahoji.

Aliyekuwa gavana wa Kiambu, William Kabogo anasema kuwa ni heri serikali izingatie kuwaajiri vijana wengi kuwa maafisa kamili wa polisi badala ya kujaribu karata ya kutoa bunduki kwa mabawabu.

Kwa sasa, kuna sheria inaundwa  ya kuhalalisha sera hii, ikiwa ndani ya Mswada wa Private Security Regulation Bill 2010 na ambao umekuwa ukiwekwa pembeni kila mwaka kufuatia pingamizi za wadau muhimu katika sekta ya usalama.

Fazul akiunga mkono pendekezo hili anasema kuwa amefanya utafiti wa kutosha na ako na uhakika ni mpango unaweza ukafaulu.

“Tumetembea katika mataifa ambayo tayari yamekumbatia mpango sawa na huu. Mataifa hayo ni kama Uganda, Morocco na Canada na ambapo mikakati ambayo inatumika huko ndiyo tutaiga na tuiimarishe ili tufaulu,” asema.

Mwenyekiti wa Kenya Security Industry Association, Caxton Munyoki anapuuzilia mbali wazo hili akilitaja kama lililokosa umakinifu wa kiwango chochote.

Anasema kuwa huwezi ukatoa elimu ya kutumia bunduki kwa raia ndani ya wiki mbili na ufikirie taifa liko salama zaidi kuliko hali yake ya awali.

“Tuko na visa ambapo serikali ilitoa bunduki kwa rais katika jamii za Pokot na Marakwet ili kusaidia kulinda maeneo yao dhidi ya uvamizi wa magenge ya mataifa jirani. Leo hii serikali inajaribu bila mafanikio kuzipokonya jamii hizo budnuki hizo. Tuko na visa katika askari wa akiba ambapo serikali imekuwa mara kwa mara ikitwaa bunduki hizo kwa msingi wa ukosefu wa uwajibikaji katika matumizi. Pia, serikali kwa sasa iko mbioni kusajili upya wote walio na leseni za kibinafsi za kumiliki bunduki,” asema Bw Munyoki.