Rashid Echesa: Waziri aliyetemwa nje
Na MWANGI MUIRURI
RASHID Echesa Mohammed ambaye alipigwa kalamu kutoka baraza la mawaziri la Rais Uhuru Kenyatta atakumbukwa kama aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Michezo na Masuala ya Vijana na kuwapa vijana motisha kuwa haijalishi hali maishani, yawezekana.
Itakumbukwa aliingia serikalini akibeba elimu ya darasa la saba.
Siku ya siku alisoma kiapo chake cha huduma kwa lugha ya Kiingereza na akavuka salama lile jina linalohangaisha wengi kulitamka – “conscientious” ambalo lina maana huduma ya bidii ya kujitolea.
Kwa hakika alilitamka kwa ufasaha akilinganishwa na Waziri wa Mazingira ambaye ni Keriako Tobiko.
Alipoingia serikalini, alionekana wazi kutelekeza majukumu yake rasmi na akawa wa kunaswa katika visa vya kila aina, mara kwa mara akipapurana na walionekana kumpinga Naibu Rais, William Ruto na ari yake ya kuwa Rais baada ya 2022, akawa wa kuonekana akitukana viongozi wa eneo la Magharibi kama Mzee Francis Atwoli kwa misingi ya kutofautiana kisiasa na la mno, jina lake likaanza kujipenyeza katika madaftari ya ufisadi mkuu, hali ambayo inathibitishwa na baadhi ya vitengo vya usalama kuwa inamulikwa kwa nia ya kumnasa hadi mahakamani.
“Ndio, tunamfuata huyu waziri wa zamani kuhusiana na kashfa kadha. Kuna madai kuwa anahusika kikamilifu na kashfa ya uhifadhi pesa kwa vitita vikubwa kinyume na sheria za Benki Kuu ya Kenya (CBK), anahusishwa na uidhinishaji haramu wa maharamia hapa nchini na pia ufisadi mwingine ambao kwa sasa unachunguzwa ili kuupa taswira kamili
ya kuandaliwa mashtaka,” kachero mmoja katika idara ya uchunguzi wa Jinai (DCI) akafichulia Taifa Leo Dijitali.
Ingawa kufutwa kazi kwake kulipokelewa kwa hisia mseto, wengine wakishabikia huku wengine wakizindua awamu za ucheshi kuhusu Echesa mitandaoni, mmoja akiandika kuwa “Rais Kenyatta amefuta kazi mshukiwa wa ufisadi aliye na elimu duni na wa umri mdogo katika baraza lake na kuwahifadhi washukiwa walio na elimu na wenye umri wa juu,” yote tisa, la kumi ni kuwa kwa sasa imekuwa, hayuko kazini.
Ukimcheka na uulizwe wewe na elimu yako yote ulipitwa wapi akiteuliwa utajibu namna gani?
Hali kamili ya kuteuliwa kwake iko katika ueledi wake wa kuratibu masuala ya kisiasa mashinani na ambapo alikuwa akisakwa kwa undi na uvumba na mirengo yote ya kisiasa hapa nchini ajumuike katika kuipigia debe hasa katika eneo la Magharibi.
Aliletwa ndani ya serikali na Uhuru Kenyatta na William Ruto kupokezwa shukran za kusaidia Jubilee kutwaa nyadhifa nane katika eneo hilo la Magharibi ambako alizaliwa na kulelewa ndani ya umasikini mkuu.
Huku akiwa alihudumu kwa wakati mmoja kama bebabeba katika kampuni ya sukari ya Mumias, Echesa pia alipigana masumbwi kujipa riziki na pia kusaidia wazazi wake na watoto wao wengine saba.
Aligunduliwa na utawala wa Rais mstaafu Mwai Kibaki mwaka wa 2007 ambapo alipewa majukumu ya kushirikisha kampeni za Party of National Unity (PNU) katika eneo bunge la Mumias na mara moja akadhihirisha uwezo wake ambapo licha ya kuwa ngome kali ya mrengo wa Raila Odinga, mzee Kibaki alikusanya kura 18,000 eneo hilo.
Utawala huo haukumfaa kwa tuzo Bw Echesa na ndipo alirejelea mahangaiko yake ya kimaisha ingawa alichuna mtaji si haba wa kumfaa kutoka harakati hizo.
Mambo yalibakia kimyakimya kwa Echesa hadi 2013 alipojiunga na mrengo wa Odinga na akawania udiwani wa Mumias na akapoteza.
Hata hivyo, alibakia kuwa kinara wa mrengo wa vijana ndani ya mrengo wa Odinga, akiwa kutoka ukoo maarufu wa Nabongo Mumia ambao hujulikana kwa ujasiri mkuu katika harakati za kimaisha.
Alioa mke mwaka wa 2007 na akabakia katika harakati za kisiasa hadi mwaka wa 2016 ambapo aliyekuwa gavana wa Bungoma, Ken Lusaka akisaidiana na William Ruto walimnyemelea na wakamshawishi kujiunga na Jubilee na akakubali.
Huku Odinga na wakereketwa wake wakiwa bado hawajang’amua ukweli wa mambo, wakidhania Achesa kuwa bado alikuwa katika kapu lao la mawindo, walikuja kushangaa mchana tena hadharani.
Walifululiza hadi eneo hilo la Mumias kucheza siasa na kisa ambapo msako wa polisi mkali ulikuwa umeshuka eneoi hilo kusaka bunduki ambazo zilikuwa zimeibwa kutoka kwa serikali.
Odinga akiandamana na gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya na wengine walikumbana na Achesa akiwa na kundi la vijana na wakifikiria kundi hilo lilikuwa hapo kuwalaki, dunia ikapasuka nusura imeze Odinga na wenzake.
“Wewe Odinga umekuja hapa na stori gani? Unataka kutwambia nini ilihali unajua vizuri msako huu ni wa kusaka majambazi wala sio watiifu kwa sheria? Unataka kuja hapa kutetea wezi wanaotuhangaisha? Majambazi wamekuwa wakipiga wenyeji na kubaka wanawake wetu kwa muda sasa. Mbona hukuja kuteta wakati huo?” Achesa akamuuliza Odinga.
Punde kidogo, ikawa ni dhahiri kuwa ni lazima Odinga na wenzake wangejitoa eneo hilo haraka iwezekanavyo kwa kuwa kundi la Achesa lilikuwa limezindua njama ya kuwashambulia.
Odinga akang’amua kuwa mbwa wake wa mawindo alikuwa amehamishia imani yake kwa UhuRuto.
Kando mwa Achesa walikuwa ni wabunge Benjamin Washiali wa Mumias Mashariki na yule wa Navakholo, Emmanuel Wangwe.
Historia
Hayo mengine ni historia kwa kuwa Echesa alishikana na wandani wa Jubilee eneo hilo, wakafadhiliwa vya kutosha na matokeo ikawa ni Jubilee kung’aa kinyume na ilivyokuwa ikidhaniwa na kwa hilo, Lusaka licha ya kupoteza ugavana Bungoma ndiye Spika wa Seneti huku Washiali akiwa ni kiraja wa Jubilee bungeni.
Echesa ndiye huyo ambaye kufikia Machi 1, 2019, ambapo ameonyeshwa mlangao, alikuwa ndani ya suti afisini akiwa ni Waziri wa Michezo na Utamaduni mshahara wake ukiwa ni Sh924,000 kwa mwezi, ongeza marupurupu ya hapa na pale na ya ziada ambayo haikosi hapa na pale katika nyadhifa hizi.
Miaka kadhaa iliyopita alikuwa akilipwa Sh3,000 na kuangalia familia yao ikisombwa na umaskini.
Kwa sasa, anasema kuwa ukwasi wake ni wa takriban Sh40 milioni.
Kwa sasa, ana kampuni yake inayofahamika kama Aust and Oust International Limited aliyoizindua mwaka wa 2008 baada ya kumalizana na kampeni za mzee Kibaki.
Wakati huo ikiwa na wafanyakazi watatu pekee, yeye akiwa mmoja wao, leo hii iko na wafanyakazi 200.