• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 PM
JAMVI: Muungano mkuu wanukia baada ya Moi, Raila kukutana

JAMVI: Muungano mkuu wanukia baada ya Moi, Raila kukutana

Na BENSON MATHEKA

MKUTANO wa kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, na mwenyekiti wa chama cha Kanu Gideon Moi mapema wiki hii umezidisha kauli za washirika wao na wadadisi kwamba kuna mipango ya kuunda muungano mkubwa wa kisiasa kabla ya 2022.

Hata hivyo, wadadisi wanasema iwapo muungano huo utaundwa huenda ukatatizika kuteua atakayepeperusha bendera yake kwenye kinyanganyiro cha urais 2022 iwapo hautaweka msingi imara.

Bw Odinga na Bw Moi walikutana kwa saa nne katika mkahawa mmoja jijini Nairobi kwa kile ambacho wandani wao walisema ilikuwa kujadili masuala yanayoathiri Wakenya na kutafuta mbinu za kuunganisha Wakenya.

Wandani wao wamekuwa wakidokeza kuwa huenda wakaungana na viongozi wengine kubuni muungano wa kisiasa utakaoteua mgombeaji mmoja wa urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Miongoni mwa waliotajwa kuwa katika muungano huo ni Bw Kalonzo Musyoka na chama chake cha Wiper, kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, Bw Odinga wa chama cha ODM, Gideon Moi wa chama cha Kanu na mrengo mmoja wa chama cha Jubilee unaoegemea upande wa Rais Uhuru Kenyatta.

Mbunge wa Tiaty William Kamket alikuwa wa kwanza kudokeza kuundwa kwa muungano huo mwaka jana aliposema kwamba Kanu inazungumza na vyama vingine kwa lengo la kubuni muungano utakaotoa mgombeaji mmoja wa urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

“Tunajadiliana na ODM, Wiper, ANC na mrengo mmoja wa chama cha Jubilee ambao hautakuwa na mgombeaji wa urais katika uchaguzi wa 2022,” Bw Kamket alinukuliwa akisema.

Bw Musyoka pia amekuwa akidokeza kuwa kuna mipango ya kuunda muungano mkubwa wa kisiasa kwa lengo la kuunganisha Wakenya kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Akizungumza akiwa Gatanga mwishoni mwa wiki, Bw Musyoka alisema kwamba viongozi wameamua kuweka kando tofauti zao za kisiasa kwa lengo la kuunganisha nchi. Ilikuwa mara ya tatu kwa Bw Musyoka kudokeza hadharani kwamba kuna mipango ya vyama vikuu nchini kuungana kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Mara ya kwanza ilikuwa alipomtangaza mgombeaji wa chama hicho kwenye uchaguzi mdogo wa kiti cha eneobunge la Embakasi Kusini na ya pili ilikuwa kwenye kongamano la chama cha Wiper ambalo lilifanyika Februari 8 eneo la Koma, Machakos.

Wadadisi wanasema kwamba muungano unaokusudiwa kuundwa unatokana na muafaka kati ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta ambao walisema unalenga kuunganisha Wakenya.

Hata hivyo, wanasema huenda baadhi ya wanasiasa wanaounga mkono muungano huo wakajipata pabaya iwapo hawataweka mikakati kabambe ya kutimiza azma zao.

“Kwa sasa, muungano unaozungumziwa unatokana na moyo wa handisheki na kwa msingi hewa kwamba kutakuwa na mabadiliko ya kikatiba ili kubuni nafasi zaidi serikalini kama vile wadhifa wa waziri mkuu, manaibu wake na kiongozi rasmi wa upinzani,” asema mdadisi wa siasa Geff Kamwanah.

“Ni msingi hewa kwa sababu hakuna anayefahamu siri ya Bw Odinga na Rais Kenyatta ambaye kulingana na katiba ilivyo, anahudumu kipindi chake cha mwisho na iwapo hakika katiba itafanyiwa marekebisho,” asema.

Kulingana na mdadisi huyu, ni Bw Mudavadi ambaye anaonekana kuchukua mwelekeo tofauti wa kisiasa kujiimarisha kabla ya 2022.

“Wengine ni sawa na wasafiri wanaopanga kuabiri meli ambayo haijaundwa. Kila aliye na azma ya kugombea urais anafaa kujipanga vyema badala ya kutegemea kuungana na wengine wampige jeki,” asema.

Wadadisi wanasema iwapo katiba haitarekebishwa au marekebisho yataenda kinyume na matarajio ya wanasiasa hao, basi baadhi yao wanaweza kujikwaa kisiasa.

Wanaopigia debe muungano huo wanasema kwamba wanataka siku zijazo, serikali iwe ikishirikisha Wakenya wote badala ya hali ilivyo kwa sasa ambapo serikali huwa ya chama na jamii chache zilizounga mkono chama kinachoshinda uchaguzi.

Wadadisi wanasema kwamba mkutano wa Bw Odinga na Bw Moi unafuatia wa mwaka jana ambapo kiongozi huyo wa chama cha ODM alimtembelea rais mstaafu Daniel Moi, nyumbani kwake Kabarak.

Hii ilikuwa muda mfupi baada ya handisheki na wadadisi wanasema kuna uwezekano Bw Odinga na Rais Kenyatta walizungumzia muungano wa kisiasa kabla ya 2022 kwenye mazungumzo yaliyotangulia kusalimiana kwao mnamo Machi 9, 2018.

Bw Musyoka pia alimtembelea Mzee Moi. Bw Moi na chama chake cha Kanu walikuwa wakimuunga Rais Kenyatta kwenye uchaguzi mkuu uliopita ambaye mpinzani wake mkuu alikuwa Bw Odinga.

“Inaonekana Gideon na Odinga wanakubaliana katika masuala kadhaa yakiwemo matatizo yanayokabili nchi. Wanataka kuwa sehemu ya suluhu ya changamoto zinazokabili nchi kupitia moyo wa handisheki,” akasema mbunge mmoja mwandani wa Bw Odinga.

Kulingana na mdadisi wa masuala ya kisiasa, Baariu Mathiu, inawezekana viongozi kubuni muungano wa kisiasa usiokuwa na lengo ya kusaidia Wakenya.

“Muungano wa kisiasa ambao ninaona ni wa familia zinazojichukulia kuwa za kifalme au familia za viongozi kwa lengo la kugawana mamlaka kuendelea kukandamiza Wakenya,” asema Bw Mathiu.

“Ukifuatilia kwa makini utagundua kwamba wanasiasa kutoka familia za waliokuwa wanasiasa maarufu miaka ya awali ya uhuru ambao wamekuwa wakikutana kupanga jinsi ya kuungana,” asema.

You can share this post!

WASONGA: Tamko la Ruto ni hatari katika vita dhidi ya...

JAMVI: Urafiki wa Uhuru na Maraga unavyotisha kuzima uhuru...

adminleo