Makala

DAU LA MAISHA: Anawapa tabasamu kina mama na vijana

March 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

KWA takriban miaka minane amekuwa kimbilio la wanawake na vijana walio katika hatari ya kuambukizwa maradhi ya Ukimwi.

Ni kazi ambayo Edith Kamau, 43, amekuwa akiiendesha kupitia Moyote, mradi aliouanzisha kwa ushirikiano na Jane Mukami na ambao umewapa nafuu wakazi wa vitongoji duni mbalimbali katika mtaa wa Kariobangi, jijini Nairobi.

Tangu kuanzishwa kwake takriban miaka minane iliyopita, mradi huu umekuwa msaada kwa wakazi wa sehemu hii na hasa walioathirika au walioambukizwa virusi vya HIV.

“Huduma zetu zajumuisha mafunzo kuhusu virusi vya HIV, kuhamasisha jamii, kuwapa wakazi uwezo wa kujisimamia kiuchumi na unasihi,” aeleza Bi Kamau.

Hasa, mradi huu umekuwa ukishughulikia wasichana walio katika umri wa kubalehe na wanawake walio katika hatari ya kuambukizwa virusi vya HIV.

Pia wamekuwa wakiwahudumia wanawake wanaokumbana na dhuluma za kinyumbani kutokana na umaskini na kiwango duni cha masomo.

“Tunawafunza kutambua haki zao hasa za afya ya uzazi, dhuluma za kijinsia, jinsi ya kujikinga dhidi ya virusi vya HIV, miongoni mwa mambo mengine,” aeleza.

Aidha wanatoa mafunzo ya kusaidia wahusika kujisimamia kiuchumi na hata kuwapa msaada wa kifedha kuanzishia biashara.

Mbali na hayo, wamekuwa wakikusanya visodo na kugawia wasichana katika shule mbalimbali ili kuhakikisha kwamba hawasusii masomo wakati wa hedhi. Na matokeo ya huduma zao yanazidi kuhisiwa katika sehemu nyingi mtaani humu.

“Tangu tuanze, idadi ya wasichana wanaosalia shuleni wakati wa hedhi imezidi kuongezeka huku takriban wasichana 500 wakinufaika na mradi huu,” aeleza.

Mbinu za kujitegemea

Aidha, familia nyingi zimebuni mbinu za kujitegemea kifedha huku zaidi ya wakazi 2000 wakinufaika kwa njia moja au nyingine.

“Kuna visa vya wanawake wanaojipata katika hatari ya kuambukizwa virusi ilhali sio kupenda kwao kwani wanajitafutia riziki. Kwa mfano kuna mwanamke aliyeshurutishwa na mumewe kuingilia ukahaba ili kupata pesa za kukidhi mahitaji ya familia yao. Ili kumuepusha na janga hili, tulimpa mafunzo na hata kumpa mtaji wa kuanzishia biashara,” aeleza.

Pia, wanashughulikia mayatima waliaochwa baada ya wazazi wao kufariki kutokana na Ukimwi.

“Kwa mfano kuna kisa cha mtoto aliyezaliwa na virusi vya HIV, na ambaye alikuwa ametelekezwa na jamaa zake baada ya kuachwa yatima. Ilitubidi kuingilia kati ili amalize shule ya msingi na kujiunga na kidato cha kwanza,” aeleza.

Anasema kumtambua anayehitaji usaidizi, wao hasa hutegemea taarifa kutoka kwa jamii.

“Hata hivyo lazima tuthibitishe kuwa mhusika kwa kweli ni mhitaji. Lazima adhihirishe yumo katika hatari ya kuambukizwa HIV au kudhulumiwa kijinsia,” asema.

Bi Edith Kamau. Picha/ Kanyiri Wahito

Bi Kamau asema msukumo ulitokana na kugundua kuwa vijana na hasa wasichana katika umri wa kubalehe walitatizika kufikia huduma za afya ya uzazi, vile vile ushauri.

“Pia kwa upande wangu nilipitia maisha magumu suala lililonifanya nioelewe mapema. Mwenzangu naye alikuwa na uzoefu wa kufanya kazi na wanawake wa umri tofauti, na hivyo tukaamua kuungana kuanzisha jukwaa kushughulikia masuala hayo,” asimulia.

Kwa sasa huku wakitumai kuendelea kubadilisha hali ya maisha ya wakazi wa mtaa wao, wanapania kupanua huduma zao kote jijini Nairobi.