Makala

MWITHIGA WA NGUGI: Tunabomoa ndoto ya Kenya kwa kuupa ufisadi kiti

March 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWITHIGA WA NGUGI

KUWEPO kwa uadilifu katika taifa lolote lile hususan kwa viongozi na wafanyakazi wa umma, kwa hakika huwa ndiyo mwanzo wa maendeleo na ustawi kwa taifa husika, lakini kinyume cha uwepo huu huwa ni kuukaribisha umaskini na kukinyofoa chochote kilicho chema kwa wananchi.

Ni wazi kwamba taifa letu limekuwa likipitia kwenye masaibu mengi, sakata za kila aina, ufujaji wa pesa za umma na ufisadi unaoonekana kuzidi kuongezeka kila uchao.

Kenya ina matatizo mengi, vijana wengi hawana kazi na mitaani hakukaliki wala kupitika kwa sababu ya ukosefu wa usalama, na badala ya kuanza kuyatatua matatizo kama haya ambayo tayari yamekuwa mzigo mzito kwa Wakenya, tunachoendelea kusikia ni kuibwa kwa mamilioni kama si mabilioni ya pesa za mlipa ushuru.

Tenda za serikali zinapotolewa, tumesikia minong’ono kutoka hapa na pale kuhusu jinsi wengine wanazitoa kwa misingi ya kujuana na hata wengine kupokezwa tenda za mamilioni ya pesa hata kama bei zao ni za juu kiasi gani kuliko za wengine, lakini kumbe mkono wa rushwa huwa unasalimiana kwa siri na kuwafanya wachache wenye nguvu kuvuna mamilioni ya pesa wasikopanda na kuwafanya mamilionea kwa madakika?

Lakini ama kweli nauliza, uadilifu na uzalendo ulikwenda wapi jamani katika taifa letu? Si kwa mara moja tumesikia serikali ikiuziwa ‘hewa’ na watu watajika na hela nyingi kupotea, mara mashirika ya kiserikali yakinunua kisichokuwepo na kwa hivyo hazina ya serikali kuendelea kuchumwa usiku na mchana na wenye nguvu na uwezo.

Ni wazi kwamba rais wetu amekuwa katika mstari wa mbele kwenye vita dhidi ya ufisadi, huku akitoa maneno makali kwa wote wanaojihusisha na saratani hii ya ufisadi, inayowanyima Wakenya wengi maendeleo na maisha bora.

Jinsi mambo yanavyoendelea kwa sasa ni kama kasi na makali tulioanza nayo dhidi ya ufisadi, inazidi kudidimia na kupata vikingi vingi njiani hususan tunapokaribia kuwanasa vigogo wakuu wa ufisadi.

Kujikosea

Kama taifa tutakuwa tunajikosea kwa kuuvumilia ufisadi na wafisadi na kamwe hatutakuwa tofauti na mtu anayehiari kumtunza na kumlisha chatu mvunguni mwake, akisahau kwamba mwishowe atageuzwa kuwa kitoweo cha yule yule chatu!

Ada ya mja kunena muungwana ni vitendo, wanachohitaji kuona Wakenya ni maneno ya rais yakifanywa tufani ya kuyakomoa majizi yote ya pesa na mali ya umma na kuyazima milele.

Wakenya wote kwa jumla hawafai kukaa kimya wakati maovu ya kiuchumi yanapoendelea kutanda na kuyatema mate yake kama bafe kwenye hazina zetu za maendelea na kuzibeza sheria zetu za nchi. Kwa kifupi, lisemwalo lipo na kama halipo laja.

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]